December 19, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Chadema: Tutaishitaki Magereza kuminya Lissu haki zake

Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema akiwa mahakamani

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitalichukulia hatua jeshi la magereza kwa kumnyima haki zake za msingi, mwenyekiti wake, Tundu Antipas Lissu, anayeshikiliwa katika Gereza Kuu la Ukonga, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Miongoni mwa haki zinazodaiwa kukiukwa na jeshi la magereza kwa Lissu, ni pamoja na kumnyima haki ya kukutana na mawakili wake kwa faragha.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Gaston Galubindi, wakati akizungumza na gazeti hili, jana jijini Dar es Salaam.

Galumbidi ni mmoja wa mawakili wa Lissu, anayekabiliwa na mashitaka ya uhaini, Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Galumbindi, alifika kwenye Gerezani Kuu la Ukonga jana tarehe 17 Desemba, kwa ajili ya kukutana na Lissu, lakini hakufanikiwa kuongea naye kwa kuwa maofisa wa magereza waliwataka wazungumze mbele yao, jamba ambalo ni kinyume cha katiba na sheria.

Galubindi amesema, ameshindwa kutekeleza jukumu lake la uwakili, ambalo ni kushauriana mwenendo wa mashauri katika kesi Na. 19605/2025 inayomkabili mwanasiasa huyo machachari wa upinzani nchini.

Amesema, “Gerezani kuna utaratibu mpya umeanzishwa ambao ni kinyume cha sheria. Nilichokutana nacho leo, ni kama ifuatavyo:

“…magereza wamenilazimisha kuzungumza na mteja wangu mbele ya maafisa wao, kinyume na Katiba ya nchi, sheria ya Magereza na kanuni za kimataifa. Hivyo, nimeshindwa kutekeleza majukumu yangu kama wakili,” ameeleza. 

Ameongeza, “kutokana na hiyo, tumekubaliana na Lissu tutafute kwanza haki ya usiri wa mazungumzo kati ya mawakili na mteja wake.”

Galubindi amesema, utendaji kazi wa magereza kinyume cha sheria, kanuni na Katiba, unazidi kushika hatamu, hivyo kurugenzi yake, haikubaliani na mazoea hayo.

“Tutatachukua hatua stahiki za kisheria na za haraka, kukomesha matendo hayo,” amefafanua.

Amesema, “Tutachukua hatua dhidi ya matendo hayo, tayari nishawasiliana na mwanasheria mkuu wa chama chetu na kurugenzi yetu ya sheria inajiandaa kuchukuia hatua hizo.

“Hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika. Magereza wanafahamu misingi ya kazi, kitendo wanachokifanya wanafahamu kuwa ni kinyume cha Ibara ya 13 ya Katiba.

“Ni kinyume cha sheria za nchi kuhusu haki za wafungwa na mahabusu na kinyume na mikataba ya kimataifa. Lakini wameamua kufanya hayo, kwa makusudi. Lazima tuchukue hatua dhidi yako,” amefafanua.

Mbali na hilo wakili huyo amesema, Lissu ameandika barua kwenda kwa Msajili wa Mahakama Kuu, kuulizia siku ambayo shauri lake, litarudi tena mahakamani.

Lakini barua ya Lissu kwenda kwa msajili wa mahakama, imechukua zaidi ya siku 10 kutoka Ukonga kwenda Mahakama Kuu, Mtaa wa Kivukoni, jijini Dar es Salaam.

Anasema, “Lissu aliandika barua kwa naibu msajili wa Mahakama kuu, tarehe 5 Desemba 2025, akitaka kufahamishwa tarehe rasmi ya session ya kesi ya uhaini inayomkabili pamoja na mwenendo wa kesi hadi ilipoishia.

“(Taarifa ya Lissu kuandika barua ilitolewa pia kwa umma) sasa Pamoja na kwamba aliandika barua tarehe 5, cha ajabu ni kwamba barua hizo zinaonekana zilifika Mahakamani tarehe 15 December 2025, yaani juzi jumatatu.”

Amesema, mahakama iliweka muda wa kusikiliza kesi ya Lissu kuwa ni kuanzia 3 Oktoba hadi tarehe 11 Novemba 2025, lakini hakuletwa Mahakamani hadi siku ya tarehe 11 na tangu siku hiyo hakuna tarehe rasmi iliyopangwa.”

Pia Lissu ameomba nyaraka za kesi Na. 28922/2025 ya mali za Chadema iliyofunguliwa na Saidi Issa Mohammed, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Chadema – Zanzibar na wenzake dhidi ya chama hicho.

About The Author

error: Content is protected !!