November 27, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Bunge la Ulaya lapitisha maazimio tisa dhidi ya Tanzania

Bunge la EU

 

BUNGE la Jumuiya ya Ulaya (EU), limepitisha kwa wingi wa kura, maazimio tisa (9) yanayoilenga Tanzania, kufuatia mauaji ya raia, ukiukwaji wa haki za binadamu na madai ya uchaguzi usio huru na haki wa 29 Oktoba mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Maazimio hayo yamepitishwa katika mkutano wa Bunge hilo, uliofanyika leo Alhamisi, tarehe 27 Novemba 2025.

Bunge hilo limesema, limepata ushahidi wa kutosha wa kuwapo matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyofanywa na vyombo vya usalama tangu siku ya uchaguzi, hali iliyosababisha vifo vya maelfu ya watu, majeruhi, raia kukamatwa kiholela na taarifa za kuwepo kwa makaburi ya halaiki.

Bunge la Ulaya limeilaani serikali kwa kile ilichokiita, “…kukanusha ukweli huu licha ya ushahidi kuongezeka.”

Bunge la Ulaya linaitaka Serikali ya Tanzania kusitisha mara moja ukamataji holela wa wanachama wa upinzani, kukamata waandishi wa habari, waandamanaji na watetezi wa haki za binadamu na Kuzuia Intaneti na kudhibiti vyombo vya habari.

Aidha, Bunge la Ulaya limelaani  kukamatwa kwa Tundu Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Lissu anashikiliwa katika gereza kuu la Ukonga, likimtuhumu kwa uhaini. Bunge la Ulaya limeitaka serikali kumuachia huru mara moja bila masharti, kumruhusu kupata matibabu, kuonana na familia yake na mawakili. 

Katika hatua nyingine, Bunge limeiagiza tume ya Ulaya kusitisha msaada wa moja kwa moja kwa mamlaka za Tanzania.

Rais wa Bunge la Ulaya ameagizwa kupeleka azimio hilo kwa Serikali ya Tanzania, Bunge la Muungano, Baraza la Ulaya, Tume ya Ulaya, Umoja wa Afrika, SADC, ACP na Umoja wa Mataifa (UN).

Bunge la Ulaya limesema, uchaguzi wa Oktoba 2025 haukuwa huru, haki, wala wa kuaminika.

Maandamano hayo ya siku tatu ya kuanzia siku ya uchaguzi wa Jumatano, mamia ya watu wanahofiwa kufariki dunia, huku hatua ya serikali kuzima mtandao wa intaneti kote nchini, ikifanya kuwa vigumu kuthibitisha idadi halisi ya vifo au majeruhi.

Msemaji wa Chadema ameliliambia shirika la habari la AFP, kwamba “takriban watu 700” wameuawa katika mapambano na vikosi vya usalama, chanzo cha kidiplomasia nchini.

About The Author

error: Content is protected !!