March 11, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

GEN Z ni kina nani, mbona mnatutesa hivi?

 

GEN Z, GEN Z, GEN Z, ninawaita mara tatu kama vile Petro alivyomkana Bwana Yesu Kristo kabla ya jogoo halijawika. Kwa nini mnatutesa hivi? Anaandika Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea)

Yaani sisi ni watu wa kukaa ndani siku ya uhuru wa Tanganyika (Desemba 9)? Tumewakosea nini mpaka mkasababisha tuzuiwe kwenda kwenye sherehe iwe uwanja wa Taifa, Jamuhuri au uwanja wowote ule uliopangwa na serikali, kuangalia ndege za kivita zikiranda angani, gwaride la askari waliovalia nadhifu na vifaa lukuki vya kisasa.

Ninyi GEN Z, ni kina nani? Mbona mlikataa haraka kufarakanishwa kwa misingi ya kidini pale wazito walipotaka kuitumia karata hiyo kuficha udhaifu wao baada ya matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 siku ambayo taifa lilifanya uchaguzi mkuu ambao uliingia doa la vurugu.

Mliamua kuutumia kikamilifu mtandao wa kijamii kukataa udini na kuchijana kama walivyosema wale jamaa. Mlilionyesha taifa kuwa sisi ni wamoja na tusioweza kugawanyika kwa sababu ya kidini.

Mliamua kujiita WAKRISLAM. Miliposalimiwa, Asalaam Alayekum. Mkajibu Waaleykum Shaloom.

Kweli ninyi ni GEN Z, niliwaona baadhi yenu (wakristo) mkicheza Qaswida za kiislamu na waislamu wakicheza nyimbo za injili za kusifu na kuabudu. Yaani mliwavua nguo na kuwakimbiza waliozoea kutumia udini kuficha udhaifu wao.

Kwa nini akili zenu zinafanya kazi haraka sana tofauti na sisi ‘wazee’ ambao kila tunachoambiwa na mkuu wa kaya na wasaidizi wake tunakiamini?

Hivi GEN Z ni kina nani? Mjomba wangu Paulo ameniambia eti ninyi ni kizazi kinachoundwa na watu waliozaliwa kati ya miaka ya 1990 na katikati ya miaka ya 2000.

Ameniambia mnatumia sana mtandao (intaneti) tangu mkiwa na umri mdogo na kama si maisha yenu yote, ameniambia mnafurahia teknolojia na mitandao ya kijamii. Ila kaniambia mnachojifunza huko hata yeye hakijui.

Ubora wao uko katika ulimwengu wa teknolojia, mitandao ya kijamii na simu janja. Ni kizazi cha kuitaka sauti kisiasa, kijamii na kiutamaduni,

Wanapenda kasi, ubunifu, uhuru wa kujieleza na kusimamia haki. Mjomba kaniambia kizazi hiki hakina hofu ya kuuliza maswali, kukosoa au kupaza sauti.

Kwa hakika, kizazi chenu kimezaliwa ndani ya enzi ya kiteknolojia na kina ufahamu mkubwa wa teknolojia na utandawazi. Si rahisi kupiga makofi na kushangilia ‘Zidumu fikra za Mwenyekiti’

Kimsingi kaniambia kama nataka niwe salama ni lazima niwaelewe, kuwasikiliza na kuwatimizia mahitaji yetu kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni tulizojiwekea.

Kweli ninyi GEN Z ndiyo wa kufanya mitaani kwetu na majiji yetu yalindwe kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)? Sasa utofauti wa majukumu yao uko wapi?

Ushirikiano huu ni kwa ajili ya kuwadhibiti msifanye maandamano yasiyo na kibali kwa kuwa nini ni wagumu kuelewa.
Mmetusababisha tutumie fedha nyingi kwenye ulinzi na sina shaka kuna huduma zitalega kwa kuwa fedha zake zimepelekwa kuimarisha ulinzi.

Ninyi GEN Z hivi hamjui tulipokaa nyumbani tarehe 9 Desemba si kwa sababu ya mapumziko bali kwa sababu yenu tumepoteza mabilioni ya fedha? Je mna mpango gani siku zijazo?

Ninyi ndiyo umewafanya wale wafuasi na wapiga debe wa chama tawala waliokuwa wakijiona wako salama na kutoa kauli za ubabe na jeuri sana wana adabu na nidhamu na wanajua hawako salama.

Mlitulazimisha hata sisi tukiokuwa wavivu wa kunua bidhaa nyingi na kuweka ndani tukabadili tabia na tukanunua vitu kwa wingi tukihofia yale ya tarehe 29 Oktoba hadi 3 Novemba kujirudia.

Mmetusaidia kudumisha uhusiano kwenye familia zetu na kuona thamani ya kila mmoja wetu. Kwa hili nitaendelea kusifu nguvu zetu.

Mmewafanya mawaziri kila wanapozungumza watueleze mipango mingi inayowaguza yenye kukuza ajira na ujuzi na fursa nyingine za kuboresha uchumi wenu.

Najiuliza mtachukua hatua gani kama mipango ya mawaziri hawa tunaona na kuwasikia isipotekelezwa?

Tutalazimika kujifungia tena tusisheherekee Sikukuu ya Krismas, Mwaka mpya au Idd? Hebu tukumbukeni wenzenu umri umeyoyota hatuna mbio za kukimbizana nanyi.

Gen Z wa Tanzania ni kizazi chenye akili, kasi, ubunifu wa kijidijati na ujasiri wa kupaza sauti.

Nani ambaye atawabishia kuwa hamjabadili mitandao, biashara, siasa, burudani, lugha na fikra za taifa kwa ujumla? Gen Z tuacheni tupumzike sisi wazee maana kuna dalili za kutofika kwenye nchi ya ahadi (Kaanani) tuliyoahidiwa.

About The Author

error: Content is protected !!