Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar
AIRTEL Africa leo imetangaza rasmi kushirikiana kimkakati na kampuni ya SpaceX kwa ajili ya kuunganisha huduma ya satelite moja kwa moja katika simu Janja (Starlink Direct to Cell) katika nchi 14 barani Afrika Airtel, ambapo Airtel inahudumia zaidi ya wateja milioni 174. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kupitia ushirikiano huu, wateja wa Airtel Afrika wenye simu janja zinazokidhi mahitaji ya kiteknolojia wataweza kupata huduma ya mawasiliano hata wakiwa katika maeneo yasiyofikiwa na miundombinu ya kawaida ya mtandao wa ardhini.
Huduma hii ya satelaiti katika simu janja (Starlink Direct to Cell ) itawawezesha wateja kuunganishwa moja kwa moja kupitia setilaiti za Starlink, mtandao mkubwa zaidi wa mawasiliano ya 4G duniani kwa upana zaidi. Hatua hii inalenga kuwafikia wananchi wanaoishi katika maeneo ya mbali na magumu kufikika, ambako ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ya ardhini umekuwa changamoto.
Utoaji wa huduma utaanza mwaka 2026, ukijumuisha matumizi ya data kwa huduma mahsusi pamoja na ujumbe mfupi wa maandishi (SMS). Ushirikiano huu pia unajumuisha utekelezaji wa mfumo wa kwanza wa intaneti ya kasi wa Starlink wa Direct to Cell, unaotumia setilaiti za kisasa zitakazowezesha simu za mkononi kupata intaneti ya kasi ya juu mara 20 zaidi ya viwango vya sasa. Utekelezaji wa huduma hii utafanyika kwa kuzingatia taratibu na vibali vya mamlaka za udhibiti katika kila nchi husika.
Kwa hatua hii, Airtel Africa inakuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano ya simu barani Afrika kuanzisha huduma satelite moja kwa moja katika simu janja ya Starlink Direct to Cell, inayotegemea zaidi ya setilaiti 650 kuwezesha mawasiliano ya kuaminika kwa wateja waliopo maeneo ya mbali. Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya Airtel Africa ya kupunguza pengo la huduma kidijitali na kuhakikisha mawasiliano yanawafikia wananchi wote bila kujali wanakoishi. Pande zote mbili zitaendelea kushirikiana kubuni na kuzifikia fursa mpya zitakazochochea ujumuishaji wa kidijitali barani Afrika.
Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema: “Airtel Africa inaendelea kujikita katika kutoa huduma bora kwa wateja wake kwa kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano zilizo thabiti na zisizokatika. Teknolojia ya Starlink ya Direct to Cell inaongeza nguvu kwenye miundombinu yetu ya ardhini kwa kufikia hata maeneo ambayo ni vigumu kuyahudumia kwa njia za kawaida. Tunajivunia ushirikiano huu ambao utaweka viwango vipya vya upatikanaji wa huduma katika masoko yetu yote 14.”
Naye Makamu wa Rais wa Mauzo wa Starlink, Stephanie Bednarek, alisema: “Kwa mara ya kwanza, watu wengi barani Afrika wataendelea kuwasiliana hata wakiwa katika maeneo ambayo mitandao ya ardhini haiwezi kufika. Tunajivunia kuona teknolojia ya Starlink Direct to Cell ikileta mabadiliko chanya katika maisha ya watu. Kupitia ushirikiano wetu na Airtel Africa, tutatoa pia teknolojia ya kizazi kipya itakayowezesha intaneti ya kasi ya juu na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu.”
ZINAZOFANANA
Buckreef Gold yaimarisha ushirikiano na jamii, yapitia upya makubaliano yao
Likizo ya ushindi inakukaribisha Meridianbet kupitia Sweet Holiday Chase
Tabasamu jipya kutoka Meridianbet kwa wanakinondoni msimu wa Sikukuu