Tundu Lissu akiwa mahakamani
SHAURI la uhaini linalomkabili Tundu Lissu, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini – CHADEMA, limeahirishwa hadi Jumatano ya 12 Novemba, kwa kile kilichoelezwa kuwa “sababu za kiusalama.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Uamuzi wa kughairisha shauri hilo leo, umefanywa na Mahakama Kuu, baada ya maombi ya upande wa mashitaka.
Kesi dhidi ya mwanasiasa huyo machachari nchini, ilipangwa kuendelea leo Jumatatu, tarehe 10 Novemba 2025, ambapo upande wa mashitaka ulitatajiwa kuendelea kuleta mashahidi wake.
Upande wa mashitaka ulisema mahakamani hapo kuwa ulipanga kumleta shahidi wake wa nne leo, lakini imeshindwa kufanya hivyo, kutokana na kuibuka ghasia katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kufuatia maandamano ya siku tatu ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba 2025.
Mashahidi wanaotoka mikoa ya Ruvuma na Mbeya wameshindwa kusafiri kufika jijini kutokana na changamoto hizo za kiusalama.
Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashitaka, hali hiyo imeathiri mchakato wa mashahidi kufika, na hivyo kufanya kesi ishindwe kuendelea kama ilivyopangwa.
Wakili wa Serikali Mkuu, Thawabu Issa, aliieleza Mahakama kuwa ombi la kuahirisha linatolewa chini ya kifungu cha 302(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 (Toleo la 2023), akibainisha kuwa mashahidi wameshindwa kufika kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.
Jamhuri iliomba kesi iahirishwe kwa siku 14, lakini Jaji Danstan Ndunguru aliamua kuhahirishwe kwa siku mbili na kueleza kuwa siku hizo ni nyingi na kwamba shauri hilo litaendelea Jumatano ijayo.
Wakili wa Lissu, Rugemeleza Nshalla, aliyeeleza kuhusu kuhairishwa kwa sababu ya usalama amesema wao wameweza kufika mahakamani maana yake hali inaruhusu wengine kufanya hivyo.
“Na tunafahamu kuwa mashahidi wengine ni wale wa kufichwa hata sijui usalama wao unahatarishwa vipi,” alihoji Nshalla.
Akaongeza, “Bahati mbaya mwenyekiti anajiwakilisha mwenyewe, hivyo hakuweza kuzungumza, tunatumaini kwamba umma ungependa kujua nini kinaendelea.”
Mwishoni mwa wiki, Makamu wa Rais, Balozi Emmanuel Nchimbi, alinukuliwa akisema, hali ya nchi iko shwari na serikali imechukua hatua za kurejesha utengemano nchini.
Katika maandamano hayo, watu kadhaa wameripotiwa kupoteza maisha huku mali za umma na binafsi zikiharibiwa.
Waandamanaji walikuwa wakitaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki lakini mamlaka nchini, lakini serikali inadai maandamano hayo yalikuwa kinyume cha sheria na yaligubikwa na ghasia na uharibifu.
Bado taarifa rasmi haijatolewa kuhusu tathmini ya madhara yaliyotokea. Maandamano hayo, ni makubwa zaidi kuwahi kutokea kuhusu uchaguzi tangu Tanzania kupata uhuru wake, miongo ya sita iliyopita.
Duru mbalimbali za ndani na nje ikiwemo wapinzani, wanaharakati na wanadiplomasia, zinaeleza kuwa mamia ya watu wameuawa na vyombo vya usalama ikiwemo polisi. Serikali imekanusha madai hayo.
Maandamano yalianzia jijini Dar es Salaam na kusambaa katika maeneo mengine ikiwemo majiji ya Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma, pamoja na maeneo mingine ya Tanzania.
ZINAZOFANANA
Chadema yalaani kukamatwa viongozi wake
Heche akimbizwa hospitali, Lema, Jacob wakamatwa
Watu 172 kortini kwa kufanya vurugu, unyang’anyi siku ya Uchaguzi