October 13, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Nitarejeshea wananchi mali zao zilizoporwa Othman Masoud

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman

 

MGOMBEA urais wa Zanzibar, kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuwarejeshea wananchi wote mali zao, walizodhulumiwa na serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar …( endelea).

“Mkinipa ridhaa ya kuwaongoza, nitahakikisha wananchi wote waliodhulumiwa mali zao na haki zao nyingine, ikiwamo ardhi, wanarejeshewa,” ameeleza Othumani.

Ametoa kauli hiyo, wakati akizungumza na wauza madagaa katika eneo la Fungu Refu, mkoa wa Kaskazini Unguja, leo Jumapili, kabla ya kuelekea Tumbatu, alikotarajiwa kuhutubia mkutano wa hadhara.

Kwa mujibu wa Othman, ambaye pia ni Makamo wa Kwanza wa Rais, katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUKI), changamoto kubwa inayowakabili wananchi, ni kunyimwa haki zao kutokana na mifumo dhaifu ya utawala na upendeleo unaojitokeza katika taasisi za umma.

Amesema, “Serikali ya ACT Wazalendo haitakuwa ya maneno matupu. Tutasimamia haki za wananchi wote, na kila aliyeonewa atarejeshewa stahiki zake kwa mujibu wa sheria.”

Mgombea huyo alitumia fursa hiyo kusikiliza kero na changamoto za wafanyabiashara hao wadogo, ikiwamo ukosefu wa masoko, miundombinu duni na vikwazo katika utoaji wa leseni, akiahidi kuweka mazingira bora zaidi ya biashara visiwani humo.

Alisema serikali anayoitarajia kuunda itatoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo ili waweze kuchangia ipasavyo katika kukuza uchumi wa Zanzibar.

“Wafanyabiashara wadogo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Tukiwapa nguvu na haki, tutakuwa tumewainua wananchi wote,” aliongeza.

Kinyang’anyiro cha urais Visiwani kinazidi kupamba moto, ambako wagombea wawili wenye nguvu, Othman Masoud Othman na Dk. Hussein Mwinyi, anayeteta nafasi yake, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanachuana jasho, kuwania nafasi hiyo.

Uchaguzi mkuu wa Zanzibar, umepangwa kufanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu.

About The Author

error: Content is protected !!