March 15, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Samia: Tutafanya maridhiano 2026

Rais Samia Suluhu Hassan

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa mwaka mpya 2026, kwa msisitizo wa maridhiano ya kitaifa, akitangaza maandalizi ya Tume ya Maridhiano, kuhimiza umoja, kusimamia uchumi na kukabiliana na changamoto za maji na tabianchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Samia ameukaribisha mwaka 2026 kwa wito wa mshikamano wa kitaifa, maridhiano ya dhati na kuimarisha ustawi wa wananchi, akisisitiza kuwa taifa linahitaji uponyaji wa pamoja baada ya kipindi kigumu cha kisiasa na kijamii.

Akihutubia taifa kutoka Tunguu, mjini Unguja, Rais Samia alisema, serikali imeanza rasmi maandalizi ya kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa, itakayohusisha wadau wote muhimu nchini.

“Tunapoanza mwaka 2026, serikali tayari imeanza kuchukua hatua za kuanzisha Tume ya Maridhiano. Tutashirikisha wadau kukubaliana muundo wake, majukumu yake na namna ya utekelezaji wake,” alisema.

Alieleza kuwa uamuzi huo umetokana na haja ya kuimarisha umoja wa kitaifa baada ya mwaka uliotikisa mshikamano wa kijamii na kisiasa nchini.

Rais amekiri kuwa kipindi kilichoelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, kilikuwa kigumu kwa Watanzania wengi, kikishuhudia mvutano wa kisiasa na maandamano yaliyosababisha maafa makubwa katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Katika mazingira hayo, aliwataka wananchi kuwa wavumilivu, wenye ukomavu wa kisiasa na uzalendo wa dhati.

“Tusikubali tofauti za kiitikadi au kimtazamo zitugawe na kutupotezea malengo ya taifa,” alieleza.

Rais pia aliwakumbuka Watanzania waliopoteza maisha au wapendwa wao katika matukio mbalimbali ya mwaka uliopita.

“Tumeondokewa na wapendwa wetu, tunaendelea kuwaombea,” alisema kwa huzuni.

Aidha, alisema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia diplomasia ya uchumi, ili kuvutia uwekezaji, kupanua biashara na kukuza ustawi wa wananchi.

“Tanzania inaendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda,” alisema.

Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia aliwahimiza Watanzania kuukaribisha mwaka 2026 kwa mshikamano, nidhamu na dhamira ya pamoja ya kulijenga taifa.

“Umoja wa kitaifa ni ajenda yetu kuu tunapouanza mwaka 2026,” alisema.

Aliongeza kuwa amani na maendeleo ya taifa vitapatikana tu endapo Watanzania watasimama pamoja licha ya tofauti zao.

About The Author

error: Content is protected !!