MRADI wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Nishati Vijijini (REA) wamesaini randama ya kusambaza umeme katika vijiji vinavyopitiwa na mradi huo kwenye mikoa minane nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo jana Jumamosi jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP Tanzania, Guillaume Dulout alisema kuwa wameamua kushirikiana na REA kwa ajili ya kusaidia wananchi wanaopitiwa na bomba la mafuta, hivyo kuleta ahueni sambamba na kulinda mazingira.
“Wananchi wa maeneo haya ni wanafamilia wa mradi huu, na sisi tumepitisha umeme kwa ajili ya kusukuma mafuta kwenye bomba letu, hivyo tumeona kwa umuhimu wao kwenye bomba letu tuwasaidie kuwapatia umeme bure,” alisema Dulout.
Alisema wataanza kusambaza umeme kwa wananchi kuanzia mkoani Kagera na kuendelea mpaka mkoani Tanga kwa kuhudumia zaidi ya mitaa 17,000.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy aliipongeza EACOP kwa kuamua kuingia makubaliano ya kusambaza umeme kwa wananchi, mbali ya kunufaisha wananchi hao vilevile itasaidia utunzaji wa mazingira katika eneo zima lililopitiwa na mradi kuanzia Kagera mpaka Tanga.
“Wananchi wa maeneo haya watatumia umeme kwa ajili ya matumizi mbalimbali hususani ya kupikia, hivyo wataacha mazoea ya kutumia kuni na mkaa ambavyo vinasababisha uharibifu wa mazingira,” alisema Mhandisi Saidy.

Alisema kwamba mpango huo ni wa miaka mitano, ambapo EACOP itachangia Sh. 2.5 bilioni kwa mwaka, na REA itachangia bilioni tano kwa kila mwaka.
Naye Meneja wa Sheria wa EACOP Tanzania, Stanley Mabiti alisema kuwa mradi huo utakuwa na tija sana kwa wananchi kwani utawainua kiuchumi kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya uchakataji wa bidhaaa mbalimbali, hivyo kujiongezea kipato.
“Mradi huu unaungana na Dira ya Taifa ya 2050 ya kuhakikisha kila mwananchi anapata nishati safi ya kupikia pamoja na shughuli zake nyingine za kimaendeleo,” alisema Mabiti.
Pamoja na hayo Mabiti aliwaasa wananchi wa maeneo hayo wachangamkie fursa hiyo na fursa nyingine zote zinazotolewa katika maeneo yanayowazunguka ili kubadilisha hali za maisha yao.
“Naomba mfahamu kwamba malengo makuu ya EACOP ni kuboresha hali za kiuchumi kwa wakazi wote waliopitiwa na mradi huu kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile shule, maji, nishati na nyinginezo.
Wanahisa wa EACOP ni TotalEnergies yenye asilimia (62), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) yakimiliki asilimia 15 kila moja na kampuni ya mafuta ya Kichina (CNOOC) ikiwa na asilimia nane.
Bomba la EACOP, lenye urefu wa kilometa 1443, linaanzia Wilaya ya Hoima nchini Uganda na kuishia nchini Tanzania katika Mkoa wa Tanga. Bomba hilo limepita katika mikoa nane ya Tanzania bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
ZINAZOFANANA
Ujumbe wa rambirambi wa Lissu kwa Mzee Edwin Mtei
Meridianbet yachochea mwamko wa usafi wa mazingira Mbezi Juu
Nufaika na Meridianbet leo