September 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Rostam ni mfano bora wawekezaji ndani na nje ya nchi-TCCIA

 

CHEMBA ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) imetoa wito kwa Serikali kuweka sera madhubuti zitakazowezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati ya Uchumi, huku ikimtaja Rostam Aziz kama mfano bora wa Mwekezaji mzawa aliyefanikiwa ndani na nje ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Rais wa TCCIA, Paul Minja, amesema ipo haja ya kuwa na mifumo ya kisheria na sera zitakazowapa kipaumbele wazawa, akisisitiza kuwa Watanzania wana uwezo wa kuwekeza na kuendesha shughuli kubwa za kiuchumi endapo watawezeshwa.

Ameyataja baadhi ya maeneo ambayo Rostam Aziz amewekeza, yakiwemo Kampuni ya Gesi ya Taifa Gas inayofanya kazi pia katika nchi za Kenya, Uganda, Zambia na Malawi, ununuzi wa hisa katika Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL), TANCOAL pamoja na Mgodi wa almasi wa Petra.

Minja ameeleza kuwa hatua hizo za uwekezaji si tu zinachochea uchumi, bali pia zinaweka msingi wa ushiriki wa wazawa katika sekta nyeti, na ni kielelezo cha kizalendo katika biashara.

Ameongeza kuwa licha ya uwepo wa sheria kama Sheria ya Ushiriki wa Watanzania (Local Content Act), Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni za Madini za mwaka 2018, bado utekelezaji wake unahitaji kuimarishwa ili kuhakikisha Watanzania hawabaki watazamaji katika shughuli za kiuchumi.

Aidha ameiomba Serikali kufuata mfano wa nchi kama Afrika Kusini, ambayo ilianzisha Sera ya Uwezeshaji wa Weusi Kiuchumi (Black Economic Empowerment), na Urusi, iliyoanzisha usimamizi mpya wa rasilimali baada ya enzi ya Usovieti, kama mifano ya Kimataifa ya kuimarisha ushiriki wa Wananchi katika uchumi.

About The Author

error: Content is protected !!