September 20, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

PBZ yaongeza faida kwa asilimia 18 katika nusu ya kwanza 2024

 

BENKI ya Watu wa Zanzibar (PBZ Bank) imetangaza ripoti yake ya kifedha ya nusu ya kwanza ya mwaka 2024, inayoonesha mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo ongezeko la faida ya jumla (net income) baada ya kodi kwa asilimia 18. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Ikiashiria maendeleo mazuri ya benki hiyo, ripoti hiyo imeonyesha ongezeko la mapato hadi kufikia kiasi cha TZS bilioni 31.15 (ikiwa ni faida kabla ya kodi TZS bilioni 44.50). Kiasi hiki kinawakilisha ongezeko la asilimia 18 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, ikithibitisha uwezo wa benki hiyo katika kuendesha ukuaji endelevu na faida.

Mafanikio hayo yamechagizwa na ongezeko la Mapato yatokayo na riba (Net Interest Income) ya benki hiyo ambayo yamefikia TZS bilioni 54.15, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14 ikilinganishwa na mwezi Juni mwaka 2023. Mafanikio haya yanatajwa kama ushahidi wa utekelezaji mzuri wa mikakati ya benki hiyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji wake Arafat Haji.

“Ukuaji huu ni ushahidi wa utekelezaji mzuri wa mikakati yetu ambayo ililenga kuongeza rasilimali zetu kwa kuboresha usimamizi na ufanisi wa muundo wa kitabu chetu cha mizania (balance sheet), tukisaidiwa na huduma bora kwa wateja wetu, na azma ya timu ya wafanyakazi wetu katika kutimiza ahadi zetu kwa wateja na wadau wetu.” Alisema Haji kupitia taarifa ya benki hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji huyo, mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yametokana na sera imara za kiuchumi zinazolenga kuchochea uwekezaji na ukuaji wa biashara, zinazotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Alisema benki hiyo imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya uendeshaji wenye ufanisi ambapo uwiano wake wa gharama za uendeshaji na mapato (cost-to-income ratio) ulikuwa asilimia 46.49, kiasi ambacho hakijavuka matakwa ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) yanayoelekeza kiwango hicho kisizidi asilimia 50.

Ufanisi wa benki hiyo hauishii kwenye matokeo yake ya kifedha bali pia unathibitishwa na ongezeko kubwa la rasilimali zake ambapo jumla yake imeongezeka hadi kufikia thamani ya TZS trilioni 2.23, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 kutoka TZS trilioni 1.83 iliyoripotiwa mwezi Juni mwaka 2023.

Zaidi, mwenendo wa mikopo wa benki hiyo umekua hadi kufikia TZS trilioni 1.11, kutoka TZS bilioni 932 iliyoripotiwa mwezi Juni 2023, huku msingi wa amana ukishuhudia ongezeko kubwa la asilimia 31 ambapo umefikia kiasi cha TZS trilioni 1.77.

Akitoa maoni juu ya ukuaji huu, Bwana Haji alisema: “Ukuaji huu unaonyesha imani ambayo wateja wetu waliweka kwetu na uwezo wetu wa kukidhi mahitaji yao ya kifedha na kuwapa suluhisho za kusaidia mahitaji yao.”

Aidha, ubora wa mali (asset quality) wa benki hiyo ulibaki kuwa imara zaidi huku kiwango cha mikopo chechefu kikiwa ni asilimia 2.44% tu ikiwa ni chini ya kiwango cha asilimia 5 kilichowekwa na BOT.

Hatua hiyo inatajwa kudhihirisha uimara wa usimamizi na utambuzi wa hatari kwenye utoaji wa mikopo .

Pamoja na mafanikio yake ya kifedha, benki hiyo pia imepiga hatua kubwa katika kuongeza uwepo wake wa kidijitali na kuongeza matawi yake nchini. Hivi karibuni benki hiyo ilifungua matawi yake mapya kwenye mikoa ya Morogoro na Mbeya huku ikiongeza idadi ya mawakala 114 wake hadi kufikia jumla kuu ya mawakala 1,350 lengo likiwa ni kuimarisha zaidi upatikanaji na ufikiwaji wake kwa wateja kote nchini.

“Zaidi ya hayo, huduma zetu kwa njia ya simu (Mobile App) imefanyiwa maboresho makubwa na sasa wateja wanaweza kuipakua mtandaoni na kuipata kupitia simu zao za aina zote ikiwa ni azma yetu ya kutoa uzoefu wa kihuduma usio na dosari za kiteknolojia.” Aliongeza Haji.

Akizungumzia mipango ijayo, Haji alisema benki hiyo itabaki kuwa imara katika jitihada zake za kuimarisha nafasi yake katika soko na kuzidi malengo yake kwa mwaka 2024.
Alisema wataendelea kuangazia na kuboresha uzoefu na kuridhika kwa wateja, wakiboresha zaidi uwekezaji wao katika teknolojia ili kuchochea uvumbuzi, na kuendeleza muundo wa kitabu cha mizania imara ili kufanikisha ukuaji endelevu.

“Tuna uhakika kwamba tuko katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yetu ya baadaye. Ninatoa shukrani zangu kwa wafanyakazi wenzangu wote katika benki kwa kazi yao nzuri miaka yote. Juhudi zao zimekuwa ni za kutia moyo sana na ndio sababu ya matokeo mazuri na ukuaji unaodumu wa benki, na tuna uhakika kwamba tuko katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yetu ya baadaye.” Alipongeza.

Aidha, aliongeza shukrani na pongezi zake kwa wateja na wadau wa benki hiyo kwa msaada wao endelevu katika ukuaji na maboresho makubwa ya benki.

About The Author