Rais Samia Suluhu Hassan
RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema walitumia nguvu inayostahili kudhibiti vurugu za tarehe 29 Oktoba 2025, akisisitiza kuwa yote yaliyotokea ilikuwa na lengo la kulinda amani ya nchi. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza leo tarehe 2 Desemba 2025, mbele ya Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rais Samia amesema Serikali ina jukumu la kikatiba kuhakikisha usalama wa raia, mali zao na utulivu wa Taifa na kwamba haiwezi kusita kuchukua hatua pale kunapojitokeza viashiria vya uvurugaji wa amani.
“Serikali ina wajibu. Tunaapa kuilinda nchi hii, usalama wa raia na mali zake. Na katika hali hiyo, nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo. Sasa tunapoambiwa kwamba tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile… nguvu ndogo ilikuwa ni ipi? Tuwaangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe?” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa kila hatua iliyochukuliwa ilikuwa ni sehemu ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi salama, huku akibainisha kuwa serikali haitasita kutumia uwezo wake wote, kukabiliana na watu wanaojaribu kupandikiza machafuko au kuvunja utulivu.
“Serikali itafanya kila linalowezekana, kadiri ya nguvu inayotumika kuharibu amani, ili kuweza kupambana na wanaopanga kuivuruga,” amesisitiza.

Kauli ya Rais Samia imekuja katika kipindi ambacho mjadala kuhusu matumizi ya nguvu za dola wakati wa tukio la tarehe 29 Oktoba 2025, unaendelea kushika kasi katika mitandao ya kijamii na mijadala ya kitaifa, huku serikali ikisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa ustawi wa Taifa
Kwa kauli hii moja, Rais Samia Suluhu Hassan aligeuza mjadala wa kitaifa juu ya matumizi ya nguvu kuwa tathmini ya msingi kuhusu mustakabali wa amani na utawala wa sheria nchini.
Kauli ya Rais Samia aliyoitoa mbele ya Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam tarehe 2 Desemba 2025 imeingia moja kwa moja katika mijadala ya kisiasa nchini. Sio kwa sababu tu imetolewa na mkuu wa nchi, bali kwa sababu imegusa kiini cha uhusiano kati ya dola, wananchi na mipaka ya matumizi ya nguvu katika kulinda amani.
Katika hotuba yake, Rais Samia alijibu hoja zilizokuwa zikizungumzwa katika mitandao ya kijamii na majukwaa ya umma kuwa Serikali ilitumia nguvu kubwa katika kudhibiti vurugu zilizotokea tarehe 29 Oktoba, kwa mtazamo wake, hatua zilizochukuliwa hazikuwa za kupita kiasi, bali zilikuwa ni sehemu ya wajibu wa kikatiba wa dola kulinda amani na kuzuia ghasia kabla hazijageuka kuwa tishio la kitaifa.
Kauli hii imeibua tafakuri pana, Je, ni kiasi gani cha nguvu kinafaa kutumika kukabiliana na vurugu? Je, dola inapaswa kusubiri mpaka uasi uwe kamili ndipo ichukue hatua? Na je, hatua hizo zinapaswa kuzingatia nini kwanza usalama wa Taifa au hofu ya kukosolewa?

Katika nadharia za utawala, dola inapewa uhalali wa kutumia nguvu pale tu inapolazimika na wakati huohuo inatakiwa kutekeleza majukumu yake bila kuvunja haki za msingi. Hata hivyo, mazingira ya vurugu yana tabia ya kuwa na ukweli mmoja mgumu hatua za polepole ndizo zinazoruhusu machafuko kukua.
Ndiyo maana Rais Samia alisisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua sawia na ukubwa wa tishio.
Kiuhalisia, kauli ya Rais Samia imefungua sura mbili za mjadala wa kisiasa, wanaoamini katika uthabiti wa dola.
Hawa wanaona kuwa hatua za Serikali zinatatua udhaifu, zinazuia ghasia na kuimarisha mamlaka ya dola katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na mawimbi ya maandamano yasiyo na mipaka.
Pia wanaohoji ukubwa wa nguvu iliyotumika, hawa wanatazama suala hili kama fursa ya kusisitiza umuhimu wa uwiano kati ya nguvu za dola na haki za kiraia, hasa katika enzi ambayo ushiriki wa wananchi katika siasa umekuwa mkubwa kupitia majukwaa ya kidijitali.
Kauli ya Rais Samia haikua tu majibu ya haraka bali imekuwa nukta ya mwanzo ya mjadala mpya, uhalali na mipaka ya matumizi ya nguvu katika kulinda utulivu wa nchi.
Katika Taifa linalosimama kati ya misingi ya demokrasia na ulinzi wa amani, hoja hizi zitabaki hai na zitahitaji majibu ya kina, si ya papo kwa papo.
Kwa sasa, ujumbe wa Rais Samia uko wazi: amani ya Tanzania ni mstari mwekundu, na serikali iko tayari kuchukua hatua zozote zilizopo ndani ya uwezo wake kuilinda.
ZINAZOFANANA
Samia: Oktoba 29 walitaka kupindua dola ninayoiongoza
TANESCO yakanusha kuhusika na shambulio la Dk. Kitima
Kifahamu kilichomo mkutano wa Samia na Wazee wa Dar