December 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

2025, mwaka mchungu usiosahaulika

 

NI takriban siku tisa zimesalia kabla ya kuhitimisha safari ya siku 365 za mwaka 2025 ambao umeingia kwenye historia ya kutawaliwa na matukio mabaya yaliyotia doa historia ya Tanzania kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).

Tunaelekea kuuaga mwaka huu huku tukitawaliwa na simanzi, uchungu kwa kupoteza nduzu zetu kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba pamoja na kuendelea kwa matukio ya utekaji, utesaji na vifo.

Baadhi ya familia ambazo ndugu zao wametekwa na mpaka leo haijulikani hatma yao, wanaendelea kulia kilio cha samaki ambacho machozi huishia majini.

Mwaka 2025 utasahaulika vipi kwenye kumbukumbu za Watanzania walioshuhudia maandamano ya Oktoba 29, yaliyosababisha vilema, vifo na uharibifu wa mali binafsi na za umma?

Mpaka leo hii, serikali haijaweka wazi idadi ya vifo kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni sawa na kusheherekea huku baadhi ya watu waliopoteza wapendwa wao wakiomba wapatiwe miili ya ndugu zao waendelee na taratibu za maziko.

Zipo familia ambazo zimezika nguo kama ishara ya kuwapa heshima ndugu zao waliouawa kwenye maandamano hayo ikiwa miili yao haijapatikana.

Humphrey Polepole

Maandamano hayo yaliyohamasishwa mitandaoni na Watanzania wa ndani na nje ya nchi, ni tukio lililotuweka kwenye wakati mgumu wa kuaminiwa na kupata misaada, mikopo na ufadhili.

Mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mara ilishuhudia vurugu hizo wakati vijana (waandamanaji) walipokabiliana na vyombo vya dola. Ni historia itakayoendelea kutuandamana kila tunapokwenda.

Vyombo hivi vya dola tunavyovigharimia kwa odi zetu ndivyo vilivyotumika kukatisha uhai wa wenzetu na kuwajeruhi walioshiriki na wasioshiriki.

Ni askari walewale tunaokula pamoja, kucheka na kulia kwenye matukio mbalimbali ndiyo waliowafyatulia risasi wenzao ili kulinda serikali isipinduliwe. Wamelinda kiapo chao.

Hata hivyo ni jambo la kusikitisha baadhi ya waliouwawa au kujeruhiwa hawakushiriki kwenye maandamano. Kilichowakuta ni kuthibitisha msemo wa ‘vita havina macho’

Mtangazaji wa vipindi vya michezo, katika radio ya Clouds, Tindwa Mtopa (Master Tindwa) aliripotiwa kupigwa risasi nje ya nyumba yao Temeke jijini Dar es Salaam.

Sheikh Hussein Msopa ‘Sharif Majini’ naye kifo chake kimetokana na kupigwa risasi tarehe 29 Oktoba nyumbani kwake Mabibo jijini Dar es Salaam.

Sharif Majini alikuwa mmoja wa wagombea waliojitokeza kuchukua fomu ya kugombea ubunge katika jimbo la Handeni Vijijini mkoani Tanga, katika uchaguzi mkuu 2025.

Hao ni baadhi ya watu mashuhuri waliofariki. Vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti idadi inayotofautiana juu ya vifo vilivyotokea. Kuna vinavyodai ni watu 700, vingine 1000 na vingine 2000. Kila kimoja na takwimu yake.

Mwaka 2025, hauwezi kuisha bila kugusia juu ya kutekwa kwa Humphrey Polepole aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba. Huyu aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Balozi huyu alifikwa na mkasa huu usiku wa kuamkia tarehe 6 Oktoba, nyumbani kwake Ununio jijini Dar es Salaam, mpaka leo hakuna taarifa zake na Jeshi la Polisi linaendelea na kuchunguza tukio hilo.

Familia ya Mwanadiplomasia huyo hasa mama yake Mzazi AnnaMary Polepole amekuwa akiomba
arudishiwe mtoto wake- Humphrey Polepole akiwa hai au amekufa.

Mdude Nyagali kada maarufu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alivamiwa na kutekwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake usiku wa terehe 2 Mei mwaka 2025 .

mwaka huu kumeripotiwa watu mbalimbali kutekwa huku familia zao zikihangaika vituo vya polisi, hospitalini kuwasaka bila mafanikio .

Hivyo ndivyo wanavyoouaga mwaka ndugu wa watu hawa.

Miongoni mwa matukio yaliyotikisa na kutawala kwa muda mfupi ni kuibuka kwa mtu aliyejitambulisha ni askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), mwenye cheo cha kapteni Charles Tesha akitaka yafanyike mabadiliko mbalimbali ili kunusuru taifa.

Maandamano ya tarehe 29 Oktoba maarufu ‘MO29’ yaliibuka kama wazo la wanaharakati na vijana wa Kitanzania, hususan kizazi cha Gen Z, waliopanga kujitokeza siku ya uchaguzi mkuu wa Tanzania,siku ya kuchagua rais, wabunge na madiwani.

Lengo lao lilikuwa kuonyesha kutoridhishwa na mwelekeo wa demokrasia, uhuru wa kisiasa na mwenendo wa uchaguzi.

Kwa siku kadhaa kabla ya tarehe hiyo, mitandao ya kijamii ilitawaliwa na mijadala iliyogubikwa na hofu, matumaini na maswali juu ya usalama wa waandamanaji.

Kwa matukio yaliyotokea mwaka 2025, swali kubwa linalobaki vichwani mwa Watanzania ni kwa namna gani tutatoka katika mazingira magumu tuliyonayo?

Je tunaweza kufanya maridhiano na kuponya majeraha tuliyonayo kwa njia iliyo safi na salama? viongozi wa kisiasa, dini, vyombo vya dola na jamii tunaweza
kujenga demokrasia inayosikiliza kabla mambo hayajaharibika?

La sivyo, matukio kama ya MO29 na kuibuka kwa sauti zisizotarajiwa yataendelea kujirudia kwa nguvu zaidi na kwa gharama kubwa kwa taifa.

About The Author

error: Content is protected !!