November 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Bilioni 366 kupeleka umeme kwenye vitongoji 3,060

 

JUMLA ya Sh 366 bilioni zinatarajiwa kutumika kutekeleza mpango wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 3,060 vilivyopo katika majimbo 15 katika awamu kwa kwanza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hayo yamebainishwa leo tarehe 20 Agosti 2024 jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa miradi huo unaolenga kufikisha umeme kwa Watanzania wote.

Pia Dk. Biteko amewaonya wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya Kimkakati ya Nishati hususan miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufanya kazi kwa uadilifu na kukamilisha kwa wakati na REA kuwasimamia wakandarasi kwa kutenda haki.

“Zipo taarifa za wakandarasi wanawaomba fedha wananchi wanapopeleka umeme vijijini ilhali Serikali imekwisha walipa, nawaomba REA na wakandarasi, nikiletewa taarifa yoyote nitachukua hatua, tendeni haki kwa wote, ” amesema Dk. Biteko.

Aidha, amesema Serikali imedhamiria kufikisha umeme katika vitongoji vyote chini ili kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme pamoja na uunganishwaji katika maeneo ya vijijini.

Amesema takribani miaka 17 hadi sasa, Serikali imekuwa ikishirikiana na washirika wa maendeleo katika utekelezaji miradi mbalimbali ya kimkakati ya nishati bora vijijini.

“Mikataba hii tuliyoishudia leo yenye jumla ya Shilingi 362,825,108,211.45 imewezeshwa kupitia ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya Dunia. Hivyo, kwa niaba ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, naomba niwashukuru washirika wa maendeleo wanaochangia katika mfuko wetu wa Nishati Vijijini hususan Benki ya Dunia, Serikali za Norway na Sweden, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD),” amesema Dk. Biteko.

Amesema wananchi wanaotarajia kunufaika na mradi huu wanayo matarajio makubwa kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme utaboresha na kuinua hali zao za maisha kupitia ushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Niwahakikishie wananchi wote kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha, na kushirikiana na wabia wa maendeleo kuhakikisha kuwa umeme unawafikia Watanzania wote, popote walipo, ” ameongeza Dk. Biteko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo David ameipongeza Serikali kwa hatua ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 3,060 jambo ambalo linakwenda kutekelezwa sasa na REA.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said amesema matarajio yaliyopo sasa ifikapo mwezi Septemba 2024 ni kuhakikisha wanafikisha umeme katika kila sehemu hapa nchini.

About The Author