September 13, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Ufuatiliaji na tathimini ni nyenzo ya utendaji kazi serikalini

 

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amehitimisha Kongamano la Nne la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza lililofanyika Jijini Mwanza akiweka mkazo kuwa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kuwa kila taasisi inatimiza wajibu wake kwa ufanisi na hivyo kufikisha huduma bora kwa wananchi. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).

Kutokana na hilo, Dk. Biteko amewataka wataalam wa ufuatiliaji na tathmini nchini kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu bila kuogopa kuchukiwa kwani taifa linawategemea ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Hakuna mtu au taasisi inayoweza kufanikisha majukumu yake bila kufanya tathmini, ninyi ndio mnaoweza kutambua changamoto mapema na kuzitafutia suluhisho kabla hazijawa kubwa, taasisi yoyote inayokosa mfumo huu inafanana na timu inayoingia uwanjani bila refa,” amesema Dk. Biteko

Ametoa mfano kuwa katika sekta ya umeme, kabla ya kupeleka huduma hiyo eneo lolote lazima tathmni ifanyike ili kuepuka kurudia kazi mara mbili na pia tathmini husaidia kuona matokeo ya huduma husika kwa wananchi.

Kuhusu Kongamano hilo, Dk. Biteko ameeleza kuwa mwaka jana lilihudhuriwa na washiriki 900 huku mwaka huu likivutia washiriki 1,300.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) kutoka Wizara ya Nishati, Anitha Ishengoma, amesema Wizara imejipanga kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathimini ili kuboresha upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu kwa Watanzania.

About The Author

error: Content is protected !!