July 12, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Msitumie kalamu zetu kuligawa taifa – Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, amewataka waandishi wa habari nchini Tanzania, kuwa makini na ili kutoligawa taifa. Anaripoti Asha Bani, Dar es Salaam … (endelea).

Alisema, “vyombo vya habari ni kama maji usipoyatumia kuyanywa utayatumia kuoga usipoyatumia kuoga yatatumika kumwagiwa ukizimia.”

Alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili mchango wa sekta ya habari nchini, kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Dk. Biteko alisema, ni lazima kushirikiana na vyombo vya habari kwa maslahi ya nchi. Huwezi kuvikwepa, ni vizuri kila mtu akatimiza wajibu wake na kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.

“…tunasipokuwa makini, waandishi habari na vyombo vyao wanaweza kugawa taifa letu kwa sababu kinaweza kugombanisha dini na hata vita,” alieleza Biteko.

Hata hivyo, naibu waziri mkuu amesema, kutokafautiana kwenye maoni si uhalifu na wala sio dhambi.

“Kila mtu aamini kile anachokiamini na kama kuna mtu anapenda Simba aachwe na kama anapenda Yanga basi aachwe pia,” ameeleza.

Aliongeza, katika kipindi hiki cha uchaguzi kuna haja ya kila mtu kumvumilia mwingine ili taifa liweze kuwa salama na kusonga mbele.

“Baada ya uchaguzi kila mtu mwenye uongozi abaki na uongozi wake na mwaandishi wabaki na uandishi wao, ili kazi za kujenga taifa baada uchaguzi ziendelee,” alifafanua.

Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi (DCP), David Misime alisema, uchaguzi ni kipindi muhimu sana na kila mtu anashiriki ili kuweza kupata haki za msingi.

Aliwaasa waandishi wa habari kuepuka kutoa taarifa za uchochezi.

Alisema, ni wajibu wa jeshi la Polisi kusimamia sheria na kuhakikisha zinafuatwa na kuheshimiwa.

About The Author

error: Content is protected !!