JESHI la polisi nchini Tanzania limesema, limejipanga kukabiliana na wimbi la uhalifu wa kimtandao na mipango ya vurugu inayosema, “inahamasishwa kupitia mitandao ya kijamii, kuelekea tarehe 9 Desemba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi hilo, makao makuu ya polisi, mjini Dodoma, David Misime, leo tarehe 3 Desemba 2025, limesema limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda maisha ya raia mali zao.
“Tunawahakikishia amani na utulivu vinaendelea kuimarika nchini,” imeeleza taarifa hiyo ya Misime.
Amesema, jeshi la polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kwa nafasi zao kuanzia ngazi za familia, kukataa watu wanaohamasisha vurugu.
Alidai kuwa wanaohamasisha maandamano wana malengo ya kuharibu taifa na kuwarudisha kwenye machungu na madhara yaliyotokea tarehe 29 Oktoba na siku zilizofuata.
Misime anasema, wanaohamasishana mtandaoni wamekuwa wakitoa maelekezo hatarishi, ikiwamo mafunzo maalum ya silaha.
“Wamekuwa wakitaka shughuli zote nchini zisimame, kuharibu na kuchoma minara ya mawasiliano ili taifa likose huduma, kufunga barabara zote kuingia na kutoka bandarini Dar es Salaam, kufunga mipaka yote ya nchi, kupora mali za watu kwa kisingizio cha njaa,” ameeleza Misime.
Kauli ya polisi imekuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutetea hatua zilizochukuliwa na vyombo vya usalama wakati wa machafuko ya 29 Oktoba 2025, siku ambayo polisi walikabiliana na waandamanaji na kusababisha vifo na majeruhi katika maeneo kadhaa nchini.
Akizungumza leo katika mkutano na wazee wa Dar es Salaam, Rais Samia alisema nguvu iliyotumika na vyombo vya dola ilikuwa ya lazima kulinda amani na kuzuia kile alichokitaja kama jaribio la mapinduzi.

Rais Samia alitupia lawama mataifa ya nje kushiriki kushawishi na kuchochea vurugu hizo.
Haya yanajiri wakati ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR), inasema imepokea ripoti zinazoonyesha kuwa mamia ya watu waliuawa, huku wengine wengi wakijeruhiwa au kuzuiliwa wakati wa kipindi cha uchaguzi.
“Baada ya intaneti kuzimwa kwa takriban wiki moja, makumi ya video na picha zilianza kuibuka mtandaoni zikionyesha atahari yamatukio ya vurugu: maafisa waliovalia sare wakionekana kufyatulia risasi umati wa watu, miili ikiwa imetapakaa mitaani, huku mingine ikiwa imerundikana nje ya hospitali,” imeeleza taarifa ya UN.
ZINAZOFANANA
Makamu wa Rais afungua maadhimisho ya Kimataifa ya usugu wa vimelea vya magonjwa
Niffer, Chavala waachiwa huru baada ya siku 40
Rais Samia: Tulitumia nguvu inayostahili, walitaka kufanya mapinduzi