September 29, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Hali ya Gaza yazidi kuwa tete, Hamas haina mawasilisno na mateka

 

KIKOSI cha kijeshi cha Hamas, Al-Qassam Brigedi, kimesema kuwa kimepoteza mawasiliano na Matan Angrest na Omri Miran, mateka wawili wa Israel, wanaoshikiliwa na kundi hilo, kufuata operesheni kali za zinaoendelea katika vitongoji viwili vya Gaza City. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Al-Qassam Brigedi, kimeitaka Israel kuwarudisha nyuma wanajeshi wake na kusitisha mashambulizi ya anga katika mji wa Gaza kwa saa 24, ili kuwaondoa mateka hao katika hatari.

Vifaru vya Israel vinaendelea kusonga mbele zaidi katika mji wa Gaza, jambo linaloashiria kuwa uwezekano wa kuwaokoa mateka hao wakiwa hai, unazidi kutoweka.

Haya yanajiri wakati Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akitarajiwa kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump, katika Ikulu ya White House, leo Jumatatu kujadili kinachoitwa, “mpango wa amani wa Gaza.”

Mpango huo uliyozinduliwa kwenye mkutano kati ya Trump na viongozi wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), wiki iliyopita, unalenga kumaliza vita kwenye ardhi ya Palestina, ndani ya siku 21.

Kwa mujibu wa Trump bado kuna “nafasi ya kweli ya ukuu katika Mashariki ya Kati,” akisisitiza kuwa makubaliano ya kumaliza vita vya Gaza yanaweza kufikiwa.

Wizara ya afya ya Gaza inaeleza kuwa idadi ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel kwenye ukanda huo imepindukia 66,000, huku wengine 168,162 wakijeruhiwa, tangu 7 Oktoba 2023.

Miongoni mwa waliofariki dunia, ni pamoja na watu 79 waliopelekwa hospitalini katika saa 24 zilizopita.

Hatima ya mateka hao wawili, waliosababisha hisia kali ndani ya Israel, inaweza kuwa na athari mbaya kwenye mkutano kati ya Netanyahu na Trump.

Trump ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kuwa amepokea “jibu la kutia moyo” kutoka kwa Israel na viongozi wa Kiarabu, kuhusu pendekezo la mpango wa amani wa Gaza na kwamba “kila mtu anataka makubaliano yafikiwe.”

Hata hivyo, Hamas imesema, bado haijapokea pendekezo lolote kutoka kwa Trump wala kutoka kwa wapatanishi.

Israel imefanya shambulio kubwa la ardhini katika mji wa Gaza, na kusambaratisha wilaya nzima huku ikiamuru mamia kwa maelfu ya Wapalestina kukimbilia katika kambi zilizo na mahema, katika kile Netanyahu anasema ni kutaka kuangamiza Hamas.

Wakati hayo yakijiri, maelfu ya Waisraeli wameandamana mjini Tel Aviv kushinikiza kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita hivyo, siku mbili kabla ya Netanyahu na Trump kukutana mjini Washington.

Waandamanaji walipokusanyika katika uwanja wa Hostage {Mateka}, waliinua bendera kubwa iliyosomeka, “Mateka wote, warudisheni nyumbani sasa.”

“Kitu pekee ambacho kinaweza kutuzuia kuteleza kwenye shimo ni makubaliano kamili na ya kina ambayo yanamaliza vita na kuwarudisha mateka wote na wanajeshi makwao,” alisema Lishay Miran Lavi, mke wa Omri.

About The Author

error: Content is protected !!