MAHKAMA Kuu ya Zanzibar inatarajiwa kuamua kesho mvutano wa kisheria uliopo kati ya Mawakili wanaomwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na upande unaolalamikia matokeo ya uchaguzi wa wabunge Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Itakuwa zamu ya Jaji Haji Suleiman Tetere ambaye tarehe 17 Januari alikamilisha usikilizaji wa hoja ya kwamba mahkama kuu ya Zanzibar haina uwezo wa kusikiliza kesi za ubunge iliyowasilishwa na mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMT. Alipomaliza usikilizaji aliakhirisha kesi na kupanga kutoa uamuzi mdogo tarehe 27 Januari.
Mawakili wa AG-SMT wakiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Alan Shija, waliieleza Mahakama Kuu inayoketi Tunguu nje ya mjini Zanzibar, kuwa hoja yao inazingatia muongozo unaotolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Akikazia hoja yao, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nalindwa Sekimanga, alieleza kuwa Ibara ya 83{1} ya Katiba hiyo na vifungu vyake {a} na {b}, vinatamka wazi kuwa masuala yanayohusu uteuzi na uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano yatashughulikiwa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakili huyo alidai yeyote anayehitaji kulalamikia uchaguzi wa ubunge, kama walivyoomba walalamikaji walioko Zanzibar, anawajibika kisheria kufuata maelekezo hayo, afungue shauri mbele ya mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anaeleza kuwa pamoja na katiba hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutambua kuwepo Mahakama Kuu ya Zanzibar, haijaitaja au kuipa mamlaka ya kushughulikia jambo lolote linalohusu malalamiko ya matokeo ya uchaguzi unaosimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi {INEC}.
Hoja hii iliibuliwa mahkamani tarehe 6 Januari 2026, pale kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika majimbo 19 ya Unguja zilipotajwa. Ilikuwa ni baada tu ya Jaji Tetere kutoa uamuzi mdogo ulioridhia hoja ya awali ya upande wa walalamikaji iliyotaka wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ wazuiwe kumwakilisha mwanasheria mkuu wa SMT kwenye kesi hizo kama ilivyowasilishwa na Wakili wa walalamikaji, Omar Said Shaaban.
Mlalamikiwa namba moja kwenye kesi hizo ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania {INEC} ya mwaka 2024 ambayo ndiyo inayoendesha na kusimamia uchaguzi wa Rais wa Tanzania, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Madiwani wa Tanzania Bara.
Wakili Omar anawakilisha walalamikaji kwenye majimbo 19 ya kisiwani Unguja wanaotaka matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025 yatenguliwe. Kesi nyengine 14 zilizofunguliwa mahakama hiyohiyo ya Zanzibar kisiwani Pemba, zimeunganishwa wiki iliyopita baada ya Jaji Haji kuridhia pande zote kuwa itahifadhi muda na mtiririko katika usikilizaji.
Akijibu hoja za upande wa Jamhuri, Wakili Omar alieleza kuwa anahofia kuwa wanasheria wenzake wamechukua tafsiri isiyo sahihi wanavotaja Ibara ya 83 ya Katiba ya Muungano. Anadai ni muhimu kwanza kuisaidia mahakama kuelewa maana ya hiyo tafsiri iliyofanywa na wanasheria wenzake, na mahkama ijue hayo mamlaka yanayobishaniwa yanatokana na nini hasa.
Akataja suala hilo kuwepo kwenye jarida la kisheria la England, Toleo la Nne, Fungu la Kumi, aya ya 314. Tafsiri hiyo imekutwa wakati wa kuamua rufaa iliyomhusu Paul John Muhozya dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Muungano.
Alidai ni msimamo wake kuwa suala la mamlaka ya Mahakama Kuu ya Zanzibar halitokani na fadhila ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali Katiba ya Zanzibar ambayo inaitambua mahkama hiyo na kuipa mamlaka yasiyo na mipaka na wajibu wa kusikiliza mashauri ya aina yoyote – ya jinai na mengineyo.
Kifungu cha 93 kinaitambua Mahakama Kuu ya Zanzibar kuwa yenye mamlaka ya kutoa maamuzi yanayofaa kuwa kumbukumbu. Alidai kuwa kifungu tatu kinaeleza mamlaka hayo yataendelea kuwepo na kwa hivyo yatakuwa yasiyo na mipaka kusikiliza na kuamua jambo lolote la kisheria lililowasilishwa kwa mujibu wa sheria inayotumika Zanzibar.
ZINAZOFANANA
EACOP yakabidhi madarasa, vyoo vya kisasa Nzega kupitia Mkandarasi Wasco Isoaf
Ujumbe wa rambirambi wa Lissu kwa Mzee Edwin Mtei
EACOP, REA kunufaisha wakazi waliopitiwa na bomba la mafuta