December 19, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mihemko ya madereva chanzo za ajali za mwisho wa mwaka

Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Joseph Mwakabonga

 

JESHI la Polisi Nchini kupitia kikosi cha Usalama barabarani limefanya ukaguzi maalumu wa mabasi ya abiria kwa ajili ya kudhibiti ajali kutokana na ongezeko kubwa la abiria kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).

Mkuu wa Operesheni Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Joseph Mwakabonga leo wakati akizungumza na madereva katika Stendi kuu ya mabasi Mkoani Arusha, amesema kuelekea mwisho wa mwaka kunajitokeza ajali kwa sababu madereva wengi wanakuwa na mihemko ya kutaka kusafirisha abiria wengi kwa muda mfupi.

ACP Mwakabonga amebainisha kuwa wanaendelea na operesheni hiyo nchi nzima ili kutoa elimu kwa madereva na abiria pamoja na kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto ili kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua kama siyo kuisha kabisa.

Aidha, amewataka madereva kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani kwani Jeshi hilo halitakuwa na muhali kwa yoyote atakayebainika kukiuka sheria.

Sambamba na hilo, amewataka madereva kujiepusha kuendesha vyombo vya moto huku wakiwa wamelewa, mwendokasi pamoja kuyapita magari mengine kwa uzembe katika maeneo hatarishi bila kuchukua tahadhari za kiusalama.

Kadhalika, amesisitiza kuwa madereva watakaobainika kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani.

Naye Issa Mohamed ambaye ni dereva wa basi la abiria pamoja na kushukuru kwa elimu waliyoipata, amesema ataenda kuwa balozi mzuri kwa madereva wenzake kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara ya ajali ambayo yanaweza kutokea.

Naibu Mkugenzi wa Elimu na Operesheni wa Shirika la kutetea haki za Abiria Tanzania (SHIKUHA) Godwin Mpinga amebainisha kuwa changamoto inayowakabili abiria wengi msimu huu ni ongezeko la nauli, hivyo shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwa abiria kuhakikisha wanalipa nauli iliyopo kwa mujibu wa sheria lakini pia kuepuka kukatiwa tiketi kwa njia ya karatasi.

About The Author

error: Content is protected !!