March 10, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mramba afafanua mradi wa umeme kutoka Ethiopia

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba

 

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa inayoikumba mikoa ya kaskazini mwa Tanzania ni upungufu wa msongo wa umeme (voltage drop), hali inayosababishwa na umbali mrefu uliopo kutoka mtambo wa uzalishaji mpaka kwa mtumiaji. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu 10 Machi 2025, Mramba amesema kuwa hatua ya ununuzi wa umeme huo utaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya kanda ya kaskazini ambayo inatumia umeme unaozalishwa mikoa ya kusini.

“Umeme mwingi wa Tanzania unazalishwa Kusini, katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, na Iringa. Hivyo. ili kufikia mteja wa kaskazini umeme huu unasafiri hadi kilomita 700 kwa baadhi ya maeneo, kwahiyo mpaka kufika kwa umeme huo kunatokea (voltage drop) kupungua kwa nguvu za msongo wa umeme kabla ya kufika kwa mtumiaji wa mwisho,” ameeleza Mramba.

Ameeleza kuwa njia pekee ya kutatua tatizo hilo ni kuweka mtambo wa kuzalisha umeme karibu na maeneo hayo au kuingiza umeme kwenye mikoa hiyo kutokea mahali pengine, hivyo makubaliano ya serikali ni kuingiza kutoka Ethiopia kupitia Kenya na kuingilia mpaka wa Namanga.

Amesema kuingia kwa umeme huo mikoa ya kaskazini utasaidia kuongeza megawati ambazo zinapungua hadi kufikia kwenye kiwango chake jambo ambalo litamaliza changamoto ya upotevu wa umeme.

Akifafanunua zaidi amesema kuwa jinsi umeme utakavyokuwa ukinunuliwa, umeme wa Ethiopia utaingizwa kwenye mfumo wa Gridi ya Kenya na kisha Kenya itatoa megawati hizo kuja kwenye gridi ya Tanzania ikifidia umeme ulioingizwa kutoka nchini Ethiopia.

“Makubaliano haya yako ya pande mbili kuna wakati sisi tutanunua umeme na kuna wakati tutatumia njia hiyo hiyo kuuza umeme kwa nchi jirani, tunavyoangalia hali ya Kaskazini kwa sasa tunaona sisi tutachukua zaidi kuliko kupeleka lakini kuna wakati na wenyewe wanaweza wakahitaji umeme na tutatumia njia hiyo hiyo kuwapelekea” amesema Mramba.

Ameongeza kuwa kununua na kuuziana umeme kwa nchi si jambo geni na Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikinunua umeme nchini Uganda kwa ajili ya Mkoa wa Kagera, nchini Zambia kwa ajili ya Mkoa wa Rukwa na nchini Kenya kwa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Tanga hususani ya mpakani.

About The Author

error: Content is protected !!