September 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yaitambulisha Kampeni ya NBC Shambani kwa wakulima wa korosho, mbaazi, ufuta Tunduru

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), imetambulisha rasmi kampeni yake ya ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ kwa wakulima wa mazao ya korosho, mbaazi na ufuta wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kupitia uchumi jumuishi unaochagizwa na huduma rasmi za kifedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tunduru … (endelea).

Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo ilifanyika mapema jana wilayani Tunduru ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Denis Masanja huku pia ikihusisha uwepo wa wadau mbalimbali wa sekta za kilimo wilayani humo wakiwemo viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika vya wakulima. Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa aliwaongoza maofisa wengine wa benki hiyo kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, DC Masanja pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa jitihada zake endelevu zinazolenga kuwasaidia wakulima katika maeneo mbalimbali hapa nchini, alisema ujio wa kampeni hiyo wilayani Tunduru utasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo hususani kupitia huduma mbalimbali za kibenki zilizobuniwa mahususi kwa kundi hilo muhimu kiuchumi ikiwemo utoaji wa elimu ya kifedha, huduma za bima na utoaji wa mikopo ya fedha na zana za kilimo kwa wakulima.

“Ubora zaidi wa kampeni hii unaonekana pale inapohusisha utoaji wa elimu ya nidhamu ya fedha miongoni mwa wakulima mmoja mmoja na vyama vya ushirika hatua ambayo itawajengea uwezo wa kuona umuhimu wa kujiwekea akiba, umuhimu wa kutumia bima mbalimbali ikiwemo bima ya afya, bima za kilimo pamoja na kuwekeza kwenye zana za kisasa za kilimo.’’

“Hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha wakulima wetu kugeukia huduma rasmi za kifedha na hivyo kuchochea uchumi jumuishi.’’ aliongeza.

Katika hatua nyingine DC Masanja alitoa ombi kwa uongozi wa benki ya NBC kuangalia uwezekano wa kufungua tawi rasmi wilayani Tunduru ili iweze kusogeza kwa ukaribu zaidi huduma zake kutokana na huduma za benki hiyo kuonekana zinaendana kwa kiasi kikubwa na mahitaji stahiki ya wakazi wa wilaya hiyo wanaojishughulisha zaidi na kilimo cha korosho, mbaazi na ufuta pamoja shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu na vito.

“Kwasasa mzunguko wa fedha wilayani Tunduru ni mkubwa sana kutokana na shughuli za wakazi wake ambao kwa mwaka wanapitia vipindi vitatu vya mauzo ya mazao yao yaani msimu wa mauzo ya korosho, msimu wa mauzo ya ufuta na msimu wa mauzo ya mbaazi.Misimu yote hii mitatu inahusisha mzunguko wa fedha unaohitaji benki iliyo karibu zaidi na wakulima kama ilivyo NBC. Hivyo, tunauomba sana uongozi wa NBC ufikirie ombi hili,’’ alisisitiza.

Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo ya miezi mitatu inayotarajiwa kuhitimishwa mwishoni mwa mwaka huu, Urassa alisema walengwa wa kampeni hiyo ni wakulima wa mazao hayo matatu kupitia vyama vya msingi, vyama vikuu vya ushirika na mkulima mmoja mmoja ambao wanahudumiwa na benki hiyo.

Kwa mujibu wa Urassa, ili walengwa hao waweze kujishindia zawadi mbalimbali zilizo ambatana na kampeni hiyo zikiwemo pampu za kupulizia dawa, baiskeli, pikipiki na maguta (pikipiki ya miguu mitatu) wanatakiwa kufungua akaunti ya NBC Shambani kisha kupitishia malipo yao kwenye akaunti hizo.

“Lengo la kampeni hii ni kuwahamasisha wakulima kutunza fedha zao kwenye mifumo rasmi ya kifedha hasa benki badala ya kutunza kwenye mifumo isiyo rasmi. Wakati tunafanyia kazi ombi la DC Masanja la kufungua tawi letu rasmi wilayani Tunduru tunawaomba sana wakulima waendelee kufurahia huduma zetu kwa njia mbadala yaani kupitia mawakala wetu waliopo hapa Tunduru pamoja na huduma yetu kwa njia ya kidigitali ya NBC Kiganjani,’’ alisema.

Wakizungumza kwa niaba ya wakulima wengine, Fadhili Salada na Grace Evarist ambao ni viongozi wa AMCOS zilizopo wilayani humo walionyesha kuguswa zaidi na huduma mbalimbali za upendeleo kwa wakulima zilizohusishwa kwenye akaunti ya NBC Shambani ikiwemo urefu wa uhai wa akaunti hizo pamoja na kutokuwepo kwa makato katika uendeshaji wa akaunti hizo.

About The Author

error: Content is protected !!