November 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Watumishi LHRC wadai kukamatwa na Polisi

 

WAFANYAKAZI wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), waliokuwa wakifanya kazi katika hoteli ya White Sands, jijini Dar es Salaam, wamekamatwa na polisi, jana tarehe 13 Novemba 2025, majira ya saa 9 usiku. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa LHRC, timu ya wafanyakazi wa kituo hicho, ilikuwa ikitekeleza majukumu yake ya kawaida hotelini hapo, kabla ya kukamatwa.

Wanasema, waliowakamata walijitambulisha kuwa ni maofisa wa usalama; walivamia eneo hilo usiku na kuwahoji kwa muda mrefu.

“Wafanyakazi wetu wamekamatwa na kubughudhiwa,” imeeleza taarifa iliyotolewa na shirika hilo kwa umma.

Shirika hilo limeongeza, “Waliowakamata watumishi wetu, wameondoka na vifaa vyao kadhaa ikiwemo kompyuta mpakato, vitambulisho na simu za mikononi.”

Taarifa hiyo inasema, wafanyakazi hao walichukuliwa na kufikishwa kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO), walikohojiwa kuanzia majira ya saa 10 asubuhi.

Baadhi ya vifaa hivyo, vimerejeshwa bila masharti, ingawa haijathibitishwa kama usalama na uadilifu wa taarifa zilizomo kwenye vifaa hivyo.

LHRC imesema ina wasiwasi mkubwa juu ya mazingira ya tukio hilo, ikieleza kwamba linaashiria ongezeko la vitendo vya matumizi makubwa ya nguvu na vitisho dhidi ya wanaharakati na wananchi wanaotekeleza kazi za utetezi wa haki za binadamu.

“Tunatiwa wasiwasi zaidi kwamba tukio hili limetokea wakati ambapo Jeshi la Polisi Tanzania limehusishwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi na vitisho dhidi ya wananchi, hali ambayo sasa imewafikia wafanyakazi wetu,” imesema taarifa hiyo.

Kituo hicho kimeeleza kuwa licha ya kurejeshewa vifaa vyao, kinaendelea kufuatilia ili kuhakikisha usalama wa watetezi wa haki za binadamu unaimarishwa na kwamba hakuna taarifa yoyote itakayopotea au kutumiwa vibaya.

Shirika hilo limesisitiza kuwa litaendelea kulinda na kutetea haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, sheria na mikataba ya kimataifa, huku kikitoa wito kwa vyombo vya dola kuheshimu mipaka ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.

Fulgence Massawe, Kaimu Mkurugenzi wa kituo hicho, ameliambia MwanaHALISI Digital, kwamba uvamizi huo umeongeza wasiwasi wa utendaji kazi kwa taasisi za uteetzi wa haki za binadamu nchini.

Amesema, tukio hilo liliwalenga moja kwa moja wafanyakazi wa kituo hicho, na kuongeza, “hii siyo mara ya kwanza, kukutwa na madhira hayo.

Juhudu za gazeti hili kumpata msemaji wa polisi, kuzungumzia jambo hilo, bado hazijafanikiwa. Tunaendelea kumtafuta.

About The Author

error: Content is protected !!