RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, ameiagiza wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, kuzuia wananchi kuuza viwanja kiholela bila kuzingatia matumizi bora ya ardhi. Anaripoti Zakia Nanga, Zanzibar … (endelea).
Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi, wakati akizindua mradi wa nyumba za kisasa za Kisakasaka B na Kisakasaka D; hafla iliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip, iliyopo Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
“Kwa muda mrefu kumekuwa na tabia ya kuuza viwanja bila kuzingatia upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii kama maji na umeme pamoja na kutotenga maeneo ya ujenzi wa barabara,” alieleza.
Amesema, hakuna taifa linaloweza kufanikiwa bila kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi na makaazi, na kusisitiza umuhimu wa mbinu mpya za upangaji wa ardhi mijini na vijijini.
Amesema, Serikali ya Zanzibar, itaendelea kuwekeza katika miradi ya nyumba za makaazi ili kuhakikisha wananchi wanapata makaazi bora kwa gharama nafuu.

Ameeleza kuwa wakati umefika wa kubadili mtazamo na kuachana na kuishi katika nyumba chakavu, akitaja nyumba za Michenzani na Kikwajuni kuwa mifano ya makaazi yaliyopitwa na wakati na kupoteza haiba ya mji.
Amebainisha kuwa maeneo ya Jang’ombe, Kwahani na Kilimani yamewekwa katika mpango maalum wa maboresho.
Kwa mujibu wake, mageuzi makubwa katika sekta ya makaazi ni muhimu ili kujenga miji yenye haiba, thamani na makaazi ya kisasa.
Akizungumzia mradi wa Kisakasaka, Rais Mwinyi alisema, eneo hilo linaenda kuwa mji wa kisasa wenye huduma zote muhimu.
Amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya kununua nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba.
Amewashauri watumishi wa umma kukopa nyumba badala ya kukopa vifaa vya ujenzi vinavyoathiri uwezo wao wa kumaliza miradi ya ujenzi.
Amesema, Serikali itaongeza mishahara na kuweka utaratibu wa makato madogo madogo kwa kipindi cha miaka 25 ili kuwawezesha kumudu gharama za nyumba hizo.

Dk. Mwinyi amekemea tabia ya kuwapa miradi wakandarasi waliowahi kushindwa kutekeleza majukumu yao na kutahadharisha kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watendaji watakaowapa kazi wakandarasi wa aina hiyo.
Amelielekeza shirika hilo, kuweka akiba ya asilimia 40 ya nyumba zinazojengwa kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha chini ili waweze kukodi nyumba hizo.
Amelipongeza shirika hilo kwa kazi nzuri na kulitaja kuwa miongoni mwa mashirika bora nchini.
Kuhusu wizara ya ardhi, rais amesema, wizara hiyo, imepunguza migogoro ya ardhi na kuwataka kuhakikisha kila mwananchi anapata hati halali kupitia kliniki za ardhi zitakazoanzishwa.
Katika hatua nyingine, Dk. Mwinyi ameziagiza Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, kuacha kujenga nyumba za watumishi wake.
Badala yake, ametaka kununua nyumba bora zinazojengwa na Shirika la Nyumba ili kupunguza gharama.
ZINAZOFANANA
China yazindua ukarabati Tazara
Serikali yaanza kuonja kibano cha kimataifa
Mtanzania aliyeuawa Israel azikwa