
WANANCHI wa Fumba Wilaya ya Magharibi B Unguja wameeleza kwa uchungu na masikitiko makubwa juu ya kuendelea kuporwa ardhi zao kutokana na uwekezaji mkubwa wa utalii unaoendelea katika maeneo yao. Wamesema badala ya uwekezaji huo kuwanufaisha, umegeuka kuwa janga na maafa kwao na familia zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Katika ziara ya kampeni iliyoongozwa na Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, wananchi walimueleza kuwa maeneo yaliyokuwa yakitumika kwa kilimo na shughuli mbalimbali za kijamii yamegeuzwa makazi na maeneo ya kibiashara ya wawekezaji.
Hali hiyo imewafanya wananchi kukosa sehemu ya kulima na kujipatia kipato.
Wananchi walisema kilichouma zaidi ni kwamba hata nafasi za ajira zinazotokana na uwekezaji huo hazijawanufaisha, kwani zimekuwa zikitolewa kwa wageni wasio wakaazi wa Fumba na Bweleo, huku vijana wa eneo hilo wakibaki bila kazi na kuwa mzigo kwa familia zao.
Mama Halima Mzee, mmoja wa wananchi wa Fumba, alisema alinyang’anywa eneo kubwa la ardhi alilorithi kutoka kwa bibi zake na ambalo alilitumia kwa kilimo. Alisema sasa ameachwa bila msaada huku akishuhudia nguvu za wenye uwezo kuhodhi kila kitu.
Wananchi walieleza kwa masikitiko makubwa kuwa maeneo muhimu ya ukanda wa bahari yameporwa na kupewa wawekezaji, jambo linalohatarisha maisha yao, urithi wao na hadhi ya jamii ya eneo hilo.
Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud, alisema hataridhishwa na hali hii ambayo imekuwa kilio cha mara kwa mara kila anakofanya ziara.
Alisema Wazanzibari walipaswa kuwa watu wa kwanza kunufaika na rasilimali ya ardhi na si wageni.
Othman alibainisha kuwa Serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha kila mwananchi anapewa thamani kwanza kuliko wawekezaji.
Alisisitiza kwamba si kila eneo lipaswe kupewa wawekezaji, bali wananchi wanapaswa kupewa kipaumbele na kulindwa dhidi ya unyanyasaji unaotokana na kuporwa kwa ardhi zao.
ZINAZOFANANA
Rostam ni mfano bora wawekezaji ndani na nje ya nchi-TCCIA
ACT tutavunja Tume ya Uchaguzi, tutaunda upya Jeshi la Polisi
Kesi ya Lissu kuanza kutolewa ushahidi Oktoba 6, Samia atajwa