November 10, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yaweka pingamizi kesi ya Heche dhidi ya IGP

John Heche, Makamu wa Mwenyekiti wa Chadema

 

UPANDE wa Jamhuri umeweka pingamizi kwenye kesi John Heche, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyomshtaki Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP) na wenzake kwa kumshikilia kinyume cha sheria, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu masjala ndogo ya Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika kesi hiyo ambayo inasikilizwa mbele ya Jaji Obadiah Bwegoge, Heche kupitia mawakili wake wameiomba mahakama hiyo iamuru afikishwe mahakamani au kupatiwa dhamana.

Heche alikamatwa na Polisi tangu tarehe 22 Oktoba 2025, alipokuwa anaingia mahakamani hapo kwa lengo la kusikiliza shauri la uhaini linalomkanili Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema.

Leo tarehe 10 Novemba 2025, upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Agatha Pima aliieleza mahakama hiyo kuwa kabla ya kuendelea na kiapo kinzani, serikali imekuja na pingamizi kuhusiana na shauri hilo pamoja na leo kuwasilisha kiapo kinzani kwa mawakili wa Heche kama walivyoagizwa na Mahakama.

Wakili Selemani Matauka ambaye anaongiza jopo na mleta maombi (Heche) alithibitishia mahakama hiyo kupokea pingamizi la Jamhuri nusu saa kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo na kuomba ahirisho la kesi hiyo kwa ajili ya kujibu hoja hizo zilizopo kwenye pingamizi lao.

Mara baada ya kusikiliza kwa pande zote mbili, Mahakama iliahirisha shauri hilo mpaka tarehe 13 Novemba 2025, Saa nne asubuhi.

About The Author

error: Content is protected !!