OMAR Said Shaban, wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, ameibua pingamizi zito la kisheria akipinga mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kushiriki katika kusimamia kesi zinazohusu masuala ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Pingamizi hilo limeibuliwa leo katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, Masjala ya Chake Chake, wakati wa kutajwa kwa shauri linalohusisha Wagombea wa Ubunge kupitia Chama cha ACT Wazalendo dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kikao hicho kilikumbwa na mabishano makali ya kitaratibu baada ya Wakili wa Waleta Maombi, Omar Said Shaaban, kuhoji uhalali wa kisheria wa mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kusimama kwa niaba ya Wajibu Maombi, ambao ni taasisi za Muungano.
Akieleza hoja zake, Wakili Shaaban alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Katiba, taasisi za Muungano ziko chini ya Serikali ya Muungano, hivyo zinapaswa kuwakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano au Wakili Mkuu wa Serikali ya Muungano (Solicitor General), na si maafisa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hata hivyo, katika hatua iliyoelezwa kuwa si ya kawaida, Naibu Msajili aliyekuwa anaendesha kikao hicho, Mheshimiwa Chausiku Kayu, aliingilia kati kabla Wakili wa Waleta Maombi hajamaliza kuwasilisha hoja zake.
Wakili Shaaban alieleza kushangazwa na hatua hiyo, akidai kuwa Naibu Msajili hakutoa fursa kwa upande wa Serikali kujibu pingamizi hilo la kisheria.
Bila kutoa uamuzi juu ya uzito wa hoja hiyo—ambayo inagusa kwa kina mipaka ya mamlaka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar—Naibu Msajili aliamua kulipeleka jalada la shauri hilo kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya kumpangia Jaji atakayesikiliza na kuamua maombi hayo.
Hatua hiyo imeacha wazi mjadala mpana wa kikatiba kuhusu uwakilishi wa taasisi za Muungano katika Mahakama za Zanzibar, suala linalotarajiwa kuwa na athari kubwa za kisheria na kiutawala.
ZINAZOFANANA
Tabasamu jipya kutoka Meridianbet kwa wanakinondoni msimu wa Sikukuu
Tanzania yawekewa vikwazo vipya Marekani
Makamu wa Rais aongoza mazishi ya Jenista Mhagama