July 18, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Vodacom, Jubilee Allianz Tanzania wajipanga ‘kuinogesha’ NBC Dodoma Marathon, wakabidhiwa jezi

 

WADHAMINI wa mbio za NBC Dodoma Marathon Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania na Kampuni ya Bima ya Jubilee Allianz Tanzania wamesisitiza dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ili kuhakikisha mbio hizo zinatimiza makusudi yake ya uwajibikaji kwa jamii huku pia zikitoa hamasa na furaha iliyokusudiwa kwa washiriki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Dhamira za wadau hao wawili zimewekwa wazi leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Rayson Foya waliotembelea makao makuu ya kampuni hizo wadhamini kwa lengo la kukabidhi jezi maalum na vifaa vitakazotumiwa na washiriki wa mbio hizo ikiwa ni ishara ya muaandaaji huyo kutambua na kuheshimu mchango wao katika kufanikisha mbio hizo.

Mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 27, mwaka huu jijini Dodoma zinalenga kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200 pamoja na kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini.

Mapema wakiwa makao makuu ya Jubilee Allianz Tanzania, Foya na ujumbe wake akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa benki ya NBC, Godwin Semunyu walipata wasaa wa kuzungumza na kukabidhi vifaa hivyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Jaideep Goel, ziara ambayo pia iliendelea kwa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania na kupokelewa na maofisa waandamizi wa kampuni hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi wa Biashara, Nguvu Kamando.

Katika mazungumzo yake na wadau hao, Foya pamoja na kuwashukuru kwa udhamini wao muhimu katika mbio hizo alisisitiza kuhusu umuhimu ushirikiano baina ya taasisi mbalimbali katika kufanikisha nia ya pamoja ambayo ni kurejesha kwa jamii kupitia jitihada mbalimbali zinazolenga kupambana na changamoto zinazowagusa wanajamii hususani katika masuala yanayohusu afya.

“NBC Dodoma Marathon sio tu tukio la kimichezo bali pia ni jukwaa la matumaini ya maisha kwa watanzania. Ushiriki wa wadau hawa wakiwemo Vodacom Tanzania na Jubilee Allianz na wadau wengine wote tuliowatembelea na tutakaoendelea kuwatembelea umekuwa ni chachu muhimu katika kufanikisha kusudi leo hilo mihumu…tunawashukuru sana’’ alisema Foya

Kwa upande wake Kamando pamoja na kupongeza ubora na ubunifu wa jezi hizo, aliishukuru benki hiyo kwa namna inavyoandaa tukio hilo kwa weledi wa hali ya juu hatua ambayo imeongeza mvuto wake kiasi cha kuwavutia maelfu ya washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.

“Zaidi tunawapongeza NBC kwa namna ambavyo wamekuwa wakilitumia tukio hilo kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikisha makusudi muhimu ya mbio hizi. Ni kupitia kuridhishwa kwetu na nia pamoja na uratibu wa mbio hizo ndio imekuwa sababu ya Vodacom Tanzania kuendelea kuziunga mkono kama wadau muhimu huu ukiwa nim waka wa pili sasa na tunaahidi kuendelea kuziunga mkono zaidi katika misimu mingine ijayo,’’ alisema.

Usajili wa mbio hizo unaendelea kupitia tovuti ya www.events.nbc.co.tz ambapo washiriki wanatakiwa kuchangia kiasi cha TZS 45,000 kwa usajili wa mtu mmoja mmoja au 42,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu 30 au zaidi.

About The Author

error: Content is protected !!