MIEZI mitatu baada ya kinachoitwa, “mauaji ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba,” mwaka jana, bado familia nyingi nchini Tanzania, hazijaweza kupata miili ya wapendwa wao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wapo ambao hawajakata tamaa na hivyo wanaendelea kuhangaika kutafuta miili ya wapendwa wao waliopotea. Lakini baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema, “huenda walizikwa kwenye makaburi ya pamoja.”
Mwandishi wa habari, Manenos Selanyika (40), ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika vurugu hizo.
Kwa mujibu wa majirani waliyozungumza na familia yake, Selanyika alipigwa risasi jijini Dar es Salaam na vikosi vya usalama, tarehe 30 Oktoba, wakati alipotoka kutafuta chakula.
Hata hivyo, juhudi za familia yake kuuchukua mwili wake zilikwamishwa na polisi.
Ndugu walimtafuta katika hospitali kadhaa jijini Dar es Salaam, bila mafanikio, na baada ya zaidi ya wiki moja bila taarifa yoyote rasmi, walilazimika kufanya mazishi ya kiishara katika kijiji cha Lambo, karibu na Mlima Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani (DW), mashirika ya haki za binadamu yanasema mamia ya familia nchini Tanzania ziko katika hali kama hiyo, huku serikali ikikabiliwa na tuhuma za kuwazika waathirika wa ghasia katika makaburi ya pamoja kwa siri – madai ambayo serikali imeyakanusha.
Vurugu hizo zilichochewa na kufungiwa kwa wagombea wa upinzani, ukosefu wa usawa kwenye uchaguzi, mifumo inayopendelea chama tawala na mengine ya aina hiyo, pamoja na kushamiri kwa vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji kwa wakosoaji wa serikali.
Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi wa urais.

Alipata asilimia 98 ya kura, baada ya siku tano za ghasia ambazo upinzani unadai zilisababisha vifo vya takribani watu elfu mbili, huku huduma za mtandao zikiwa zimezimwa kote nchini.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Rais Samia aligusia vurugu za baada ya uchaguzi bila kutaja idadi ya waliouawa.
Alisema: “Kwa washirika wetu katika jumuiya ya kidiplomasia na wageni wanaoishi hapa Tanzania, natoa pole zangu za dhati kwa hali ya kutokuwa na uhakika, usumbufu wa huduma, na kuzimwa kwa intaneti. Tunatambua changamoto za machafuko na vurugu zilizojitokeza siku ya uchaguzi na muda mfupi baada ya hapo.
“Hatua tulizochukua zilikuwa muhimu ili kulinda utaratibu wa kikatiba na kuhakikisha usalama wa wananchi wote pamoja na jumuiya ya kidiplomasia.”
Lakini serikali haijatoa takwimu rasmi za vifo. Shirika la habari la AFP, lililoripoti matukio haya, limesema serikali haikujibu maswali yaliyowasilishwa kuhusiana na madai hayo.
Katika tukio jingine, mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Sheila Gyumi, ambalo siyo jina ambalo si lake halisi, amenukuliwa akisema, mume wake, aliyekuwa dereva wa bodaboda, alitoweka siku ya uchaguzi alipokwenda kazini kama kawaida.

Hadi sasa, familia haijui alipo, hali iliyomwacha mjane huyo akihangaika kugharamia kodi ya nyumba na ada ya shule ya mtoto wao.
Daktari mmoja katika hospitali kubwa jijini Dar es Salaam aliwahi kuiambia AFP kuwa mamia ya miili ilichukuliwa kutoka mochwari na maafisa wa usalama wakati wa kilele cha machafuko.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), Padre Charles Kitima, ameripotiwa akisema, vyombo vya usalama vilishinikiza uongozi wa hospitali zinazomilikiwa na kanisa hilo, ili kupewa majeruhi waliokuwa wanatibiwa. Alisema, serikali iliagiza wote waliojeruhiwa wasitibiwe.
Uchunguzi wa shirika huru la Centre for Information Resilience umeonyesha dalili za matumizi ya risasi za moto na uwezekano wa kuwepo kwa makaburi ya pamoja kupitia uchambuzi wa picha za satelaiti.
ZINAZOFANANA
Tamko la ACT Wazalendo juu ya maamuzi ya kesi ya uchaguzi
Mvutano wa kisheria SMT/SMZ kuamuliwa
EACOP yakabidhi madarasa, vyoo vya kisasa Nzega kupitia Mkandarasi Wasco Isoaf