MWIGULU Madilu Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, amekutana na wahariri wa vyombo vya habari jana Jumanne, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Katika mkutano huo, pamoja na mengine, Mwigulu alieleza madhira yaliyotokea kwenye maandamano ya 29 Oktoba, yaliyopinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa siku hiyo.
Mbali na kupinga kufanyika uchaguzi, waandamanaji walilalamikia kushamiri kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo utekaji na utesaji; kubambikia watu kesi na ukatili dhidi ya wanadamu. Yafuatayo ni sehemu ya maswali aliyoulizwa.
Deodatus Balile: Hapa nchini, mtu akimuona Polisi anaanza kujikagua nina bangi?
Wakati mwingine hauna bangi, lakini mpaka unafika kituo cha Polisi, tayari una misokoto mitano ya bangi kwenye mfuko.
Tunabadilishaje sura hii, ili kuhakikisha jeshi la Polisi linakuwa na uadilifu na kama wako watu wanaoteka wakashughulikiwe?
Waziri Mkuu – Mwigulu:
- Hili jambo halipaswi kutufikisha kwenye kuuana. Sote tunakubalina kwamba wahalifu wanatakiwa wakamatwe, tumejiwekea sheria, kama tunaona utaratibu tunaotumia umetufikisha kutoaminiana, kuleta taharuki, ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameunda tume.
- Sote tunakubaliana kwamba wahalifu wanatakiwa wakamatwe. Tatizo ni pale taratibu zetu zinapovurugika na kuleta kutoaminiana. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan), ameunda tume kuangalia maeneo yenye mapungufu hasa ya uhusiano, utawala na namna ya kukamata.
Kwamba, makosa ya mtu mmoja yasionekane kama ni sura ya taasisi nzima.

Jesse Kwayu – MwanaHALISI:
Umetueleza madhara ya yaliyotokea 29 Oktoba, vituo vilivyoharibiwa, nyumba, magari mpaka pikipiki, kwanini kigugumizi kutuambia waliokufa? Mnaficha nini?
Kwa sababu waliokota maiti ni polisi, utaratibu wa kupeleka maiti mochwari unajulikana, hii takwimu inafichwa ili nini?
Kwayu alikuwa ameongezea pia swali la Balile aliyetaka kufahamu ni watu wangapi wamefariki? Alisema, Aljazeera wanatuambia 700, taasisi zingine zinasema watu 10,000.
Waziri Mkuu – Mwigulu:
Tukubali kwamba vurugu hizi zimepoteza maisha ya watu. Lakini mnataka tuhesabu kama magari? Maisha ya watu mnataka tuhesabu kama magari? Hivi mnajua damu ya binadamu ilivyo?
Watu wanaongea elfu ngapi, sijui ngapi. Tusidharau uhai. Haya mambo yana madhara hata kiuchumi.
Caren-Tausi Mbowe:
Kuna madai ya kuwapo kaburi la halaiki na familia kutopatiwa miili ya ndugu zao waliofariki.
Mpaka sasa hivi mtaani watu wanalalamika sana kutopata maiti za ndugu zao, kwanini hali inakuwa hivyo? Sisi waandishi wa habari tumeathirika pia, mmoja wa waandishi wetu hajapatikana na wamezika nguo, sawa tumepata matatizo, madhira yametukuta, kwanini watu hawapewi maiti zao?
Waziri Mkuu – Mwigulu.
Hakujibu tuhuma za kaburi la halaiki. Alisisitiza msimamo wa serikali wa kushughulikia matukio kwa utaratibu, na kwamba Tanzania haijawahi kuwa na historia ya kufanya mambo ya aina hiyo.
Akasema, serikali inasubiri taarifa kamili kutoka kwa mamlaka zinazochunguza matukio ya 29 Oktoba.

Neville Meena:
Tunavyozungumza sasa hivi Waziri Mkuu, vyombo vya habari Tanzania hatuna pa kusimama, tunaonekana ni watu wa hovyo ambao hatukufanya kazi yoyote wakati wa uchaguzi, na hii ilitokana na serikali kutuminya kututisha kutokana na kile ambacho tulitaka kufanya, na hasa TCRA (Mamkala ya Mawasiliano Tanzania), kutuandikia barua na kutukataza hiki na kile.
Nini kauli yako kuhusiana na taasisi za serikali kutuingilia katika uhuru wetu wa kihariri na kutukataza kufanya kazi yetu ya kitaaluma inavyostahili?
Waziri Mkuu – Mwigulu:
Kama kuna tukio, nafikiri tushughulikie na tukio husika, Tanzania iko kwenye kumbukumbu ya kutofanya mambo ya aina hiyo, na mwaka huu tu taasisi zote za uandishi tulikuwa tunafanya tuzo, unaweza kupata tuzo kwenye nchi ambayo sio wewe unaandika, kwamba unaingiliwa kwenye uhariri?
Matukio yanaweza kujitokeza na mimi hilo sitaki tubishane nalo, ikitokea tuzishugulikie.
Salim Kikeke:
Kuna ushahidi gani kwamba kilichotokea tarehe 29 Oktoba, kilikuwa economic sabotage? Na je, waliokamatwa ni raia wa nje?
Kuna taarifa zinazungumzia vyombo vya usalama kufyatua risasi za moto hovyo hovyo, nataka kuuliza kulikuwa na order ya ‘shoot to kill’ (agizo la kufyatua risasi na kuua0 na kama ilikuwepo ilikuwa imetolewa na nani?
Waziri Mkuu – Mwigulu:
Tanzania si mali ya chama chochote, na rasilimali zake si mali ya mtu binafsi. Fedha zinazoathiriwa ni za wananchi. Mtu akilenga kuharibu hayo, hiyo ni economic sabotage – kuhujumu na kuharibu uchumi.
Katika mkutano huo alitaja takwimu za mali zilizoharibiwa kwa kuchomwa moto wakati wa vurugu za maandamano hayo ya Oktoba 29, 2025. Ofisi za serikali 756, vituo vya mabasi ya mwendo kasi 27, mabasi 6, nyumba binafsi 273, vituo vya Polisi 159, vituo binafsi vya mafuta 672.
Pia magari ya watu binafsi 1,642 yalichomwa, pikipiki 2,268 na magari ya serikali 976 zikiwa ni takwimu za awali.
Kuhusu vyombo vya usalama kufyatulia risasi raia, Waziri Mkuu alisema yafuatayo:
Pakitokea vurugu, unarudi lini kuuliza kwamba nishoot ama nisishoot? Na tunaona idadi kubwa ya askari wamepoteza Maisha yao, nani kaweka order (kaagiza) wapigwe risasi? Hili ni jambo baya limeshatokeatusubiri tupewe ukweli wake, ukitaka tupewe aliyetoa, aliye-shoot askari (agizo hilo) order hiyo alipokea wapi?
Kwa maneno mafupi ni kwamba, maswali yalikuwa mengi na majibu yalikuwa marefu. Yapo yaliyojibiwa kikamilifu na yapo yaliyopotezewa.
Miongoni mwa ambayo Waziri Mkuu Mwigulu ameyapotezea, ni pamoja na idadi ya waliofariki dunia; miili kutopatikana, tuhuma za kaburi la halaiki, utekaji, utesaji na mauaji.
ZINAZOFANANA
Rais wa zamani wa Brazil, anaanza maisha mapaya gerezani
Vyombo vya habari vimesifiwa au vimedhihakiwa?
Heri ya siku ya kuzaliwa kwa Polepole, ni siku 51 tangu ametekwa