
KAMPUNI ya Bima ya Sanlam Insurance, mmoja wa wadhamini muhimu mbio za NBC Dodoma Marathon, imesisitiza dhamira yake ya kutumia mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 27 mwaka huu jijijni Dodoma kufikisha elimu zaidi kuhusu umuhimu wa bima kwa wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo wanamichezo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Dhamira hiyo imewekwa wazi na Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo Mika Samwel wakati wa hafla fupi ya utambulisho rasmi wa kampuni hiyo kama mmoja wa wadhamini muhimu wa mbio hizo mara sita mfululizo.
Hafla ya utambulisho huo imefanyika leo jijini Dar es Salaam ikihusisha maofisa waandamizi kutoka kwa mdhamini huyo pamoja na maofisa kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambao ndio waandaaji na waratibu wa mbio hizo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Tatiana Masimba pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa benki ya NBC, Godwin Semunyu.
“Pamoja na kuunga mkono agenda kuu za mbio hizi ambazo ni kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200 pamoja na kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini, Sanlam Insurance tumejipanga kuhakikisha kwamba tunatumia vema mbio hizi katika kufikisha elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima mbalimbali ikiwemo bima ya afya kwa makundi tofauti ya wananchi wakiwemo wanamichezo,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Mika bado jamii wakiwemo wadau wa michezo wanakabiliwa na changamoto ya kutofikiwa kikamilifu na elimu kuhusu faida na umuhimu wa bima hivyo kampuni hiyo imejizatiti kutumia vema tukio hilo na mengine mengi kuhakikisha wapenyeza elimu kuhusu umuhimu wa aina mbalimbali za bima ikiwemo bima ya afya, bima ya maisha na bima ya biashara mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wafanyabiashara na wadau wa michezo.
Akizungumzia ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili, Semunyu pamoja na kuipongeza kampuni hiyo kwa kuendeleza udhamini wake kwa mwaka wa sita mfululizo alisema benki hiyo kama muandaaji wa mbio za NBC Dodoma Marathon wamejipanga kuhakikisha kwamba wanatumia mbio hizo kuunga mkono pia dhamira ya kampuni ya Sanlam Insurance ya kufikisha elimu ya bima kwa jamii.
“Kama ambavyo wenzetu wa Sanlam Insurance wameona umuhimu wa kushirikiana nasi katika kufanikisha mkakati wa kukusanya kiasi cha Sh. 700 milioni ili kufanikisha agenda kuu ya mbio hizi nasi pia tumejizatiti kuhakikisha kwamba tunatumia kila nafasi tunayoipata katika kipindi chote cha hamasa za mbio hizi kutoa elimu kuhusu umuhimu wa bima kwa makundi yote ya kijamii wakiwemo wadau wa mchezo huu wa riadha pamoja michezo mingine ikiwemo mpira wa miguu ambapo sisi ni wadau muhimu,” alisema Semunyu.
Akizungumzia mafanikio ya kimichezo na kiuchumi ya mbio hizo tangu kuanzishwa kwake huu ukiwa ni msimu wa sita sasa, Tatiana alisema pamoja na kuchochea ajira kwa wadau wa mchezo huo pamoja na kuwa chanzo cha kipato kwa wanariadha hususani washindi, mbio hizo zimekuwa zikitumiwa na wanaridha wa ndani kama namna bora ya kujiandaa na mashindano makubwa ya kimataifa kutokana na ushiriki wa wanaridha wengi kutoka nje ya nchi wanaoshiriki mbio hizo kila mwaka.
“Na hadi kufikia sasa mwitikio wa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi ni mkubwa huku usajili wa mbio hizi ukiendelea kupitia tovuti ya events.nbc.co.tz ambapo washiriki wanatakiwa kuchangia kiasi cha TZS 45,000 kwa usajili wa mtu mmoja mmoja au 42,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu 30 au zaidi.
ZINAZOFANANA
Ligi Kuu Uingereza kurejea Agosti 15, wabashiri wa Meridianbet kaa tayari
Real Madrid vs Al Hilal kukupatia faida mara 2 leo
Kiwanda cha GF chatengeneza magari 4,000 nchini