September 11, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TMA yatangaza utabiri wa mvua za vuli za Oktoba mpaka Desemba

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a

 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema Mvua zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi Chini ya Wastani katika maeneo mengi na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dk. Ladislaus Chang’a wakati wa mkutano na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2025), katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, leo tarehe 11 Septemba 2025.

“Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2025 katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na kusambaa katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2025. Mvua zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2026,” alifafanua Dk. Chang’a.

Dk. Chang’a alitoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ikizingatiwa kuwa mwelekeo wa mvua uliotolewa ni kipindi cha msimu wa miezi mitatu, hivyo viashairia vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadaliko ya muda mfupu utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.

“Mvua za Vuli zinatarajiwa kuongezeka kidogo mwezi Desemba, 2025 na Vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu huu wa Vuli,” aliongeza Dk. Chang’a

Aidha, Dk. Chang’a alisema kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea kutoa taarifa za utabiri wa msimu mahususi kwa ngazi ya Wilaya.Wilaya 86 zilizo katika ukanda unaopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka zitapatiwa utabiri huo wa maeneo madogo.

Msimu wa Mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

About The Author

error: Content is protected !!