Wananchi wakinunua mahitaji mnadani
USEMI ‘uking’atwa na nyoka hata unyasi ukitikisika utashtuka’ unaendelea kudhihirika kwa baadhi ya wananchi nchini wanaofikiria tishio la maandamano yaliyotangazwa kufanyika tarehe 9 Desemba, 2025 huku wakiwa na kumbukumbu ya vurugu zilizotokea 29 Oktoba 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Siku hiyo walishuhudia risasi zilizotoka kwa askari zikipoteza uhai wa wananchi wenzao, zikiwajeruhi wengine walioshiriki na wasioshiriki kwenye maandamano yanayoitwa ni ‘vurugu’ zilizofanywa na vijana walioshawishiwa na wageni wenye kutamani rasilimali za taifa.
Sasa wanafikiria maandamano ya 9 Desemba yaliyopewa jina fupi la ‘D9.’ Swali kubwa linaloendelea kutawala vichwani mwa wananchi huku moyo wa kila mmoja ukibeba hofu ya nini kitatokea siku hiyo iwapo wazuia maandamano watakapokabiliana na waandamanaji.Anaripoti Fedrick Gama …(endelea)
Wananchi wanajiuliza hali itakuaje wakizuiwa kutoka majumbani mwao wakati kundi kubwa ni lile lenye kutegemea kutoka ili wapata riziki ya siku husika?
Wengi wao hawana akiba ya fedha wala chakula, wanahofia milio ya mabomu ya machozi na risasi. Wanahofia kile kilichotokea Oktoba 29 kinaweza kujirudia.

“Nina hofu kubwa sana kama maandamano haya yatafanyika familia yangu itapitia wakati mgumu sana kwasababu maisha yangu ni magumu, sina kazi wala biashara ya uhakika. Kama maandamano haya yatatokea yataiweka familia yangu katika mazingira magumu sana, Ili familia yangu ipate chakula inanilazimu nitoke nikatafute chochote kile huko barabarani, sasa kama yakifanyika maandamano sijui tutaishije?” Anasema Nasma Athuman mkazi wa Sinza kwa Remmy jijini Dar es Salaam.
Mkazi wa Buguruni Rozana, ambaye hakupenda jina lake liandikwe, anasema iwapo maandamano yatafanyika yatamuathiri kwa kiwango kikubwa kwa sababu hajajiandaa kwa chochote na hana fedha za kununua chakula.
Anasema anatamani kwenda nyumbani kwao Zanzibar lakini anashindwa kwa kuwa hana nauli “biashara pekee ninayotegemea ni kuuza vitumbua lakini biashara yangu katika mazingira ya kama yale ya tarehe 29 Oktoba hudorora hakuna mtu wa kumuuzia, kusema kweli nipo katika wakati mgumu”.
Omari Mkali mkazi wa eneo la Kibamba Shule, amesema kuwa watu wanakimbilia sokoni (mnadani) kukusanya vitu vya kuweka ndani wakihofia maandamano.

“Jana nimepita pale mnadani kama ilivyo kawaida yangu siku ya Jumatano kunakuwa na ‘gulio’ lakini niliona baadhi ya wafanyabiashara wameshamaliza bidhaa walizokuwa nazo. Huwa napita pale saa mbili usiku lakini jana nilipita saa 12 jioni nikaona mambo tofauti nilipowauliza wauzaji wakaniamba wateja wanachukua tahadhari ya kuwa na vitu mapema,” Amesema
Naye Ayoub Mussa, mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, amesema hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa tarehe 2 Desemba, 2025 ina pande mbili, moja ni kuwakatisha tamaa wanandamaji lakini upande wa pili ukawachochea wajitokeze.
Amesema baada ya kauli hiyo mitandaoni kuliibuka mijadala kuwa kauli ya Rais Samia haikulenga kuwaponya waliojeruhiwa na waliopoteza ndugu zao kwenye maandamano ya tarehe 29 na hawajapata miili ya ndugu zao hivyo wanaweza kujitokeza ili kupunguza hasira zao.
Katika hotuba yake aliyoitoa juzi, tarehe 2, Desemba 2025 Rais Samia Suluhu Hassan, alizungumza na wazee wa jiji la Dar es Salaam ambapo alionya wale wote wanaotaka kuandamana ‘D9’ wajue serikali imejipanga na itatumia nguvu kulingana na tukio litakavyokuwa.
Kwa maelezo yake Rais Samia aliwakosoa wale wanaolaumu askari kuwapiga risasi watu walioandamana ambapo alisisitiza kuwa ‘nguvu iliyotumika ilistahili’.

Rais Samia alisema nguvu hiyo ilitumika kwa kulikuwa na jaribio la kuipindua serikali kuondoa dola iliyopo madarakani katika maandamano yaliyofanyika siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, na kusababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Katika hotuba yake, Rais Samia amesema tukio hilo ni la “kutengeneza na waliotengeneza walidhamiria makubwa.”
Kauli ya Rais Samia inakuja takriban mwezi mmoja upite tangu vurugu hizo zitokee na kutia doa historia nzuri ya Tanzania kuwa ni kisiwa cha amani, utulivu na mfano wa kuigwa katika demokrasia.
Rais Samia ameshaunda tume ya kuchunguza kiini cha tukio hilo na mzizi wa vijana kuingia barabarani kwa ajili ya maandamano.
Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba tarehe 25 Novemba 2025, alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini amesema kuwa maandamano ya Oktoba 29 yamesababisha uharibifu wa mali ikiwemo kuchoma ofisi za serikali 756; vituo vya mabasi ya mwendokasi 27; mabasi sita; nyumba za watu binafsi 273; vituo vya polisi 159; vituo vya mafuta 672; magari ya watu binafsi 1,642; pikipiki 2,268; magari ya serikali 976 zikiwemo ambulance.
ZINAZOFANANA
Umoja wa Mataifa, Marekani yaikaba koo Tanzania
Wanafunzi 937,581 wachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza, wasichana vinara
Ujumbe umefika, watawala wamepotezea