October 3, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Masawe ateuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa TPSF

Deogratius Massawe

 

DEOGRATIUS Massawe ameteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Sekta binafsi nchini – The Tanzania Private Sector Federation (TPSF). Anaripoti Mwandishi Wetu, dar es Salaam … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na Rais wa Sekta binafsi Tanzania, Angelina Ngalula, imeeleza kuwa Massawe anakaimu nafasi hiyo kuanzia leo tarehe 3 Oktoba 2025.

Kabla ya Masawe kukabidhiwa mikoba hiyo, nafasi hiyo, ilikuwa inashikiliwa na Raphel Maganga, ambaye uteuzi wake umesitishwa.

Hakuna sababu zilizoeleza kuwapo kwa mabadiliko hayo.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikipambana kuendelea kuweka mazingira bora ya biashara na kuvutia uwekezaji nchini, hususani katika kukuza mazingira thabiti yanayowezesha maendeleo ya taifa.

Massawe ni mchumi, mtaalamu wa fedha na sera akiwa na Shahada ya Uzamili ya Biashara katika Uhasibu, Shahada ya Kwanza ya Forodha na Usimamizi wa Kodi, Diploma ya Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (IPSAS).

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo, ni Mhasibu wa Umma aliyesajiliwa (CPA) na mkufunzi wa fedha aliyeidhinishwa (CFE).

Taarifa hiyo inasema, anachukua nafasi hiyo akiwa na uzoefu katika sekta ya ushauri kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi.

“Massawe aliwahi kuhudumu kama mkuu wa Idara ya fedha sekta binafsi.

Anakuja na hazina kubwa ya uzoefu katika uongozi wa kifedha, upangaji mkakati na maendeleo ya taasisi uwezo muhimu katika kuendelea kuimarisha nafasi ya sekta binafsi, kama sauti ya sekta binafsi nchini,” imeeleza taarifa ya Ngalula.

Sekta binafsi ina jukumu muhimu katika kuchangia ongezeko la ajira, uvumbuzi, pato la taifa na ukuaji wa uchumi nchini.

About The Author

error: Content is protected !!