December 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Jeshi la Polisi ni mwendo wa ‘kukanusha’

Msemaji wa Polisi, DCP David Misime

 

JESHI la polisi nchini limeingia kwenye rekodi ya kutoa makanusho mengi kwa muda mfupi kupitia mitandao yake ya kijamii kila linapohusishwa na jambo fulani . Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).

Makanusho haya, ambayo sasa yamekuwa ‘yatrend’ kwenye taarifa za taasisi hiyo, yameibua maswali makubwa kwa wananchi, yapi ni ukweli na upi ni uongo? Badala ya kuzima moto wa sintofahamu, baadhi ya makanusho haya yamezidi kuongeza mashaka kwenye jamii na kupanua ufa wa kutoaminiana kati ya vyombo vya dola na jamii.

Mfano wa karibuni ni tukio la tarehe 22 Desemba 2025, ambapo Jeshi la Polisi lilikana taarifa zilizosambaa kuwa katibu wa Chadema kanda ya kati, Ashura Masoud, amekamatwa wakati akijiandaa kuzungumza na waandishi wa habari. Polisi walieleza kuwa hakukamatwa bali aliitwa kituoni kwa ajili ya mahojiano ya kawaida.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilipingwa wazi na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Gaston Galubindi, aliyethibitisha kuwa Ashura, alikamatwa akiwa ofisini kwake Dodoma. Tofauti hizi za simulizi zimeacha wananchi wakijiuliza, mahojiano ya kawaida ni yapi yanayofanyika chini ya mazingira ya kukamatwa?

Changamoto kubwa zaidi imekuwa pale ambapo hata taarifa zenye ushuhuda wa moja kwa moja au ushahidi wa kimazingira zimekuwa zikikanushwa au kupuuzwa, huku maelezo rasmi yakichelewa kutolewa au yakionekana kukosa uzito wa kina.

Hali hii imesababisha kutoa mwanya mpana kwa tetesi, nadharia na simulizi mbadala kusambaa kwa kasi zaidi mitandaoni kuliko taarifa rasmi.

Tukio jingine lililorudisha mjadala huu mezani ni taarifa ya tarehe 21 Desemba 2025, ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro lilikana madai ya uvamizi wa watu wenye silaha nyumbani kwa wazazi wa mwanaharakati wa haki za binadamu, Godlisten Malisa, katika Kijiji cha Old Moshi Kidia.

Polisi walieleza kuwa si kweli kuwa mama mzazi wa Malisa aliwekwa chini ya ulinzi mkali, wakidai kuwa askari walifika nyumbani hapo kwa ajili ya uchunguzi wa taarifa ya uvamizi uliodaiwa kutokea usiku wa manane.

Mfululizo huu wa makanusho uliendelea tena tarehe 23 Desemba 2025, pale Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lilipokanusha taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii, hususan Facebook na Instagram, zilizodai kuwa gari la polisi lilihusika katika ajali iliyosababisha kifo cha mwananchi katika eneo la Kongowe wilayani Kibaha.

Polisi walisisitiza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote, hata hivyo kwa sehemu ya wananchi, kanusho hilo halikupokelewa kama ukweli wa mwisho bali kama sehemu ya mnyororo wa taarifa zinazopingana na simulizi za mashuhuda.

Israh Midemba mkazi wa Kisemvule pwani amesema kuwa imani ya wananchi kwa jeshi hilo imeshuka hivyo hawaamini kauli zao “yaani jeshi letu limekosa bahati kauli zao zina nia njema lakini bahati mbaya kwa wananchi limepoteza imani”.

Baadhi wa watumiaji wa mitandoa ya kijamii wametoa maoni mbalimbali kuhusu mjadala huo :- Tatu_bila amehoji “Lini mtakubali kilasiku kukanusha polisi?

Ni ukweli kwamba yapo madai yanayoelekezwa kwa Jeshi la Polisi ambayo hayana msingi wowote wa ukweli. Lakini kutokana na historia ndefu ya tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, na ukosefu wa uwajibikaji wa wazi katika baadhi ya matukio ya nyuma, wananchi wamekuwa wepesi kuyaamini hata madai dhaifu.

About The Author

error: Content is protected !!