
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata baadhi ya waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, kwa tuhuma za kukaidi agizo la serikali la kulifuta kanisa hilo na kuendelea kufanya ibada kinyume cha sheria. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).
SACP Jumanne Muliro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, amesema watu hao wamechukuliwa na polisi ili kutoa maelezo ikiwa walikuwa hawajafahamu maelekezo ya serikali au walikaidi makusudi agizo hilo kwa lengo la kuzua fujo.
“Wakati tukielekeza nini cha kufanya (kufungwa kwa kanisa la Askofu Gwajima) kulingana na maelekezo ya kisheria, kuna baadhi ya watu walikuwa wanafanya mambo ya kutoelewa, kwahiyo ikabidi tuwachukue na tunaendelea kuongea nao kujua kweli walikuwa hawaelewi kilichokuwa kinatekelezwa au walikuwa wanafanya tu kukataa kwa maana ya kutaka kusababisha fujo,” amesema Kamanda Muliro.
Kamanda Muliro ameeleza kuwa Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kusimamia sheria na amani, na kwamba hatua ya kufungwa kwa kanisa hilo ni utekelezaji wa maamuzi ya kisheria yaliyotolewa na mamlaka husika. Amesisitiza kuwa endapo kanisa au viongozi wake watataka kurejeshwa kwenye shughuli zao za awali, basi wanapaswa kufuata utaratibu wa kukata rufaa kwa mujibu wa sheria.
“Wanaweza kukata rufaa kwa mamlaka za kisheria na kama wakiruhusiwa, sisi polisi tutaendelea kuzingatia sheria. Hatuna tatizo na yeyote anayetii sheria,” amesema.
Tarehe 2 Juni, 2025, Serikali ilitangaza kulifuta rasmi Kanisa la Ufufuo na Uzima, ikieleza kuwa limekiuka Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa, hatua ambayo imeelezwa kuwa ililenga kuichonganisha Serikali na wananchi.
ZINAZOFANANA
Tundu Lissu apinga kesi yake kuahirishwa tena
Idadi ya waliofariki ajali ya Same yafikia 39
DAS Kinondoni aipongeza MONTI International kwa kuibua, kulea vipaji vya watoto