November 27, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Waongoza watalii wafunguka maandamano wakazi Ngorongoro

 

BAADHI ya waongoza watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, jijini Arusha, wamewataka watu wanaohamasisha wakazi waishio hifadhini humo kuandamana kuacha kwani kitendo hicho kinachafua taswira ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Wito huo umetolewa ikiwa zimepita takribani siku nne tangu wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro kuingia barabarani kufanya maandamano wakiitaka Serikali kufanyia kazi malalamiko yao ikiwemo uboreshwaji wa huduma za kijamii.

Gidion Joseph, muongoza watalii katika hifadhi hiyo, amesema maandamano hayo yanaweza yakasababisha vurugu na kuathiri shughuli za utalii ambazo kwa sasa zimeimarika kutokana na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutangaza suala hilo kimataifa kupitia filamu ya Royal Tour.

“Ningependa kukemea watu wanaoendelea kuchochea kuhusu suala la wamasai, kiukweli si jambo zuri kuchochea ili kuleta mgoml shughuli za utalii zisimame zisiendelee, sio jambo zuri,” amesema Joseph.

Joseph amesema “nchi inapata mapato kupitia utalii, tunapata huduma kupitia fedha za kigeni zinazotokana na watalii. Watu wasitumike kuchochea vurugu kwa ajili ya maslahi ya watu wachache.”

Aidha, Joseph amesema maandamano hayo hayajazuia shughuli za utalii hifadhini humo, kwani wanaendelea kuwahudumia wageni kama kawaida.

“Kiukweli niuchukue nafasi hii kuwaeleza watu wanaopotosha kuwa Ngorongoro si salama, kiukweli iko salama Mimi nilikuwa na wageni nimewatembeza na wamefurahia sana,” amesema Joseph.

Naye Daniel Bayo, ameshauri sintofahamu inayoendelea Ngorongoro itafutiwe ufumbuzi ili iendelee kuwa shwari.

“Ngorongoro usalama upo wa kutosha na ninavyoongea nimetokea Serengeti nilikuwa siku tano hivyo Ngorongoro ni shwari. Tanzania ni ya kwetu, tukiichafua sote tumechafuka,” amesema Bayo.

Baadhi ya wakazi wa Ngorongoro wameandamana wakimtaka Rais Samia afike hifadhini hapo kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero zao.

About The Author