January 27, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tamko la ACT Wazalendo juu ya maamuzi ya kesi ya uchaguzi

MAHAKAMA Kuu ya Zanzibar (Masjala Kuu Tunguu) mbele ya Jaji Haji S. Khamis imetoa uamuzi wa kihistoria lakini wenye kusikitisha, kufuatia Pingamizi la Serikali (Preliminary Objection) lililokuwa linahoji mamlaka ya mahakama hiyo kusikiliza mashauri ya uchaguzi wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa majimbo ya Zanzibar.

Katika uamuzi wake, Jaji amekubaliana na hoja ya Serikali kuwa Mahakama Kuu ya Zanzibar haina uwezo (Jurisdiction) wa kusikiliza mashauri hayo, na kwamba mwananchi wa Zanzibar anayetaka kupinga matokeo ya Ubunge hana budi kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania Bara.

  1. Uamuzi Huu Unamaanisha Nini Kwa Zanzibar?

ACT Wazalendo inapenda kuufahamisha umma kuwa uamuzi huu si wa kisheria tu, bali ni pigo kwa hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano:

    1. Mahakama Kuu Zanzibar Imepunguzwa Nguvu: Kwa uamuzi huu, Mahakama yetu imejivua mamlaka ya kutoa haki kwa wananchi wake katika ardhi yake. Inasikitisha kuona chombo kikuu cha utoaji haki Zanzibar kikikubali kuwa “hakina meno” mbele ya masuala ya Muungano yanayofanyika hapa hapa Zanzibar.

    1. Kudhalilishwa kwa Katiba: Uamuzi huu unashindilia msumari kwenye hoja kuwa Zanzibar ni “mkoa” tu ndani ya Muungano na si nchi yenye mamlaka kamili ya Kimahakama kama inavyotambuliwa na Kifungu cha 93(1) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.

    2. Haki Imewekwa Nyuma ya Bahari: Wazanzibari sasa wamelazimishwa kuwa ikiwa kura zao zitaibiwa au kukiukwa, haki yao haipo Tunguu wala Vuga, bali ipo Dar es Salaam au Dodoma. Hii ni kuminya upatikanaji wa haki kwa makusudi.

  1. Hatima ya Mashauri ya Uchaguzi

Uamuzi huu unamaanisha kuwa kesi zote za Wabunge zilizofunguliwa na wagombea wetu zimefutwa kwa hoja ya kiufundi bila hata kusikilizwa kwa hoja za msingi za wizi wa kura na ukiukwaji wa kanuni. Huu ni mkakati wa makusudi wa kisheria wa kuwalinda washindi haramu.

  1. Hatua Zitakazofuata

ACT Wazalendo haitakubali dhuluma hii ipite bila kupingwa. Tayari tumewaelekeza mawakili wetu kuanza mchakato wa kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ili kupinga tafsiri hii finyu ya sheria inayodhalilisha Mahakama ya Zanzibar.

  1. Wito wetu kwa Wazanzibari:

Huu ni wakati wa utulivu lakini pia ni wakati wa kutafakari mustakabali wa nchi yetu. Haki inapokosekana mahakamani, inabaki mioyoni mwa watu. Tutasimama kidete kuhakikisha kuwa Zanzibar haidunishwi na kuwa haki ya mpiga kura haipotei kwa kivuli cha “Mamlaka ya Mahakama.”

Imetolewa na:

Salim A. Bimani,

Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma, Chama cha ACT-Wazalendo

27 JANUARI, 2026.

About The Author

error: Content is protected !!