
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ameelezea dhamira ya uongozi wa mkoa huo kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kuandaa hafla kubwa ya futari mahususi kwa makundi maalum wakiwemo watoto yatima zaidi ya 600 kutoka vituo vyote vya kulelea watoto hao mkoani humo ili kutoa wasaa kwao kufurahia pamoja mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
RC Mtanda alielezea dhamira hiyo mwisho mwa wiki aliposhiriki hafla ya futari iliyoandaliwa na benki ya NBC mahususi kwa wateja wake wa Kiislamu jijini Mwanza. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini, wateja, viongozi wa serikali pamoja wafanyakazi wa benki ya NBC huku Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, ,Rayson Foya akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi kwenye hafla hiyo.
Akizungumzia mpango wa hafla ya watoto yatima jijini humo mbele ya wageni waalikwa, RC Mtanda alisema itahusisha jumla ya vituo 16 vya kulelea watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu ili kutoa wasaa wa kwa wadau mbalimbali jijini humo ikiwemo benki ya NBC kushiriki futari ya pamoja na watoto hao.

“Baada ya hafla hii ya NBC mahususi kwa ajili ya wateja wao hatua inayofuata ni kushiriki pamoja futari kama hii na moja ya kundi lenye uhitaji kama ambavyo miongozo ya dini yetu inavyotuongoza. Badala ya kila taasisi kuandaa shughuli kama hizi kwa kujitegemea peke yao tumeona ni vema wote tuwe na shughuli ya pamoja ili kutoa wasaa kwa wadau wenye nia kama NBC kuweza kuwafikia walengwa wenye uhitaji haswa’’ alisema.
Pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa ushirikiano wake na wateja wake wenye imani ya kiislamu hususani katika mwezi huu wa Ramadhani huku akisisitiza umuhimu wa mahusiano yanayogusa na kuheshimu misingi ya imani za dini kwa wateja wa benki, RC Mtanda pia aliishukuru benki hiyo kupitia matawi yake ya Mwanza na Nyanza kwa namna inavyoshirikiana na serikali katika kufanikisha mipango ya maendeleo hususani katika nyanja ya elimu.
Kwa upande wake, Foya alisisitiza juu ya umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya benki hiyo na wadau wake muhimu ikiwemo Serikali na wateja. Alitumia fursa hiyo kuzungumzia huduma maalum inayotolewa na Benki ya NBC kwa wateja wa Kiislamu inayojulikana kama La Riba, ambayo inazingatia mafundisho ya Kiislamu kuhusu riba.
“NBC tunatambua kuwa Ramadhan ni nguzo muhimu ya imani ya Kiislamu, wakati wa ibada, upendo, na sadaka. Hivyo kwa kutambua thamani hiyo, futari hii ni ishara ya kuthamini mahusiano yetu sisi, wateja wetu na wadau wetu wote ikiwemo serikali, ikiwa ni njia mojawapo ya kushirikiana pamoja baraka za mwezi huu,’’ alisema Foya.
Kwa mujibu wa Foya, ushirikiano umekuwa ukiambatana na utoaji wa huduma bora kwa wateja wa benki hiyo kwa kuzingatia mahitaji maalum.
“Katika kuthibitisha dhamira yetu hii ni hivi karibuni tu tulitambulisha rasmi ‘App yetu ya NBC Kiganjani ikiwa na maboresho makubwa zaidi kulingana na mahitaji ya wateja wetu ambao sasa wanaweza kufungua akaunti popote walipo, kufanya malipo ya serikali (GEPG), kununua umeme (LUKU), na kulipa ankara mbalimbali kwa urahisi,’’ alisema.
Hafla hiyo pia ilihusisha utoaji wa zawadi kwa wageni waalikwa. Kwa wateja wa Kiislamu wa benki ya NBC jijini Mwanza, hafla hiyo ilikuwa fursa nzuri ya kufurahi pamoja na kujenga uhusiano mzuri miongoni mwao na benki hiyo.
ZINAZOFANANA
Siri iliyojicha, kasino inavyotoa utajiri kirahisi
Jinsi ya kupiga pesa ndefu kasino
Exim yaandaa futari Tanga, Zanzibar kuimarisha uhusiano wa kijamii