September 13, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ATCL yatangaza safara ya Dar-Lagos kwa dola 850

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) @airtanzania_atcl imetangaza rasmi uzinduzi wa Mchongo Na. 29, safari mpya za moja kwa moja kati ya Dar es salaam na Lagos, Nigeria. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na ATCL, imesema safari ya kwanza inatarajiwa kuanza tarehe 19 Septemba 2025, kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kituo hicho cha 29 cha safari ni cha kihistoria, kwani ni safari ya kwanza ya ratiba kufanywa na ATCL kwa Afrika Magharibi, hatua hii inalenga kufungua fursa mpya za kibiashara, usafirishaji na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.

ATCL imeongeza kuwa katika kusherehekea mafanikio haya, imetoa nafasi 100 kwa wadau wake ili kushiriki kwenye safari ya kwanza, ambapo watapaswa kulipa USD 850 na kisha kupatiwa tiketi ya kwenda na kurudi (Dar–Lagos–Dar), huduma ya visa, malazi ya siku mbili, pamoja na kuhudhuria hafla ya kibiashara itakayowakutanisha Wafanyabiashara, Viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia, na Watanzania waishio Nigeria.

Aidha, kwa wale ambao hawatabahatika kuwa miongoni mwa Washiriki 100 ATCL imetoa bei ya punguzo kwa tiketi ambapo tiketi inaanzia USD 399.

Safari za Lagos zitafanyika mara tatu kwa wiki, kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa, na zinatarajiwa kuchukua takriban masaa matano (5) kutoka Dar es salaam.

About The Author

error: Content is protected !!