November 25, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Polisi yathibitisha kutoa kwa mauaji ya mtoto wa miaka miwili Mara

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara limethibitisha kutokea kwa mauaji ya Mariam Paye Lubunda, mtoto mwenye umri wa miaka 2 na miezi 9 mkazi wa mtaa wa Zanzibar, Manispaa ya Mji wa Musoma, mkoa wa Mara. Anaripoti Joyce Ndeki, Mara …(endelea).

Taarifa iliyotolewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, leo tarehe 25 Novemba 2025, kuthibitisha tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea tarehe 22 Novemba 2025, majira ya saa 10.00 jioni katika mtaa wa Zanzibar, kata ya Makoko, Manispaa ya Musoma ambapo mtoto Mariam Lubunda aliyekuwa akiishi na wazazi wake, aliuawa kwa kutumbukizwa ndani ya shimo la maji taka.

Shimo hili lilikuwa lipo jirani na nyumbani kwao na mtu aliyetekeleza unyama huo ametambulika kwa jina la William Kanegea mwenye umri wa miaka miaka 20, mjita mkulima na mkazi wa Mtaa wa Buhare.

Inaelezwa kuwa, William Kanegea, anaedaiwa kuwa na changamoto ya afya ya akili alimchukua mtoto Mariam ambaye alimkuta peke yake nyumbani kwao kisha akafunua mfuniko wa shimo la maji taka na kumtumbikiza mtoto huyo akiwa hai na kupelekea kifo chake.

Aidha, mtuhumiwa baada ya kutekeleza tukio hilo alikimbia kusikojulikana lakini wananchi wema walimfuatilia na kufanikiwa kumkamata na kujichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi.

Jeshi la Polisi lilifika eneo hilo na kumkuta mtuhumiwa akiwa na hali mbaya ambapo alichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Manispaa ya Musoma na akiwa anaendelea na matibabu, na baadaye alifariki dunia.

About The Author

error: Content is protected !!