Tundu Lissu akiwa mahakamani
UJUMBE WA RAMBIRAMBI WA TUNDU ANTIPHAS LISSU KUFUATIA KIFO CHA MZEE EDWIN ISAAC MBILIEWI MTEI
EDWIN MTEI:
MJENZI WA NCHI, KIONGOZI WA MFANO
Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe na wanafamilia wa marehemu Edwin Mtei,
Viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ndugu wananchi, waombolezaji, mabibi na mabwana;
Nimepokea taarifa za kifo cha Mwenyekiti Mwanzilishi na Mwasisi wa Chama chetu, marehemu Edwin Isaac Mbiliewi Mtei kwa masikitiko makubwa. Katika hili nafikiri sitakosea nikisema kwamba siko peke yangu. Hata hivyo, naombeni mniruhusu niwape pole nyingi watoto, wajukuu, ndugu na wanafamilia wa marehemu Mzee Mtei. Salamu hizi za rambirambi zinawahusu pia viongozi, wanachama na wafuasi wote wa CHADEMA popote walipo katika nchi yetu na nje ya nchi. Aidha, Mzee Mtei alisimama katika mstari wa mbele kabisa katika harakati za ujenzi wa nchi yetu; kwa sababu hiyo, salamu hizi ziwafikie pia wananchi wote wa Tanzania katika ujumla wao.
Maandiko Matakatifu yanatufundisha katika Zaburi 90:10, kwamba “miaka ya kuishi ni sabini, au tukiwa wenye afya, themanini…” Mwenyezi Mungu alimbariki marehemu Mzee Mtei kwa kumpa ziada
ya miaka ishirini na nne (24) katika gawio lake la kawaida la miaka ya hapa duniani; na alimzidishia miaka kumi na minne katika nyongeza yake ya miaka kumi kwa wenye afya.
W.E.B Dubois, kiongozi wa harakati za ukombozi wa Waafrika duniani, aliandika katika kusherehekea miaka tisini ya kuzaliwa kwake kwamba “…kama kuishi hakukupi thamani, busara na maana ya maisha, basi hakuna sababu yoyote ile ya kuishi.”
Miaka tisini na nne (94) ya maisha ya marehemu Mzee Mtei yalitupa thamani kubwa, yalijaa busara tele na yalikuwa na maana kubwa. Naomba nikope maneno ya Amiri bin Sudi, au kwa jina lake maarufu ‘Andanenga’, mtenzi na mshairi maarufu wa Kiswahili, pale aliposema: Mzee Mtei …. “alisheheni sifa nyingi sana, njema zisizo idadi, za marefu na mapana, hazipimiki kwa yadi, ilobaki sisi kushindana, dua tumuombe wadudi, ampokee Baba yetu, kwa fukisho la ubani, udi na uvumba.”
Ndugu Waombolezaji,
Marehemu Mzee Mtei alikuwa mmojawapo wa wajenzi wakuu wa misingi mikuu ya kiuchumi ya nchi yetu, hasa katika miongo miwili ya mwanzo ya Uhuru. Alikuwa mmojawapo wa wasomi mahiri wa kwanza katika fani ya uchumi wa mara baada ya Uhuru. Kwa sababu ya umahiri wake, haikuwa ajabu kwamba pale wakuu wa nchi za Afrika Mashariki walipoamua kuvunja iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, na kila nchi kuanzisha Benki Kuu yake, Edwin
Mtei aliteuliwa kuwa Gavana Mteule, hata kabla Benki Kuu yenyewe haijaanzishwa rasmi. Kwa vyovyote vile itakavyokuwa, jina la Edwin Isaac Mbiliewi Mtei litahusishwa milele na Benki Kuu ya Tanzania; jina na saini yake yalikuwa kwenye noti za kwanza kabisa kutolewa na Benki Kuu ya Tanzania kati ya mwaka 1966 na 1974; na kati ya mwaka 1978 na 1981 alipokuwa Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa nafasi yake ya Gavana wa Benki Kuu na baadae Waziri wa Fedha, Mzee Mtei alikuwa mmoja wa washiriki wakuu katika kutunga na kutekeleza sera za kiuchumi za serikali ya Mwalimu Nyerere. Historia halisi ya nchi yetu haiwezi kumtenganisha Mzee Mtei na Azimio la Arusha lililopelekea utaifishaji wa mali za makampuni na mashirika binafsi na kuanzishwa kwa mfumo wa serikali kuhodhi njia zote muhimu za uchumi, yote yakifanywa kwa jina la Ujamaa na Kujitegemea. Na wala historia ya kweli ya nchi yetu haiwezi kumtenganisha Mzee Mtei na kushindwa kwa sera hizo kuanzia miaka ya mwisho ya sabini. Alikuwa ‘jikoni’ wakati sera hizo zinaandaliwa; na alikuwa mmoja wa ‘wapishi’!
Heshima yake kuu, na mchango wake kuhusu suala hili ambalo historia ya nchi yetu itauenzi milele ni huu; Mzee Mtei hakunyamaza mara alipogundua kwamba sera za kiuchumi za serikali yake, sera alizoshiriki kuzitunga na kuzisimamia hazitekelezeki tena. Mzee Mtei alimkabili Mwalimu na kumweleza ukweli wake; kwamba sera za kiuchumi za Azimio la Arusha zilikuwa zimeshindikana kutekelezwa; akamshauri Mwalimu kubadili msimamo wake ili kwenda
sambamba na mahitaji ya nyakati na hali halisi ya uchumi wa kimataifa.
Hili halikuwa jambo jepesi. Mwaka ambao Mzee Mtei aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, Mwalimu alisema katika mahojiano na BBC kwamba, alikuwa na madaraka, kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu, ya kuwa Dikteta kama angetaka! Mfumo wa Kikatiba na kiutawala wa aina hii sio tu ulimgeuza Rais kuwa Mungu mtu, bali pia ulitengeneza mazingira mazuri ya ‘uchawa’ miongoni mwa viongozi na watendaji wa serikali na chama pekee cha siasa cha wajati huo, yaani TANU na baadaye CCM. Baadhi yenu mtakumbuka salamu rasmi za kisiasa za miaka hiyo; ‘Zidumu Fikra za Mwenyekiti wa CCM!’ Mzee Mtei alikuwa na ujasiri wa kumweleza Mwalimu, kwa heshima zote, kwamba fikra zake za kiuchumi zilikuwa zimefeli; hazikupaswa kuendelea kudumishwa!
Kwa ujasiri huo huo, marehemu Mzee Mtei aliwajibika kwa kujiuzulu nafasi pale Mwalimu alipomkatalia ushauri wake huo. Alikuwa na uadilifu wa kuona kwamba haikuwa sahihi kwake kuendelea kutumikia nchi yetu katika masuala ambayo msimamo wake ulikuwa tofauti na msimamo wa Kiongozi Mkuu wa Serikali yake. Leo hii, kwa jinsi ambavyo ‘uchawa’ kwa Rais umekuwa ni donda ndugu na umekithiri katika ngazi zote za utumishi wa umma na hata katika sekta binafsi, tunaweza kupima kiwango cha juu cha ujasiri wa Mzee Mtei na uzalendo wake kwa nchi yetu. Itoshe tu kusema, kama nyongeza, kwamba yale yote ambayo Mzee Mtei aliyapendekeza kwa Mwalimu na yakakataliwa, yalikubaliwa na kuanza kutekelezwa
Miaka miwili tu baada ya Mzee Mtei kulazimika kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Fedha! Kwa maneno mengine, ukweli wa msimamo wake ulithibitishwa kwa vitendo, licha ya yeye mwenyewe kulazimika kuwa nje ya Serikali. Kwangu mimi, hii ndio thamani na maana kubwa ya maisha marefu ya Mzee Edwin Mtei.
Ndugu Waombolezaji,
Mzee Edwin Mtei alikuwa mjenzi wa demokrasia ya vyama vingi katika nchi yetu. Na kwenye hili, kama ilivyokuwa hulka yake, aliongoza kwa mfano na kwa vitendo. Alikuwa mmoja wa Waasisi na Mwenyekiti Mwanzilishi wa CHADEMA. Leo hii, CHADEMA ndio chama kikuu cha siasa katika nchi yetu; sio CCM, kwa sababu CCM ni chama-dola, sio chama cha siasa kinachoishi kwa ridhaa na mapenzi ya wananchi na wanachama wake. CHADEMA, chama cha Edwin Isaac Mbiliewi Mtei, kinaishi kwa ridhaa na mapenzi ya mamilioni ya Watanzania kwa sababu Mzee Mtei alitufundisha kuwa utumishi wa kisiasa sio biashara au mahali pa kujipatia fedha au vyeo, bali ni huduma na utumishi kwa
wananchi.
Kama Mwenyektii Mwanzilishi, Mzee Mtei hakuwahi kupokea mshahara au posho yoyote kutoka kwa Chama. Hakuwahi kupatiwa gari au usafiri wa Chama; na wala hakuwahi kuwa diwani au mbunge wa CHADEMA. Hakuwahi kutumia uongozi wake wa Chama kujinufaisha yeye binafsi au watoto wake au ndugu na marafiki zake. Kwa Edwin Mtei uongozi ulikuwa ni dhamana, sio fursa. Alitumia
Muda wake, na mali zake na nguvu zake kukijenga Chama na kuwatumikia wanachama na wananchi wake. Na hii ndio thamani nyingine kubwa na maana muhimu ya maisha marefu ya Mzee Edwin Mtei. Thamani hii na maana hii ya maisha yake imejidhihirisha wazi katika miaka hii kumi ambapo Chama chetu, viongozi wake, wanachama na wafuasi wake tumepitishwa katika bonde la uvuli wa mauti mara kwa mara. Tumeumizwa sana, lakini tumeimarishwa sana pia, kwa sababu ya mfano wa utumishi na kujitolea aliotuwekea Mzee Edwin Mtei. Na kwa mfano huo tutashinda.
Ndugu Waombolezaji,
Mzee Edwin Mtei ametuachia urithi mwingine wenye thamani na maana kubwa kwa Chama chetu na nchi yetu. Alitumikia Chama chetu kama Mwenyekiti wake kwa kipindi kimoja tu cha miaka mitano. Ilipofika mwaka 1998, akiwa na umri wa miaka sitini na sita (66), Mzee Mtei aliamua kustaafu uongozi wa Chama ili, kwa maneno yake mwenyewe, “kupisha damu changa” kuchukua uongozi wa Chama. Kama angetaka angeweza kuendelea kuongoza Chama kwa kipindi kingine kimoja au hata viwili. Lakini, kwa Edwin Mtei, uongozi wa Chama ulikuwa ni dhamana, sio fursa ya kung’ang’ania madarakani. Na kwa sababu ya mfano wake huo, CHADEMA imekuwa na itaendelea kuwa Chama pekee chenye kubeba matumaini na ndoto za mamilioni ya wananchi wetu ya kujenga nchi yenye kujali haki, uhuru na utu na maendeleo ya kweli ya watu wetu.
Ndugu Waombolezaji,
Mambo ya kusema juu ya Mzee wetu huyu ni mengi na mazuri, hatutaweza kuyamaliza yote kwa muda mfupi tulionao leo. Naomba nimalizie salamu zangu hizi kwa jambo moja ninaloamini ni muhimu kwa nchi yetu. Jambo hili linatudhihirishia aina ya kiongozi ambaye Edwin Mtei alikuwa, na thamani na maana ya maisha yake marefu.
Kwa muda mrefu wa miaka ya uhuru, viongozi wetu wa kisiasa hawakujenga utamaduni wa
kuandika na kuchapisha vitabu na maandiko yanayohusu historia za maisha na nyakati zao baada ya kuondoka madarakani. Mwalimu Nyerere na rika lake lote la kwanza la uhuru waliondoka bila kutuachia simulizi za maisha na nyakati zao na changamoto walizokabiliana nazo kutoka kwenye midomo na kalamu zao wenyewe. Hatuna ‘autobiography’ au ‘memoirs’ za Mwalimu au Rashid Mfaume Kawawa, au za kiongozi mwingine wa rika hilo. Kwa sababu ya ombwe hili katika kumbukumbu zetu za pamoja, ufahamu wetu kama viongozi na wananchi kuhusu historia yetu wenyewe na kuhusu matukio muhimu ya historia hiyo ni ndogo na wakati mwingine haupo kabisa. Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei alitupatia mfano wa namna ya kuondokana na upofu huu wa kujitakia. Mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka sabini na saba (77), Mzee Mtei alichapisha ‘From Goatherd to Governor’ (Kutoka Mchunga Mbuzi Hadi Gavana), historia ya maisha na nyakati zake. Kwa sababu ya ‘autobiography’ hii, tumeweza kufahamu mambo mengi kuhusu nchi yetu ambayo pengine tusingeyafahamu.
Tumeweza kufahamu, kwa mfano, jinsi sera za Ujamaa na Kujitegemea zilivyoipeleka nchi yetu kwenye lindi kubwa la matatizo ya kiuchumi. Tumeweza kufahamu angalau jinsi ambavyo kiongozi mmoja mwenye ujasiri na mwadilifu alivyosimama na kumwambia Mwalimu Nyerere ukweli wa hali yetu halisi na jinsi alivyowajibika kwa sababu ya kusimamia ukweli huo.
Kwa sababu ya mfano alioonyesha Mzee Mtei, viongozi wetu wengine nao walipata ujasiri wa kuandika na kuchapisha kumbukumbu za maisha yao na nyakati zao. Mwaka 2019, marehemu Rais Benjamin William Mkapa alichapisha ‘My Life, My Purpose’ (Maisha Yangu, Kusudio Langu), ambacho, kwa kiasi kikubwa, ni utetezi wake wa miaka kumi ya urais wake. Kwa kitabu hicho, marehemu Mzee Mkapa naye alituachia maelezo yake binafsi juu ya changamoto alizokumbana nazo katika maisha yake na alivyokabiliana nazo. Pengine kiongozi aliyetupatia kumbukumbu bora zaidi za maisha ya utumishi wa umma na uongozi wa kisiasa ni ‘Mzee Rukhsa’, marehemu Rais Ali Hassan Mwinyi ambaye kitabu chake chenye kichwa hicho kilichapishwa mwaka 2022. Kitabi hicho kina hazina kubwa ya taarifa za matukio mbalimbali ya utawala wa Mwalimu Nyerere nay a utawala wa Rais Mwinyi yeye mwenyewe. Tumshukuru Mzee Mtei kwa kuwa mwasisi wa utamaduni huu mpya wa kisiasa katika nchi yetu.
Ndugu Waombolezaji,
Sasa naomba kumaliza salamu zangu hizi. Edwin Isaac Mbiliewi Mtei aliishi maisha marefu na yenye thamani, maana na mafundisho mengi kwetu. Hatupaswi kuomboleza kifo chake;
tunapaswa kusherehekea maisha yake marefu. Hatumdai chochote; alikwisha lipa madeni yake yote kwetu na kwa nchi yake na riba juu. Alivipiga vita vilivyo vizuri; aliilinda Imani yake, na sasa mwendo wake ameumaliza.
Basi tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha mema na marefu, kwa malezi bora aliyotupatia, kwa utumishi uliotukuka na adilifu wa Edwin Isaac Mbiliewi Mtei. Na sisi sote ambao maisha yetu yaliguswa na kufadhiliwa na baba yetu huyu, tuungane katika dua hii: “Ewe Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na nchi, mapenzi yako yametimia, uyasamehe makosa ya baba yetu huyu, umwangazie nuru ya uso wako, uiweke roho yake mahali pema peponi. Amina.”
Nawashukuru kwa uvumilivu wenu na Mwenyezi Mungu awape nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.
Tundu Antiphas Lissu
Gereza Kuu la Ukonga – Dar es Salaam January 2026
ZINAZOFANANA
EACOP, REA kunufaisha wakazi waliopitiwa na bomba la mafuta
Meridianbet yachochea mwamko wa usafi wa mazingira Mbezi Juu
Chadema: Muda wa zuio la kufanya shughuli za siasa umekwisha