
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemkabidhi funguo Jaji Mkuu wa Tanzania Ibrahim Hamis kama ishara ya ufunguzi wa majengo ya mahakama kubwa barani Afrika ya Tanzania yaliyojengwa eneo la Tambukareli mkoani Dodoma. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dodoma…(endelea)
Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 5 Aprili 2025 ikiwa ni sehemu ya mpango wa maboresho ya miundombinu ya Mahakama ili kuongeza ufanisi na upatikanaji wa haki kwa wakati.
Akizungumza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Elisante Ole Gabriel amesema Jengo hilo linaweka rekodi ya kuwa Jengo kubwa zaidi barani Afrika na la sita kwa ukubwa duniani.
“Jengo hili lipo kwenye kiwanja ambacho kina ukubwa wa hekta 18.9 sawa na hekari 45.5. Rais, jengo hili limejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 129.7 na lina ukubwa wa ghorofa tisa na jumla ya sakafu zake ukizijumlisha inakuwa na ukubwa wa mita za mraba za square Mita 63, 244,” amesema Elisante.
Amefafanua, “jumla ya sakafu yaani zile mita za mraba 63,244 ni sawa na shamba la kawaida la hekari 13 kwahiyo hili ni jengo kubwa sana na kwa ulinganifu na majengo mengine duniani.
“Jengo la kwanza kwa ukubwa wa mita za mraba kwenye sakafu lipo barani Asia likiwa na ukubwa wa sakafu za mraba Mita 147,000, la pili mpaka la sita yapo ulaya ambapo la sita lina ukubwa wa sakafu 53,000 na letu hili unalotuzindulia hapa Rais lina ukubwa wa sakafu za mraba mita 63, 244. Maana yake Rais leo jengo hili unalotuzindulia leo hapa linakuwa la sita kwa ukubwa wa sakafu na la kwanza barani Afrika,” amesema Elisante.
Aidha, Elisante amesema jengo hilo ambalo ni kati ya majengo makubwa zaidi ya Mahakama duniani na kubwa zaidi barani Afrika lina vifaa vya kisasa vya TEHAMA pamoja na eneo maalum kwa ajili ya kutua Helkopta.
Pamoja na hayo amesema kuwa serikali ilitenga kiasi cha Sh.146. 16 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo imekamilika na mingine ikiendelea kutekelezwa.
ZINAZOFANANA
PZG-PR yashinda tuzo ya ‘Best PR Agency 2024’ nchini Tanzania
TRA yawashukuru Wahariri kwa kuhamasisha ulipaji kodi
TEF yawarejesha tena Balile, Machumu