BARAZA la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, limetaka wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama wawajibike, au kuwajibishwa na mamlaka zao za uteuzi, kutokana na matendo maovu waliyofanyiwa raia, wakati wa maandamano ya 29 Oktoba. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).
Akisoma tamko la baraza hilo, leo Jumamosi, tarehe 15 Novemba 2025, baada ya siku nne za tafakari na sala, Rais wa Baraza hilo Askofu Wolfgang Pisa, amesema, hasira ya wananchi ipo katika kuona hakuna anayewajibika kwa matendo maovu yaliyofanyika.
Amesema, “Taifa limeumizwa na liko katika hatari ya kugawanyika zaidi, hivyo ni muhimu kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wote wawajibike, au kuwajibishwa na mamlaka zao za uteuzi, ili kurejesha matumaini, haki na amani.”
Maaskofu wamesema, viongozi na mamlaka lazima walipe umuhimu tukio hilo la maafa; wakiri ukweli, watoe pole kwa familia na kukemea mauaji yaliyofanyika wakisisitiza kuwa “waliouawa ni ndugu zetu.”
Amesema, kwakuwa jambo hilo limesababisha maafa, baraza linashauri ufanyike uchunguzi utakaowashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.
TEC imependeza uchunguzi huo, kushirikisha wadau wasiyofungamana na upande wowote, kama jumuiya na taasisi za kimataifa, dini na asasi za kiraia; na wataalamu wa haki na mambo ya kidemokrasia na serikali iwe tayari kupokea na kufanyia kazi ripoti watakayoitoa.
Aidha, maaskofu wanawahimiza viongozi wote kuishi kwa uadilifu, ukweli na uwajibikaji; wote waliokamatwa kabla, wakati au baada ya uchaguzi kwa hila na bila mashauri ya haki, waachiwe huru bila masharti.
Kauli ya taasisi hiyo yenye ushawishi mkubwa nchini, imekuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutangaza kuwa serikali imeunda tume maalumu ya kuchunguza matukio yaliyotokea wakati wa maandamano hayo.
Alisema, “Serikali imechukua hatua ya kuunda tume itakayochunguza kwa undani kilichotokea ili tujue kiini cha tatizo.”
Alisema, taarifa ya tume hiyo, ndio itakayotuongoza kwenye mazungumzo ya kuleta maridhiano na kudumisha amani.
Rais alitangaza pia msamaha kwa vijana waliokamatwa kufuatia maandamano ya siku tatu yaliyofanyika kuanzia siku ya uchaguzi – 29 Oktoba 2025.
Maandamano hayo yaliripotiwa kusababisha vifo vya watu kadhaa, wengine kujeruhiwa, na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Takribani vijana 600 walikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uhaini na uchochezi wa kuhamasisha umma kwenye maandamano ya kupinga uchaguzi huo.
Hata hivyo, serikali kupitia kwa aliyekuwa waziri wake wa mambo ya nje, Mohamed Thabit Kombo, imeeleza kuwa haifahamu idadi kamili ya waliouawa au hasara iliyopatikana.
Katika uchaguzi huo, tume ya uchaguzi, ilimtangaza Samia kuwa mshindi kwa kupata karibu asilimia 98 ya kura zinazodaiwa kupigwa.
Kuhusu kufufuliwa kwa mchakato wa Katiba mpya, TEC limetaka mchakato huo kuanza mara moja kwa kushirikisha wadau wote ili taifa lisirudi kwenye machafuko.
TEC imewaalika Watanzania kuendelea kusali ili haki, amani, ukweli na uponyaji viweze kurejea, huku ikiwafariji waliopoteza wapendwa na kuwaombea majeruhi wapone kwa haraka.
Baraza hili limesema, limethibitika kuwa baadhi ya waliopoteza maisha, miili yao haijapatikana na kwamba inasikitisha kuwa baadhi ya watu walipotaka kuwazika wapendwa wao, hawakuikuta miili yao.
TEC imeomba kama wadau wengine walivyokwisha omba kuwa ni hekima na busara kuwapatia wanafamilia miili ya wapendwa wao wakaipumzishe au kuisitiri kwa heshima kadiri ya imani ya dini, mila, desturi na tamaduni zao.
“Imani yetu inatufundisha kuwa kuna maisha baada ya kifo na kifo ni kuanza maisha mapya na pia miili hii itafufuliwa siku ya mwisho maana parapanda italia wafu watafufuliwa wasiwe na uharibifu nasi tutabadilika (1 Kor. 15:52),” amesema Pisa, rais wa TEC na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi.
ZINAZOFANANA
Shinikizo la kufanyika uchunguzi wa mauaji ya 29 Oktoba lashika kasi
Meridianbet yaendelea kuwekeza kwa jamii kupitia MRC Rehabilitation Centre
Samia atangaza msamaha kwa waandamanaji