Rais Samia Suluhu Hassan
RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzungumza na wanaoitwa, “Wazee wa mkoa wa Dar es Salaam,” leo Jumanne, kuanzia saa tano asubuhi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa kutoka Ikulu jijini Dar es Salaam na Zanzibar zinasema, Rais Samia anatarajiwa kutumia mkutano huo, kuelezea mkakati wa serikali wa kurejesha taifa pamoja.
“Rais Samia anatarajia kutumia mkutano huu, kuzungumzia umuhimu wa kurejesha taifa pamoja. Kuomba wananchi waunge mkono serikali yao na kurejesha umoja wa kitaifa,” ameeleza afisa mmoja wa serikali kwa sharti la kutotajwa lake.
Amesema, “Mkutano unalenga kushusha joto la kisiasa nchini.”
Hata hivyo, mkutano wa Rais unafanyka siku moja baada ya Kanisa Katoliki nchini, kutonesha vidonda vilivyotokana na maandamano ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima amesema, Rais anawajibu wa kuhakikisha watu wote waliohusika na mauaji ya waandamanaji, wanawajibika au kuwajibishwa na wakiri makosa.
Amesema, hali hiyo ndio njia pekee ya kupunguza maumivu na hasira za Watanzania.
Katika maandamano hayo, yaliyodumu kwa siku tatu kuanzia 29 Oktoba 2025, watu kadhaa wameripotiwa kupoteza maisha, wakati wakishinikiza kuwapo mabadiliko mbalimbali kwenye mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki.
Idadi ya vifo inatofautiana, huku hatua ya serikali kuzima mtandao wa intaneti kote nchini ikifanya kuwa vigumu kuthibitisha idadi halisi ya vifo au majeruhi.
Mpaka sasa, Serikali ilitoa taarifa ya awali ya tathmini ya madhara yaliyotokea kutokana na maandamano hayo makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini tangu taifa hili lipate uhuru miongo zaidi ya sita iliyopita.
Maandamano hayo yaliyoanzia jijini Dar es Salaam na kusambaa katika maeneo mengine ikiwemo Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma, pamoja na mikoa mingine, yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya umma na binafsi, ikiwemo vituo vya Polisi, ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), vituo vya mafuta na maduka.
Aidha, mtoa taarifa huyo amesema, rais Samia pia atatumia mkutano huo, kukemea kwa uzito mkubwa, kwa mara ya kwanza, vitendo vya utekaji nchini.
Kwa takribani miaka sita sasa, taifa limekumbwa na vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji; watu kadhaa wamechukuliwa na hawajulikani waliko mpaka sasa.
ZINAZOFANANA
Samia: Oktoba 29 walitaka kupindua dola ninayoiongoza
TANESCO yakanusha kuhusika na shambulio la Dk. Kitima
Katibu wa Nyerere akosoa mkutano wa Samia na Wazee wa Dar es Salaam