August 31, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Monalisa apinga kutimuliwa ACT-Wazalendo, wadau wasema, hilo limeishaaa

Monalisa Ndala

 

MONALISA Joseph Ndala, aliyetangazwa na chama cha ACT- Wazalendo, kufukuzwa ndani ya chama hicho, amepinga kuvuliwa uanachama wake. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumamosi jijini Dar es Salaam, Monalisa alisema, hatua ya kuvuliwa kwake uanachama, haikubariki kwa mujibu wa sheria.

Amesema, yeye amesajiliwa mkoani Dar es Salaam, na kwamba uamuzi uliofanywa na tawi la Mafifi mkoani Iringa, ni kinyume na kanuni na katiba ya chama chake.

Ametoa siku mbili kwa Katibu mkuu wa ACT- Wazalendo, kutoka hadharani na kuikataa barua iliyotolea na uongozi wa tawi la Mafifi. Ametishia kuchukua hatua iwapo hilo halitafanyika.

Kwa mujibu wa Monalisa, bado anaendelea kuamini kuwa chama chake hakikufuata utaratibu katika uteuzi wa mgombea wake urais, Luhaga Mpina, aliyezuiliwa na tume ya uchaguzi na msajili wa vyama vya siasa, kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Mpina (50), ameondolewa kwenye kinyang’anyiro cha urais, baada ya Monalisa anayedaiwa kutumika na wenye kukitakia mabaya chama hicho, kulalamikia uteuzi huo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na Francis Mutungi, Msajili ya Vyama vya Siasa, tarehe 26 Agosti 2025, Mpina ameondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho, kutokana na kupoteza sifa.

Alidai kuwa alijiunga na upinzani tarehe 5 Agosti –   baada ya kutofautiana na kilichokuwa chama chake –   aliidhiniwa kuwa mgombea urais tarehe 6 Agosti 2025, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za chama hicho.

Amesema, “Nimejiridhisha kuwa Kanuni za uchaguzi za ACT-Wazalendo za mwaka 2024, kwamba zinatumika pia katika kuteua wagombea katika uchaguzi wa kiserikali.” Hivyo Mutungi anasema, “Malalamiko ya Monalisa yamekubaliwa.

Akishindilia hoja yake, Jaji Mutungi anasema, “…hakuna ubishi kwamba tarehe ya mwisho ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa udhamini wa ACT-Wazalendo, ilikuwa ni tarehe 25 Mei mwaka huu.”

Ameongeza, “Luhaga Mpina, alipata uwanachama wa ACT-Wazalendo, tarehe 5 Agosti 2025. Hivyo zoezi la uchukuaji fomu, kutokana na ratiba iliyotangazwa ilikamilika kabla ya Mpina hajawa mwanachama wa chama chako.”

Wachambuzi wa mambo wanasema, msimamo uliochukuliwa na uongozi wa ACT-Wazalendo, mkoani Iringa, hata kama haukufuata taratibu, tayari utakuwa umezima mradi wa Monalisa.

“Kwa uamuzi huu, Monalisa hataweza tena kuja makao makuu ya chama, kwa kuwa siyo mwanachama wetu. Hii haitajalisha uamuzi ulikuwa halali au siyo halali. Ataendelea kutumika akiwa nje ya chama,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamzi wa ACT-Wazalendo, ambaye hakupenda kutajwa jina.

Ameongeza, “Hataweza kuhudhuria vikao vya chama. Kwa maneno mengine, biashara yake, hapa itakuwa imefika mwisho. Duka limefungwa kama lilivyofungwa duka la Lebrus Mchome, aliyetumika kukishitaki Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa msajili.”

About The Author

error: Content is protected !!