April 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yaeleza mchango wa Sekta binafsi nchini

 

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Stanislaus Nyongo, ametoa wito kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya nchi kwani zina mchango mkubwa kwa taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Ameyasema hayo leo Aprili 16, 2025 wakati akifungua Mdahalo wa Kitaifa ulioandaliwa na Media Brains kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) wenye Mada Kuu ya Ubia wa Sekta ya umma na Sekta Binafsi katika Muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Amesema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika maeneo mbalimbali kama vile sekta ya usafirishaji ikiwemo bandari, sekta ya nishati na usafiri wa umma pamoja na huduma za kijamii.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia, Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira bora, wezeshi na shindani kwa sekta binafsi ili kufanya kazi kwa ufanisi.

“Na ili tufanikiwe katika jambo hili, lazima tujipange na kuandaa midahalo kama hii ili kubadilisha fikra zetu na kujipanga vizuri. Kwa hiyo nitoe wito kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mikakati ya nchi,” amesema.

Amefafanua kuwa, katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta binafsi imepewa kipaumbele katika kuchangia kwenye Dira hiyo.

“Mdahalo huu umekuja wakati ambapo Taifa letu limeingia katika hatua muhimu ya kupanga mustakabali wa Maendeleo yake kwa miongo ijayo kupitia maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

“Tunampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kutumia wananchi kukusanya maoni ya Dira hii. Tunatambua kuwa safari ya maendeleo ni endelevu kwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 iko katika hatua za utekelezaji na serikali imeanza katika maandalizi ya Dira mpya,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila amesema uchumi wa nchi hauwezi kujengwa bila kuzishirikisha sekta binafsi.

Amesema dunia nzima inafanya ubia na masuala hayo yamekuwa ni ajenda kubwa kwenye mijadala ya uchumi duniani.

“Duniani kote imekuwa ni ngumu kwa serikali hizi kutekeleza matarajio ya wananchi kwa kutumia kodi na mikopo… na ushahidi wake ni takwimu za hali ya uchumi wa dunia. Uchumi wa dunia kufika mwaka jana Novemba ulikuwa takribani Trilioni Dola za Marekani 115, lakini deni la serikali zote duniani ilikuwa takribani Trilioni Dola za Marekani 102.

“Deni la dunia yote kwa maana ya serikali, sekta binafsi na kaya ilikuwa ni zaidi ya Dola Trilioni 315… tafsiri yake ni kwamba uchumi wa dunia unaendeshwa kwa mikopo,” amesema.

Kafulila amefafanua kuwa uchumi wa Dunia zaidi ya asilimia 90 ni mikopo ambapo kwenye upande wa Afrika mikopo ya serikali kwa uchumi ni takribani asilimia 67 na kwa Tanzania ni asilimia 47.

“Unaweza ukaona pamoja na maneno kwamba deni la serikali linaongezeka, lakini utaona Tanzania kuna utofauti mkubwa, na hii ni kielelezo kuwa serikali ya awamu ya sita inasimamia vizuri hali ya uchumi,” amesema.

Amebainisha kuwa mdahalo huo ni sehemu ya kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu masuala ya ubia na kuweza kutafakari kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Hii ni fursa kubwa ya kujadili namna ambavyo tunataka kuwa na uchumi wa nchi yetu kwenda mwaka 2050. Lazima kufungua uchumi kwa kuongeza ubia sekta za ndani na nje kushiriki katika kujenga uchumi na serikali ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa nchi,” ameongeza.

Awali akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Chagu Nghoma, kuna fursa nyingi ya uwekezaji za kukuza uchumi katika mkoa huo, ikiwamo sekta ya uchumi wa buluu ukilenga ufugaji wa samaki na shughuli nyingine zinazofanyika katika Ziwa Victoria.

Amesema pamoja na hayo pia kuna maeneo mengi yanayofaa kwa ufugaji wa mifungo kama vile ng’ombe, mbuzi.

Ameeleza kuwa kuhusu uchumi wa buluu kuna ufugaji wa samaki ambayo inahitaji kwa kiasi kikubwa uwekezaji wa viwanda na kuwekeza katika chakula cha samaki, pia viwanda vya nyama vinahitajika zaidi.

“Mkoa wa Mwanza una maeneo mengi ya uwekezaji na upo tayari kuyatoa maeneo hayo kwa watu binafsi na serikali. Uchumi wa mtu unaanza na mtu binafsi, ni lazima kufikiria nini unataka kufanya katika kuboresha uchumi binafsi na nchi,” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!