
Rais Samia Suluhu Hassan
KWA mujibu wa taarifa ya Africa CDC, Tanzania imepunguza kwa asilimia kubwa vifo vya wajawazito ambapo, kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 hadi 104 mwaka 2022. Takwimu ambazo zimetafsiliwa kama hatua kubwa katika kulinda afya ya Mama na Mtoto. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hatua hiyo imekuja kufuatia uwekezaji katika miradi mikubwa iliyolenga kuboresha huduma za afya, hasa kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga.
Baadhi ya hatua zilizochangia kupungua kwa vifo vya wajawazito ni, ujenzi na Uboreshaji wa Miundombinu ya Afya kwa kuboresha hospitali za wilaya, vituo vya afya, na zahanati ili kuhakikisha huduma za uzazi zinapatikana kwa urahisi.
Ujenzi wa hospitali mpya 100 zilizojengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku vituo vya afya zaidi ya 400 vikiboreshwa na kupatiwa vifaa tiba vya kisasa.
Hatua zingine ni upatikanaji wa Vifaa Tiba kama mashine za Ultrasound, na Dawa Muhimu za dharura kwa wajawazito, mafunzo kwa wahudumu wa Afya ikiwemo wakunga, na madaktari kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa kutosha kushughulikia changamoto zinazohusiana na uzazi.
Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya wanawake na watoto wachanga 12,000 wameokolewa kupitia mfumo huu. M-Mama unatumia teknolojia ya kisasa inayowezesha wagonjwa kupewa usafiri wa haraka kutoka maeneo ya mbali kwenda katika hospitali zinazotoa huduma za uzazi salama. Mfumo huu umetambuliwa kimataifa kama mfano bora wa ubunifu wa huduma za afya barani Afrika.
Katika hatua nyingine iliyopelekea Tanzania kutambulika kupiga hatua katika sekta hiyo, ni Rais Samia Suluhu Hassan kupokea tuzo ya The Global Goalkeeper aliyotunukiwa na Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation, tuzo ambayo ambayo hutolewa kwa kiongozi aliyeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya na maendeleo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Rais Samia alisisitiza kuwa ni ushindi wa Watanzania wote, hususan wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele katika kupambana na vifo vya wajawazito. Alisema serikali yake itaendelea kuongeza jitihada ili kufikia lengo la kupunguza vifo vya wajawazito hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
ZINAZOFANANA
Korea Kusini kuchangia USD Mil 104 maboresho ya Muhimbili
Muhimbili kuvuna mifupa kwa ajili ya kutengenezea taya ya chini kwa Mil 6.2
MOI yaokoa Bil 150 kwa miaka minne, kuanzisha benki ya mifupa