
TUNDU Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anaenndelea na kumuuliza maswali ya dodoso (cross examination), shahidi wa pili wa serikali John Kaaya ‘Afisa wa Polisi anayeshughulika na doria la ya uhalifu mtandaoni ambapo wiki iiyopita Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam iliahirisha shauri hilo Na. 19605/2025 kutokana na pingamizi liliwasiishwa na upande wa Jamhuri juu ya hatua ya Lissu ya kutaka kulinganisha maelezo aliyoyatoa shahidi mahakamani hapo kama yanalingana na maelezo yake aliyotoa polisi.
Shauri hilo linalosikilizwa na jopo la majaji wa tatu linaloongozwa na jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu , Kanda ya Iringa Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Jaji James Karayemaha, na Jaji Ferdinand Kiwonde.
Uamuzi kama ifuatavyo, “Mtakumba siku ya Ijumaa tarehe 10 Oktoba, wakati shahidi anaendelea kutoa ushahidi, mshitakiwa alitarajia kumdodosa Shahidi kuhusu maelezo yake aliyotoa Polisi na kulinganisha na yale aliyotoa hapa mahakamani. Upande wa Mashitaka ukaweka pingamizi.
“Pingamizi hilo lilisema taratibu hazijafuatwa wakati wa kutaka ku impeach shahidi na hivyo walijikita hapo upande wa Mashitaka.
“Kwamba hatua ziko tatu ambazo ni kusoma maelezo, kufanya ulinganifu na baadae kuomba yapokelewe. Yeye alifanya hatua ya kwanza na kuhamia ya tatu hii ya Pili hakuipitia kwa mujibu wa kesi mbalimbali. Kifungu cha 163 cha Sheria ya Ushahidi kimeeleza bayana.
“Kwa kuzingatia hayo mahakama inakubali na kuyapokea maelezo hayo kuwa sehemu ya ushahidi wa upande wa utetezi” – uamuzi wa majaji.”
Shauri linaendelea Lissu anaendelea alipoishia na kumtaka shahidi kuyatambua maelezo yake ambayo shahidi ameyatambua na kuomba mahakama kutaokea kama kielelezo chake (utetezi).
Majaji wamekipokea kielelezo hicho na kuwepewa jina la utambuzi kama exhibit D1 kielelezo cha ushahidi wa utetezi .
Lissu anaendelea na dodoso kupitia kielelezo hicho kwa shahidi kama ifuatavyo:-
Anapatiwa hapa Shahidi kielelezo chake.
Lissu: Tarehe 09 Oktoba ukiwa unatoa ushahidi uliiambia mahakama kwamba uliajiriwa Polisi Februari 2006?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Sasa soma mstari wa kwanza wa maelezo yako?
Kaaya: Mimi ndie mwenye majina nimeajiriwa na Polisi Mwaka 2005.
Lissu: Kwahiyo kumbe ni 2005 ndio uliajiriwa.
Lissu: Ni kweli au si kweli ulisema kwamba ulipata mafunzo ya upolisi kwenye chuo cha polisi Zanzibar?
Kaaya: Ni ya kweli.
Lissu: Hayo maelezo yapo kwenye hiyo statement yako ya polisi?
Kaaya: Hayapo.
Lissu: Nilijifunza sheria mbalimbali na kazi za polisi, First Aid na mambo mengine. waeleze majaji kama hayo yapo?
Kaaya: Nimeyapata kwenye vyuo mbalimbali ikiwemo chuo cha polisi Kurasini, Moshi.
Lissu: Chuo cha Polisi Zanzibar na uliyojifunzia Zanzibar yapo?
Kaaya: Huwezi ajiriwa na Jeshi la Polisi bila kujifunza kwahiyo nilienda vyuo vingi.
Lissu: Usipoteze muda.
Kaaya: Naomba nipewe muda nijieleze.
Lissu: Hakuna kujieleza hapa we jibu maswali
Kaaya: Hayo ya Zanzibar kiukweli hayapo.
Lissu: Kwenye ushahidi wako hapa mahakamani baada ya hayo mafunzo Zanzibar ulitunikiwa cheti certificate of competence?
Kayaa: Ni kweli.
Lissu: Yapo wapi kwenye maelezo yako?
Kaaya: Waheshimiwa majaji hayapo.
Lissu: Ulisema hapa mahakamani kuwa uliajiriwa kama ‘Police Constable’ 2006 hadi 2021 ulipokuwa ‘special sargeant’?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Ongeza sauti wewe polisi.
Lissu: Waeleze majaji kama hicho cheo cha ‘special sargeant’ kipo kwenye vyeo vya polisi hapa Tanzania.
Kaaya: Nilisema nimehudhuria mafunzo ya ‘special sargeant’ na sio cheo cha special Sergent.
Lissu: Waheshimiwa majaji someni mlichoandika mtusaidie alisema nini tafadhali sana nawaombeni.
Jaji: Alipandishwa cheo cha rank ya ‘special sergeant’.
Lissu: Sasa tuambie katika muundo wa jeshi la polisi kama hicho cheo kipo?
Kaaya: Hicho cheo kipo ndio maana hayo mafunzo yalikuwepo na nilihudhuria.
Lissu: Je huo ushahidi wa ‘special sargeant uko wapi kwenye maelezo yako ya Polisi?
Kaaya: Waheshimiwa majaji hayapo.
Lissu: Ni kweli kwamba ulisema ulipokamilisha hayo mafunzo ulipewa cheti cha kushiriki hayo mafunzo na useme kama umeandika kwenye maelezo yako?
Kaaya: Ni kweli nilisema na ni kweli kuwa hayapo kwenye maelezo yangu. Nilisema hapa mahakamani pekee.
Lissu: Je ni kweli au si kweli ulisema mwezi Oktoba 2021 ulipelekwa kwenda kusomea Assistant Inspector kule Moshi?
Kaaya: Ni kweli
Lissu: Yako wapi hayo kwenye maelezo yako ya polisi?
Kaaya: Hayapo.
Lissu: Ni kweli au si kweli kwa ushahidi wako baada ya mafunzo ya ‘Assistant Inspector’ ilipofika Februari 2022 ukafuzu na kupata cheti cha mahudhurio?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Hivi kwanini huongezi sauti?
Kaaya: Sawa nitaongeza.
Lissu: haya jibu swali?
Kaaya: Hayo maelekezo hayapo kwenye maelezo yangu ya Polisi.
Lissu: Waeleze majaji kama ni kweli tarehe 09/10 ulisema hapa mwezi June 2025 ulipandishwa cheo na kuwa full Inspector kwasababu ya utendaji kazi mzuri?
Kaaya: Ni kweli majaji.
Lissu: Waeleze sasa hayo mambo mema kama yapo kwenye maelezo yako ya polisi?
Kaaya: Na yenyewe hayapo.
Lissu: Ulienda kwenye mafunzo ya miezi miwili kuanzia Januari hadi Machi 2020 ulijifunza forensic investigation in modern science?
Kaaya: Nilisema lakini hayapo kwenye maelezo yangu ya polisi.
Lissu: Ni kweli au sio kweli kwenye ushahidi wako wa Tarehe 9 Oktoba, ulisema ulipata mafunzo ya Sissco certified support in Cyber security?
Kaaya: Ni kweli nilisema.
Lissu: Yako wapi kwenye maelezo yako?
Kaaya: Hayapo
Lissu: Sasa kwanini hutoi sauti polisi?
Kaaya: Natoa.
Lissu: Haya toa basi.
Kaaya: Sawa natoa.
Lissu: Waeleze majaji kama ni kweli ulisema vilevile ulisomea computer Hacking katika chuo cha Unique Academy pale Upanga?
Kaaya: Nilisema kweli hapa mahakamani.
Lissu: Ulisema kama umesomea computer Hacking?
Kaaya: Sikusema.
Lissu: Kwamba mafunzo yalichukua miezi miwili yaani wiki 8?
Kaaya: Ni kweli nilisema ila kwenye haya maelezo hapa sijaandika.
Lissu: Ulisema ili mtu yeyote kuweza kutumia mitandao ya Kijamii mtumiaji huyo anatakiwa kujisajili kwa kuweka taarifa zake ili zionekane na watumiaji wengine?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Pia ulisema ukiwa unajisajili unapata ‘username’ jina lako, password na email address unaviweka?
Kaaya: Ni kweli ila sikusema unaweka nilisema unaandaa.
Lissu: Basi ni sawa jibu sasa swali langu kama hayo maelezo yapo kwenye hayo maelezo yako ya Polisi.
Kaaya: Hayapo kabisa.
Lissu: baada ya kuandaa yote hayo unaingia kwenye uwanja wa mtandao husika kwa kadri ya maelekezo utakayopewa?
Kaaya: Ni sahihi nilisema hapa lakini kwenye maelezo niliyotoa Polisi haupo, usije sema nisome wakati sikuandika.
Lissu: Ulisema kuhusu ukurasa wa mtumiaji yaani user page?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je upo kwenye maelezo yako ya polisi?
Kaaya: Haupo.
Lissu: Baada ya hapo ulisema hivi kwamba kwenye YouTube ukiingia, unaweka username na email address na password na baada ya hapo unajaza taarifa.
Kaaya: Sikusema neno kuandaa.
Lissu: Haya tutumie neno la kuandaa. kwahiyo unaandaa nilivyotaja hapo juu. Wakati gani sasa?
Kaaya: Wakati unajisajili.
Lissu: Baadae unapewa masharti ya kuingia si ndio baada ya hapo?
Kaaya: Ndio
Lissu: Then unapewa URL?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Sasa waeleze majaji kama yapo kwenye maelezo yako, ukisema kwa sauti polisi inapendeza sana?
Kaaya: Hayapo kabisa.
Lissu: Kwa ushahidi wako ukishapata hiyo channel system locator ni unique ID isiyoweza kutimika na mtu yeyote?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je yote hayo yako kwenye maelezo yako polisi?
Kaaya: Hayapo.
Lissu: Ulisoma Data protection na ethical computer Hacking?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Yako wapi kwenye hilo karatasi uliloandika polisi?
Kaaya: Hayako. Sikuandika.
Lissu: Kwamba ulipata cheti pia?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Yako wapi?
Kaaya: Hakuna.
Lissu: Kuhusu maandalizi yako ukifika asubuhi kazini kwenye maelezo uliandika?
Kaaya: Sikuandika.
Lissu: ‘Police notebook’ umeisema sana.
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Umeileta mahakamani.
Kaaya: Sijaileta kwasababu…
Lissu: Sababu isubiri kwanza, utaitoa siku nyingine.
Lissu: Kuhusu kukagua vifaa vyako kabla ya kazi pia?
Kaaya: Nilisema lakini sikuandika kwenye maelezo yangu ya polisi.
Lissu: Ulisema unayo program na software inayokuwezesha kufanya doria mtandaoni?
Kaaya: Nilisema ndio.
Lissu: Kwenye maelezo hayo uliyoshika yapo?
Kaaya: Hayapo kabisa.
Lissu: Twende kwenye ya Tarehe 4 Aprili 2025, ulisema hapa kwamba ulifika ofisini saa 12 asubuhi?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je umeandika hayo?
Kaaya: Sikuandika.
Lissu: Kwamba ulikuwa na vitendea kazi pia ulisema?
Kaaya: Hayo yapo ila ‘notebook’ lakini haipo, sikuandika.
Lissu: Ulivyoanza kuperuzi ulikutana na maneno Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia majimboni No Reforms, No Election njia panda.
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Na ukaeleza kwamba uliangalia hiyo video yote.
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Kwa ushahidi wako ulisema uliangalia hiyo video kwasababu ulikuwa na wasikiliziaji elfu 39?
Kaaya: Si kweli nilisema watazamaji elfu 39.
Lissu: Basi twende na hao watazamaji uliosema.
Lissu: Kwahiyo kilichokufanya ni hao watazamaji elfu 39 na comment 300?
Kaaya: Ni sahihi.
Lissu: Je hayo yapo kwenye maelezo yako Polisi.
Kaaya: Hayapo.
Lissu: Katika ushahidi wako umeeleza ulivyomaliza kuangalia hiyo video na wakati unaiangalia ulichukua ‘police notebook’ yako na kuwa unaandika baadhi ya maudhui?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: je kama uliandika kwenye maelezo yako polisi wambie majaji?
Kaaya: Hebu rudia.
Lissu: Je ulisema ulikuwa na ‘notebook’ na kuandika uliyokuwa unayaona na kama hayo umeandika kwenye maelezo yako?
Kaaya: Taarifa hizo zipo lakini polisi notebook sijaandika kwenye maelezo yangu.
Lissu: Ulisema baadae ulimpa taarifa kiongozi wako wa dawati la doria mtandaoni na je upo kwenye maelezo yako Polisi?
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Waheshimiwa majaji naomba msomeeni shahidi, akumbushwe alichosema.
”Mahali aliposema baada ya kutazama hiyo video alipomaliza kutazama na kuandika maudhui kwenye notebook ndipo alimjulisha mkuu wake wa kitengo na akamwambia aende kutoa taarifa kwa George”
Jaji: Baada ya kuandika matukio yote kwenye ‘notebook’ yangu.
Lissu: Shahidi sasa wambie majaji kama hayo waliyokusomea yapo kwenye maelezo yako polisi?
Kaaya: baadhi hayapo.
Lissu: Yapi hayo ambayo hayapo.
Kaaya: Hayo ya ‘Polisi notebook’.
Lissu: Je ya saa nne?
Kaaya: Na yenyewe hayapo.
Lissu: Ulisema umeenda kutoa taarifa kwa SSP George, ambae amepanda cheo juzi hapa?
Kaaya: Sina taarifa kama amepanda cheo.
Lissu: Ulienda kumuona saa nne na ulipomaliza ni saa nne hiyo hiyo sasa uliwezaje?
Kaaya: Saa moja ina dakika 60 kwahiyo kwenye hiyo mida ya saa nne ndio nilimaliza hayo yote.
Lissu: Ulipofika kwa SSP George ulimueleza ulichoona kwenye mtandao wa YouTube.
Kaaya: Ni sahihi nilimuonensha kwa simu yangu.
Lissu: Na ni kweli ulimuonesha baadhi ya vipande vilivyokuwa na viashiria vya jinai na ulimuonesha vipande vipande?
Kaaya: Ni sahihi.
Lissu: Je hayo maelezo yapo kwenye maelezo yako ya polisi?
Kaaya: Hayapo.
Lissu: Ni kweli ulisema ulimuonesha video ukisoma maelezo yako ya polisi na hujafafanua kama ulimuonesha vipande au laaa?
Kaaya: Sikuandika kama nimemuonesha.
Lissu: Ulieleza pia hapa mahakamani kwamba wakati unamuonesha SSP George hiyo video clip na yeye alichukua ‘police notebook’ yake na kujaza taarifa anazoona?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je hayo kuhusu afande George kama yapo kwenye maelezo yako polisi waambie majaji?
Kaaya: Hayapo.
Lissu: Angalia maelezo yako kwa makini tena halafu ukimaliza waeleze majaji kama umesema chochote juu ya Tarehe 07 Aprili 2025, chochote yani hata kusema tarehe yenyewe.
Kaaya: Kipo.
Lissu: Kiko wapi?
Lissu: Anamkumbusha alichosema hapa mahakamani kuhusu tarehe 7 Aprili.
Lissu: Je yapo kwenye maelezo?
Kaaya: Hayapo ndio, nilishakujibu.
Lissu: Ulisema pia hapa mahakamani flash disc aina ya XIOXIA yenye GB 8. Sasa waeleze kama ipo kwenye maelezo yako polisi?
Kaaya: Hiyo XIOXIA haipo kweneye maelezo yangu polisi.
Lissu: Siku hiyo ya tarehe 7 Aprili watazamaji walikua wamefikia takribani elfu 52?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Hilo nalo lipo polisi?
Kaaya: Sikuandika kwenye maelezo.
Lissu: Ulisema comments zilikuwa bado 300?
Kaaya: sikumbuki.
Lissu: Sasa nikikuuliza kama comments zilikuwa 300 ni ushahidi wa uongo utasemaje?
Kaaya: Si kweli.
Lissu: Siku unatoa ushahidi hapa tarehe 09 Oktoba saa 7 na dakika 45 ilikuwa na comments 144?
Kaaya: Si kweli kwasababu mimi siijui.
Lissu: Pia ulisema uliifanyia encryption na kuiwekea password?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je hilo nalo lipo kwenye maelekezo yako ya polisi?
Kaaya: Halipo.
Lissu: Pia ulisema kwamba George alikwambia upakue, PF 147 ulijaza na kuimark DM na baada ya hapo SSP GEORGE majira ya saa 9 mchana ukamwambia kuwa nimeshafanya hilo?
Kaaya: Ni sawa.
Lissu: Akachukua diary (shajara) yake na kukwambia tayari amefungua kesi/jalada?
Kaaya: Kweli.
Lissu: Je hayo yote yapo?
Kaaya: Shahidi anajibu kwa kutungisha kichwa.
Lissu: Unamaanisha nini kufanya hivyo?
Kaaya: hayapo.
Lissu: Ulisema kwamba ulimpelekea Peter Malugala hicho kielelezo ambae ni mtunza vielelezo?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Sasa waeleze majaji kama katika maelezo yako uliandika haya na hata kutaja jina la Peter Malugala.
Kaaya: Halipo.
Lissu: Malugala alijaza form Na. PF. 16 kama yapo kwenye maelezo yako polisi?
Kaaya: Hayo hayapo.
Lissu: Tarehe 8 Aprili uliitwa tena na SSP George ofisini kwake. Je hayo maelezo yako polisi?
Kaaya: Hayapo kwenye maelezo yangu Polisi.
Lissu: SSP George alikuuliza kuhusu picha mjongeo na akakuelekeza umpatie mpelelezi password ya hiyo video na ukaangalia password hiyo kwenye notebook ya mpelelezi?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je yapo kwenye maelezo polisi?
Kaaya: hayapo kwenye maelezo yangu ya Polisi.
Lissu: Je wakati unautoa ushahidi wako mahakamani ulisema chochote kwanini uliyosema mahakamani hayapo kwenye maelezo yako ya polisi?
Kaaya: Hayo maelezo sikutoa.
Lissu: Kwanini mwaka wako uliotaja mahakamani ule 2006 na ule 2005 uliousema polisi ulieleza kwanini zinatofautiana?
Kaaya: Halipo hilo.
Lissu: Umewahi kuhudhuria Shule ya Msingi?
Kaaya: 1989 hadi 1995 nilisoma Nganyeni na Ryakilimu huko Marangu Primary School.
Lissu: Je sekondari umewahi soma?
Kaaya: Nimeanza mwaka 1996 na kuhitimu 1999 shule ya sekondari Lyakilimu.
Lissu: Ni sahihi nikisema ulimaliza form four ‘kidato cha nne’ hapo?
Kaaya: Sahihi.
Lissu: Ulipata division ngapi?
Amesimama Wakili wa Serikali kuwa anapinga swali la kumuuliza shahidi ufaulu wake. Kifungu cha 167 cha sheria ya ushahidi kinasema jambo hilo sio relevant kabisa. Kikubwa amemaliza shule mengine ni siri ya shahidi.
Anasimama Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga, nae anasema swali hilo linalenga kutaka nini? kifungu cha 164 kinasema kwanini maswali ya namna hii yanaulizwa. Tukiacha hili ataulizwa una wake wangapi?
Lissu: Waheshimiwa majaji mimi siulizi swali bila sababu ya kiushahidi.
”Suala la elimu ya shahidi limejitokeza sana katika examination in Chief. Wameeleza vyuo alivyopitia, Moshi na Zanzibar. Wameeleza extensively, Wangetaka tusiyajue wasingeyaanzisha, wameanzisha wavumilie”,
Swala la academic qualification linahusu namna gani maafisa wa polisi wanaajiriwa. O.54(1) ya PGO inahusu namna wanavyoajiriwa. Anaisoma hapa. Kama alipata zero alipaswa kuwa police officer huyu”alieleza Lissu.
PGO pia inasema PGO 53(10) on promotions on Inspectorate shall normally be to personnel with the following qualifications including form four qualifications.
Was he fit to be promoted to Inspectorate?kama alipata zero ajibu tu, haya mambo waliyaleta wenyewe. Wavumilie sasa muda huu”ameendelea Lissu.
Lissu: Mbona nimeuliza ya shule ya Msingi hamjasema kitu. Mmeanza kulalamika nilipofika kwenye form four? Mmeyataka: Mtapata.
Anasimama Katuga: Tumesikia Majibu ya Mshitakiwa hajaelewa pingamizi letu. Hatujapinga, elimu yake ya shule ya msingi. Suala la Division sio relevant kabisa.
“Na PGO haijasema apate division ngapi? Imezungumzia elimu kwa ujumla. Kwanza ufaulu wa form four ni kuanzia Division one, two, three na Four. Hizo zote ni ufaulu,”
Jaji: Mahakama imewasikiliza na kuona muishie hapo tu, msiende kwenye alipata nini?
Lissu: Je ulisoma kidato cha tano na sita?
Kaaya: Sikusoma.
Lissu: Waeleze majaji kama una advanced Diploma ya kitu chochote?
Kaaya: Ninayo.
Lissu: Ya nini?
Kaaya: Refrigeration na air condition advanced diploma. Nilisoma Nairobi.
Lissu: Umesoma maswala ya mafriji chuo gani?
Kaaya: Waheshimiwa majaji naomba mahakama hii isiwe chombo cha kutoa taarifa za mashahidi na isiwe nia ya kudhalilisha. Naomba Mahakama ilinde taarifa zangu binafsi naomba tulizingatie hilo.
Jaji Ndunguru: Shahidi unapaswa kurelax kabisa. Kama kuna swali la kukudhalilisha hatutaruhusu ujibu. Tutaingilia kati. Wewe kama shahidi fanya kazi yako.
“Hayo mengine kwamba yanaandikwa mitandaoni achana nayo. Watu wengine wanaweza kucheka kwasababu hawafahamu
“Mahakama tukiona unatwezwa utu wako tutaingilia hayo ya mitandaoni hatuhusiki nayo na hatuwezi kuyazungumzia hapa,” Jaji Ndunguru.
Lissu: Sasa turudie. Je una Advanced Diploma
Kaaya: Ninayo.
Lissu: Ni ya kitu gani na umepatia wapi?
Kaaya: Advanced diploma Refrigilation and air condition na electrical installation. Nilipata chuo cha ufundi Veta na baadae integlobal college iko Nairobi.
Lissu: Waeleze maana ya NACTE unaifahamu?
Kaaya: Naifahamu.
Lissu: Je hicho chuo kinatambulika na NACTE?
Kaaya: Ndio kinatambulika.
Lissu: Je una shahada ya Chuo Kikuu?
Kaaya: Ninayo.
Lissu: Ipi?
Kaaya: Chuo kikuu huria cha Tanzania.
Lissu: Umesoma nini na lini?
Kaaya: Nina degree ya LL.B mwaka 2019.
Lissu: Kumbe ni Mwanasheria Mwenzangu. Sasa waeleze majaji kama hayo yote umeyaeleza una shahada ya Sheria.
Kaaya: Sikuandika.
Lissu: Waeleze majaji kama ushahidi wako wa wiki iliyopita na yale maelezo yako ya polisi kuwa una advanced diploma in refrigilation and air condition?
Kaaya: Sijaeleza kabisa..
Lissu: Je ulieleza sababu ya kutokueleza mambo haya matamu ?
Kaaya: Sikueleza.
Lissu: Ulisema umesoma chuo cha Unique Academy?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Hiki ni chuo gani hivi?
Kaaya: Sio chuo kikuu, sio chuo kinachotoa advanced diploma, hiki chuo tulipelekwa maafisa wa polisi. Huwa tunapelekwa maeneo mbalimbali ikiwemo ‘UDOM’ tunaendaga.
Lissu: Ukisema sina uhakika nalo ni jibu. Ukisema sijui nalo ni jibu. Sasa nataka unijibu swali langu hiyo unique academy inatoa diploma ya chochote.
Kaaya: Nafikiri inatoa.
Lissu: Je hicho chuo kinatambulika na mamlaka ya ithibati ya hivyo vyuo vya ufundi?
Kaaya: Sijui kabisa.
Lissu: Shahidi umesema umesomea chuo cha Polisi Zanzibar umepata cheti cha mahudhurio na chuo cha Polisi Moshi na Dar es Salaam na Unique Academy kote umepata vyeti?
Kaaya: Ndio.
Lissu: Sasa nikisema wewe Inspector John Kaaya nikisema huna qualification yoyote nitakuwa nakosea?
Kaaya: Utakuwa unakosea.
Lissu: Soma maana ya Professional qualification kwenye PGO.
Kaaya: Means advanced diploma and above
Lissu: Je kwa tafsiri hiyo ya PGO ambayo ni advanced diploma au shahada ya Chuo kikuu?
Kaaya: Ni sahihi.
Lissu: Kwa hiyo huna qualification ila una vyeti vyeti vya hapa na pale? Kweli au sio kweli?
Kaaya: Sikueleza hayo mambo.
Lissu: Sasa nataka tuzungumze kuhusu masuala ya mtandaoni. Umesema wewe ni mtaalamu, hebu tuambie ulisema lazima ufanye usajili kwanza ili uweze kuingia mtandaoni. Je utaratibu huo ni wa aina hiyo hiyo katika mitandao yote?
Kaaya: Utaratibu unatofautiana.
Lissu: Je YouTube inamilikiwa na Google?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Mtu yeyote mwenye google account anaweza kuingia YouTube?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je ni kweli kwamba ili kuwa na google account unachohitaji kuwa nacho ni username na password peke yake?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je ukiwa na google account unaweza kuingia YouTube?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je ukiwa na gmail account huhitaji channel URL ili kupakua video au kuangalia?
Kaaya: Waheshimiwa majaji nataka nitoe maelezo kidogo. Kwa hiyo sio kweli.
Lissu: Kuna kitu kinaitwa YouTube user account kweli au si kweli?
Kaaya: Ni kitu sawa na URL ni kitu kimoja.
Lissu: Sasa hiyo channel URL umuhimu wake inakuwezesha ukiwa nayo ku like au ku comment kwenye picha za YouTube mitandaoni?
Kaaya: Ni sahihi ukiwa na email inatosha
Lissu: Mtu mwenye hiyo account ya kawaida hiyo ya gmail anaweza kuweka video huko YouTube?
Kaaya: Ni sahihi anaweza hata live streaming anaweza.
Lissu: Kwahiyo ni ushahidi wako kwamba mtu yeyote mwenye gmail account anaweza kurusha video youtube ya JAMBO TV?
Kaaya: Hauwezi kuingia kwenye ukurasa wa JAMBO TV.
Lissu: Sasa waeleze majaji kama ni kweli au si kweli mtu pekee anayeweza kufungua youtube channel kama JAMBO TV, THE CHANZO TV AU MWANZO TV ni mtu mwenye URL ??
Kaaya: Waheshimiwa majaji kipo naona swali lake liko kivingine?
Lissu: Sasa naomba kuuliza swali la mwisho twende break. Je unafahamu aliyefungua youtube channel inayoitwa Jambo TV?
Kaaya: Simfahamu.
Lissu: Je ni nani mwenye password ya JAMBO TV?
Kaaya: Simfahamu.
Lissu: Waeleze majaji kama mtu asiye na hiyo password asiyekuwa operator wa Jambo tv anaweza kuweka kwenye mtandao wa Jambo Tv YouTube?
Kaaya: Huwezi.
Lissu: Waheshimiwa majaji tukale.
Baada ya mapumziko ya saa moja shauri linaendelea kama ifuatavyo;-
Lissu: Shahidi waeleze majaji kwamba hii video iliyosababisha yote haya ilirekodiwa kwenye mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025 makao makuu ya Chadema?
Kaaya: Sehemu iliyorekodiwa sina ushahidi nayo.
Lissu: Je huo mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025 ulikuwa live Kwenye Jambo Tv, YouTube na channels zingine?
Kaaya: Sikupeleleza kuhusu hiyo mitandao mingine?
Lissu: Umeieleza mahakama hii tarehe 9 Oktoba na leo pia umesema huwa mnafanya doria mtandaoni masaa 24 sasa waeleze majaji nani alikuwa doria siku ya tarehe 3 Aprili 2025
Kaaya: Kuwa zamu unaweza kuwa una concentrate kwenye mtandao wowote sio lazima youtube. Kwahiyo wa tarehe 3 Aprili hakutoa taarifa.
Lissu: Huyo aliyetakiwa kuona na hakuona ni nani?
Kaaya: Hadi nipitie taarifa ya aliyekuwa zamu siku ile ni nani?
Lissu: kwahiyo humjui?
Kaaya: Sina kumbukumbu.
Lissu: Sasa turudi tena kwenye historia yako ya utendaji kazi wa jeshi la Polisi.
Ulisema umepandishwa cheo kuwa full Inspector mwezi juni mwaka huu kwasababu ya utendaji kazi mzuri?
Kaaya: Ndio.
Lissu: Ni sahihi huu ni mwaka wa 19 uko kazini?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Na katika hii miaka 19 umepanda cheo kwa kuwa police constable kuwa Inspector ni hicho tu?
Kaaya: Sahihi.
Lissu: Waeleze majaji sasa utaratibu wa kupanda vyeo kwamba ukiajiriwa kama Police Constable cheo kinachofuata ni Corporal?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Kutoka Constable kwenda Corporal inatakiwa utumie miaka 6 tu?
Kaaya: Mpaka nijikumbumbushe.
Lissu: Nitakukumbusha. Majaji naomba nimsomee shahidi PGO 53(11) Inasema rank promotion. Constable before promoted to Corporal shall have 6 years of service. Ni kweli au sio kweli?
Kaaya: Samahani majaji naomba aniambie ni ya mwaka gani?
Lissu: Mwaka 2021.
Kaaya: Lakini jaji zipo pia kanuni za utumishi wa umma.
Lissu: Mimi mambo ya utumishi wa umma siyajui. Nazungumzia mapolisi na PGO hapa.
Lissu: Sasa kuwa Corporal kuwa Sergent inatakiwa kuwa na miaka mitatu hapo. Unafahamu hilo?
Kaaya: Hebu nipe nisome mwenyewe unaweza kuwa unanidanganya
Lissu: Kwahiyo ni miaka mingapi?
Kaaya: Mitatu.
Lissu: Kutoka Sergent kinachofuata ni cheo gani? PGO 53(11) hapohapo.
Kaaya: Staff Sergent.
Lissu: Hadi hapo ni miaka mingapi jumla.
Kaaya: 12 hapo.
Lissu: Cheo cha Special Sergent kipo hapo?
Kaaya: Hicho cheo hakipo.
Lissu: Umesema wewe ni Inspector
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Ili upande vyeo na kupata cheo cha Inspector PGO inasema angalau uwe na angalau miaka miwili ya Staff Sergent.
Kaaya: Ni kweli ila naomba nitoe ufafanuzi
Lissu: Ufafanuzi siutaki kaa nao.
Lissu: Waeleze majaji kama umewahi kuwa Staff segernt ?
Kaaya: Sijawahi kuwa Staff Sergent.
Lissu: Je kuwa Corporal umewahi?
Kaaya: Sijawahi.
Lissu: Ila umekuwa na cheo cha special sergent.
Kaaya: Nimekuwa sergent.
Lissu: Mwaka gani?
Kaaya: 2021.
Lissu: Tuendelee na utendaji wako wa kazi. Kati ya Sergent 2021 na kuwa assistant Inspector imekuchukua miaka mingapi?
Kaaya: Ilinichukua miezi nane tu.
Lissu: Je haya mambo ya vyeo ulisema kwenye maelezo yako ya polisi?
Kaaya: Sikusema.
Lissu: Kwahiyo ni sahihi kwamba imekuchukua miaka 15 hadi ukawa sergent?
Kaaya: Sahihi.
Lissu: Kwa utararatibu wa PGO ilitakiwa utumie miaka 9?
Kaaya: Ukiwa na mashitaka hupandi cheo.
Lissu: Sasa tuambie wewe ulikuwa na mashitaka gani?
Kaaya: Mimi sikuwa na mashitaka.
Lissu: Kwanini hukupanda cheo wewe? Maana umetumia miaka 15 kupanda cheo na sio 9 kwa mujibu wa PGO?
Kaaya: Sio mimi tu.
Lissu: nataka wewe hao wengine tutajua.
Kaaya: Mimi sijajua anayepandisha cheo sio mimi.
Lissu: Mimi sikusema lolote kuhusu utendaji kazi wako mzuri. Umepandishwa cheo umesema ni utendaji mzuri hujapandishwa unasema anajua muajiri kwanini?
Kaaya: Sielewi kwakweli.
Lissu: Naomba nimsomeee Apendix A PGO 53. Vigezo vya kupandishwa vyeo ni seniority, utendaji yaani sifa, na possession on educational qualification yaani kisomo na utaaluma.unakubaliana na hii?
Kaaya: Hiyo ni general rule.
Lissu: Additional Qualification to be considered ni good conduct, education, professional knowledge, good manner, sobriety yaani usiwe mlevi. Na hii unaisemeaje?
Kaaya: Hiyo nayo ni general rule.
Lissu: Hukupandishwa cheo kwa miaka 15 kwasababu hufai?
Kaaya: Sio kweli.
Lissu: Ulisema una shahada ya chuo kikuu ya sheria na umepata advanced diploma ya air condition hukupandishwa cheo?
Kaaya: Inategemea nilipata lini hivyo visomo.
Lissu: Sasa nikurudishe kwenye maelezo yako. Waheshimiwa majaji apewe D1 shahidi (kielelezo cha maelezo yake aliyotoa polisi ).
Lissu: Ushahidi wa Tarehe 9 Oktoba ukiwa hapa mahakamani ulibaini kuwa ile video ina viashiria vya jinai?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Kwahiyo kwenye hili maneno yako ya kizimbani na polisi yanalingana?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Sasa swali langu umesema wewe ni mwanasheria waeleze majaji matamashi yenye viashiria vya jinai ni kosa gani kwenye sheria za Tanzania.
Kaaya: Hakuna nililosema kwamba hilo ni kosa.
Lissu: Nakuuliza viashiria vya jinai ni kosa gani kwa mujibu wa sheria za Tanzania?
Kaaya: Sijasema kama kulikuwa na kosa.
Lissu: Kwahiyo ni kosa gani?
Kaaya: Hadi nivi identify ni viashiria gani?
Lissu: Kama wewe ni Laweyer unawezaje kusema kitu kikachunguzwe kama hujaona kama ni kosa?
Kaaya: Mimi sikuainisha makosa. Baada ya upelelezi ndio ingejulikana.
Lissu: Je kwenye patrol yako ulisema unaperuzi ili kung’amua makosa ya jinai?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Sasa tuambie uling’amua makosa gani?
Kaaya: Niliona kuna false information. Nikaona niwambie hii taarifa ya kweli au sio kweli.
Lissu: Kwahiyo wewe uling’amua kosa?
Kaaya: Ndio taarifa za uongo.
Lissu: Je kwenye maelezo yako yote ulisema wapi kuna kosa la uhaini?
Kaaya: Kwenye maelezo yangu sijaandika kosa la uhaini.
Lissu: Je kwenye maelezo yako yote umeeleza kwamba kuna kosa la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni?
Kaaya: Sijaandika kosa lolote na hilo halipo.
Lissu: Kwa vile wewe umedai ni Mwanasheria ni sawa au sio sawa kusema unafahamu kifungu cha sheria nilichoshitakiwa nacho yaani kifungu cha 39(2)(d) ya Penal Code(kanuni ya adhabu?
Kaaya: Nafahamu.
Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu kwamba mtu anayesambaza maneno ya kihaini sio yule alaiyeanzisha. Na yeye anakuwa amefanya kosa la uhaini? Waeleze majaji kama unafahamu.
Kaaya: Inategemea.
Lissu: Inategemea nini?
Kaaya: Inategemea na upelelezi. Sheria inategemea na upelelezi.
Lissu: Kuna watu wamesambaza hayo maneno ikiwemo Jambo TV instagram na YouTube?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Ilipelekwa Arusha one Digital?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Ilipelekwa clouds media instagram?
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Ilipelekwa Mwanzo TV youtube?
Kaaya: Ni kweli nakumbuka.
Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu au hufahamu kama ninakabiliwa na kesi mahakama ya kisutu ya kusambaza taarifa za uongo?
Kaaya: Nafahamu.
Lissu: Waeleleze majaji kama kwenye hiyo kesi ya Kisutu umeandika maelezo ya shahidi na waeleze kama ni kweli au si kweli ulikwisha kutoa ushahidi tarehe 16 juni 2025.
Anasimama wakili wa serikali Job Mrema – Mheshimiwa Jaji hili jambo lilishakatazwa tunakoelekea muda huu.
Lissu: Waheshimiwa majaji katika kesi ya jinai ya kuuliza maswali ya mambo ambayo ni irrelevant. Upande wa utetezi kwenye utetezi wanaruhusiwa kuuliza maswali hayo. Mimi sina hicho kizuizi. Wasome kifungu cha s. 156 cha Evidence Act. Kwamba nini kiulizwe kwenye examination in Chief na kwenye cross Examination.
Pia swali langu la Kisutu ni kuonesha this witness is lying. Kuna mambo amesema Kisutu hapa hajasema anajifanya amesahau. Hili pingamizi halina msingi wowote.
Job Mrema: Kifungu cha 156 cha Evidence Act kwasababu tayari tuko estopped.
Wakili mwingine wa serikali anasimama Ajuaye Zengeli. Sisi tulikatazwa lakini pia na yeye akatazwe.
Majaji wanatafakari na kujadili kwa dakika kadhaa hapa.
Jaji Ndunguru: Nashauri tusiende Kisutu lakini ukiona ni muhimu we uliza tu.
Lissu: Je hiyo video ya Tarehe 3 ilichapishwa Arusha one, Mwanzo, The Chanzo.
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Pia yalichapishwa instagram Clouds?
Kaaya: Nakumbuka.
Lissu: Kutokana na hayo unayokumbuka hawa Clouds kwenye instagram, Jambo TV YouTube na Instagram hawa walioshiriki kwa mujibu wa sheria ya uhaini wamefanya kosa la uhaini?
Kaaya: Inategemea na upelelezi
Lissu: Je watu wanaosambaza maneno ya ugaidi na kuyasambaza kwa watu wengine na wao wanakuwa wameshiriki tendo la ugaidi.
Kaaya: Sikufanya huo upelelezi kwahiyo ya ugaidi sifahamu.
Lissu: Je unafahamu kuna kosa la kula njama kwenye uhaini?
Kaaya: Najua lipo kosa la kula njama.
Lissu: Je mimi mshitakiwa ndie niliyewaalika hao waaandishi wa habari waje kwenye mkutano?
Kaaya: Mimi sikupeleleza.
Lissu: Unamfahamu SSP George Bagyemu?
Kaaya: Ndio namfahamu.
Lissu: Yeye alisema mimi ndio niliwaalika, Wewe unasemaje?
Kaaya: Mimi sijui sikushirikishwa kabisa.
Lissu: Hati ya mashitaka inayonikabili inasema kwamba nilitamka hayo maneno na kuyachapisha kwenye mitandao ya kijamii. Wewe unasemaje?
Kaaya: Ninapotoa taarifa kwa umma kwa kualika waandishi maana yake nimeridhia.
Lissu: Sikiliza swali ndio ujibu. Tuhuma inasema nilizungumza na kuchapisha. Wewe unasemaje?
Kaaya: Unapowaalika waandishi maana yake umesambaza.
Lissu: Je mimi ni mmiliki wa Jambo Tv?
Kaaya: Simfahamu.
Lissu: Je mimi ni Mkurugenzi?
Kaaya: Mkurugenzi simfahamu.
Lissu: Je mimi ni mwandishi?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Je mimi ni mfanyakazi wa Jambo TV?
Kaaya: Hilo nalo sifahamu.
Lissu: Je nilikuwa na mamlaka au uwezo wowote kuja kwenye mkutano wa tarehe 03 Aprili 2025?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Je mimi siku hiyo mimi ndie nilishikilia video camera na kuanza kurusha video mubashara.
Kaaya: Aliyeshika camera hakuonekana.
Lissu: Ila aliyekuwa anaongea alionekana na yeye ameshika makamera?
Kaaya: Hapana.
Lissu: Mtu anayeita mkutano wa wanahabari anakuwa na mamlaka ya kuwaelekeza namna ya kuripoti habari husika?
Kaaya: Inategemea, sifahamu mambo ambavyo huwa yanaenda.
Lissu: Je hao waliorusha wa clouds na Jambo tv sasa waeleze kama kuna hata mmoja ameshitakiwa na mimi?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Kwahiyo unawafahamu mshitakiwa mwingine?
Kaaya: Namjua mmoja tu.
Lissu: Kwanini nimeshitakiwa peke yangu?
Kaaya: Sijui upelelezi umefikia wapi na mpelelezi wa Kesi yupo.
Lissu: Je unafahamu ule mkutano ulikuwa ni mkutano kati ya mwenyekiti wa chama na watia nia wa ubunge Chadema?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Sasa hayo maneno yalisemwa mbele ya watu wote hao watia nia na viongozi wengine.
Kaaya: Sijui kama walisikia wote
Lissu: Unafahamu kuna kosa linaitwa mispresion of treason yaani kupata taarifa za kigaidi na usizitoe polisi ni kosa la uhaini adhabu yake ni kifo?
Kaaya: Sijui kabisa.
Lissu: Sasa hao wote niliowataja wameshitakiwa kwa mispresion of treason? Au shida yenu ilikuwa ni Mwenyekiti tu awepo jela ili asimsumbue Mama. Nani aliyeshitakiwa mwingine sema?
Kaaya: Hakuna aliyeshitakiwa.
Lissu: Nataka tuzungumzie maelezo yako uliyotoa Polisi. Waeleze majaji nani aliyeandika maelezo haya? Exhibit D1.
Kaaya: Ni mimi binafsi.
Lissu: Nani alikuapisha au kukukanya kwamba ukisema uongo ni kosa?
Kaaya: Hakuna aliyenikanya.
Lissu: Nani aliyethibitisha kwamba hayo maneno ni kweli?
Kaaya: Ni mimi mwenyewe.
Lissu: Nani alikuwa shahidi yako, aliyekushuhudia ukifanya hayo.
Kaaya: Hakuna.
Lissu: Ni kweli au sio kweli kifungu cha 11(4) cha CPA kinasema maelezo hayo ya shahidi yanatakiwa yaandikwe na Polisi mwingine?
Kaaya: Naomba unisomee kwanza kifungu.
Lissu: Anasomewa .
Kaaya: Hakuna kifungu kinachomkataza police officer kujikanya na kujiandikia.
Lissu: Mimi niliambiwa mahakama sio mama yangu sasa na mimi nawauliza nyie mapolisi hizi sheria ni mama yenu, nyie mnadhani sisi raia ndio tunapaswa kutii sheria bila shurti?
Kaaya: Sio mama yetu ndio.
Lissu: PGO No. 236 inasema any police officer is authorised to record statement from any person who he believe has knowledge on the matter. Kumbe mnapaswa kuandika maelezo ya mtu yeyote. Tuko pamoja hapo?
Kaaya: Ni sahihi kabisa.
Lissu: Ukiendelea kusoma hapo inasema kwamba Jambo hilo limeelezwa kwenye sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai na inaeleza signature of the recording officer must be there, the recording officer will comment on the witness reliability, kama ni mkweli au vipi? Sasa unasemaje kuhusu yote haya.
Kaaya: Hapo haijazungumza
Lissu: Utajijazia nini kwenye sehemu ya comment ya kusema police atoe comment kuhusu alichosema shahidi ni uongo au sio uongo.
Kaaya: Mimi sidhani kama polisi anaweza kusema uongo.
Lissu: Nyie mapolisi wa Tanzania ndio msiseme uongo?
Lissu: wewe ni aina ya afisa wa polisi wa aina gani usiyefahamu mambo yote niliyokuuliza kuhusu yapo kwenye PGO, Ndio maanaa hupandi vyeo we Polisi kwa miaka 15?
Jaji: Mshitakiwa taratibu tusifike huko.
Lissu: Naendelea sasa nataka tusome kwenye introduction ya PGO pale mwanzo kabisa. PGO inasema mnatakiwa kuwa na weledi katika kazi ili kufanya majukumu yenu.
Sasa wewe kila saa unasema sijui , sifahamu , sio kweli utapanda vyeo kama majibu yako ndio haya hujui , hujui kila saa?
Kaaya: Sio kweli.
Lissu: Katika maelezo yako ulisema miongoni mwa matamshi hayo ni pamoja na hao ambao huwezi kuwajua polisi wanakuja na vibegi vya kura feki. Je hayo maneno anakuwa amefanya kosa la uhaini?
Kaaya: Inategemea
Lissu: Inategemea nini?
Kaaya: Kimya
Lissu: huna jibu haya tuendeleee.
Lissu: Matamshi mengine ulisema ameandika kuwa majaji nao ni watu wa Rais wanataka kuteuliwa vyeo kwahiyo mahakamani hakuendeki. Je mtu akisema maneno hayo ni uhaini.
Kaaya: Inategemea
Lissu: Inategemea na mapolisi mtakaobambikia watu kesi.?
Kaaya: kimya
Lissu: Tuendelee maneno mengine ulisema nimesema mimi eti ” Rais alisema hakikisheni wapinzani hawaendi kokote” je yana shida gani?
Kaaya: Sidhani maelezo hayo kama yapo kwenye shitaka. Maelezo yangu hakuna niliposema hapa na hapa ni uhaini.
Lissu: Ni sawa wewe hujasema kabisa mimi ni mhaini. Shahidi Na. 2 nakuelewa vizuri. Sasa tuendelee unasema pia nilisema na mimi nataka nichaguliwe kwenye kacheo fulani. Je kusema hivyo ni kosa la uhaini?
Kaaya: Sijaidentify kama ni kosa la uhaini.
Lissu: Pia unasema nilisema mkutano wetu unasema ‘NO reforms no election’ na tutahamasisha uasi ili kuzuia uchaguzi ni uhaini?
Kaaya: Ni kosa.
Lissu: Mtu anayetaka kuzuia uchaguzi kwa maandamano au migomo au njia nyingine yoyote isipokuwa kumuua Rais. Je ni kosa gani?
Kaaya: Tuzungumzie maelezo yote kwa pamoja.
Lissu: Kuzuia uchaguzi ni kosa, ngoja nikutaftie sheria hapa unadhani kuwa mwanasheria ni miezi 6 kama ya CCP Moshi kile Chuo cha Polisi. Sheria sio rahisi hivyo,Sasa nimepata sheria ya wabunge na madiwani isome sheria hiyo.
Jaji Ndunguru: Mshitakiwa kesho ni sikukuu na imeshafika saa 11 na jioni kwahiyo naomba tuishie hapo.
Lissu: Kesho ni Sikukuu gani mimi sifahamu niko jela.
Jaji: Nyerere Day na tunaahirisha hadi tarehe 15/10/2025 kesho kutwa, naomba tukutane saa tatu asubuhi.
Lissu: Shahidi nakusubiri sana kesho kutwa hiyo.
ZINAZOFANANA
Nitarejeshea wananchi mali zao zilizoporwa Othman Masoud
John Heche ateta na Marando
Mgombea udiwani Kinyerezi ajinadi kuwa mtu wa vitendo zaidi