November 4, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Dk. Mpango amkabidhi Nchimbi ofisi leo

 

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amempongeza na kumshukuru Makamu wa Rais Mstaafu Dk. Philip Mpango kwa mchango aliyoutoa wakati wa kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Sita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa makabidhiano ya Ofisi ya Makamu wa Rais, yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma. Amesema kazi kubwa imefanyika katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Sita, ambayo ilitoa urahisi wakati wa ufanyaji kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Makamu wa Rais amesema ataendeleza jukumu la kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwezo wake wote ili kutekeleza vema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia amemsihi, Makamu wa Rais Mstaafu, Dk. Philip Mpango kuendelea kutoa mchango wake pale utakapohitajika, katika utekelezaji wa sera mbalimbali za Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwemo masuala ya uchumi wa buluu.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Mstaafu Dk. Philip Mpango amempongeza Makamu wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi kwa nafasi hiyo muhimu na kumsihi kutekeleza vema majukumu ya kuwa mshauri namba moja wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia amemsihi kutumia hekima na unyenyekevu wakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya kuwahudumia wananchi.

About The Author

error: Content is protected !!