March 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ACT Wazalendo kuwashitaki wateule wa Rais Mwinyi

Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban

 

CHAMA cha ACT Wazalendo kinachukua hatua ya kushitaki kibinafsi viongozi wateule wa Rais wanaotuhumiwa kutoa amri za kukamatwa na kuwekwa ndani wanasiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwanasheria Mkuu wa chama, Omar Said Shaaban katika mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika Ofisi Kuu ya Chama Vuga mjini hapa.

Omar ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mshirika katika Kampuni ya Uwakili nchini amesema chama kitagharamia kesi ambazo walalamikaji imethibitika hawana uwezo.

Hatua hii inakuja kipindi hichi ambacho taratibu za kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2025 zimeanza baada ya kutangazwa na Tume za Uchaguzi nchini.

Hatua ya kwanza: Kufuatilia matukio ya kihalifu dhidi ya ubinaadam na kunyima uhuru mwananchi yaliyoanza kutokea.

Pili: Kuandikia rasmi viongozi wa kisiasa wanaotuhumiwa kwa hayo.

Tatu: Kuwasiliana na mawakili watakaoshirikiana na Ofisi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Chama.

Tayari mawakili wamemwandikia Sadifa Juma Sadifa, kumtaka amlipe mwananchi aliyeshambuliwa, kuumizwa na kuwekwa Kituo cha Polisi kwa amri yake.

Sadifa ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, lakini anatajwa kwa hadhi yake binafsi kwa kile alichokisema Mwanasheria Omar “maovu aloyafanya ameyafanya binafsi, hakutumwa na mamlaka iliyomteua.”

Sadifa anatuhumiwa kuelekeza kushambuliwa kwa Said Ali na kuswekwa kituo cha Polisi Bububu.

Said alijeruhiwa na kupata maumivu makali kutokana na kipigo ambacho Sadifa alitoa amri akitumia kivuli cha Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.

Tukio hilo ni muendelezo wa matukio mengi ya kuvunja sheria yanayofanywa wakati huu Tume ya Uchaguzi Zanzibar ikiendesha kazi ya uandikishaji wapigakura wapya wa kujumuishwa kwenye Daftari la Kudumu la WapigaKura Zanzibar.

Baada ya kukamilisha uandikishaji kisiwani Pemba tarehe 13 Februari, kazi hiyo inaendelea Unguja ambako kwa Wilaya ya Magharibi B inatarajiwa kukamilika kesho tarehe 6 Machi na kuhamia Mkoa wa Kusini Unguja.

Malalamiko ya matukio ya utumiaji nguvu ya mamlaka yameripotiwa kwingi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya wakitajwa kusimamia kwa nafasi zao mikakati ya kusaidia CCM.

Baada ya hali ya afadhali Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Simai Msaraka aliripotiwa kupora kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi mwananchi, hali imekuwa tofauti Magharibi A ambako pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT, Khadija Anuwar alikatekwa na mazombi na hatimaye kupelekwa Polisi Mwera taarifa ziliposambazwa mitandaoni.

Kwenye siku yake ya kwanza jana, uandikishaji ulianza kwa shoo ya askari wa vikosi vya ulinzi vya SMZ kutumia gari zilizoondolewa namba za usajili zikiwa zimejaa askari wenye silaha zikipita mitaani huku zikiliza ving’ora.

Muandishi wa habari hizi alishuhudia msafara wa gari tano ukipita barabara ya Fuoni Meli Tano kwendea Kwarara ambako kipo Kituo cha uandikishaji cha Tanwir katika Shehia ya Kijitoupele, Jimbo la Pangawe.

Wakati vikosi vikihanikiza barabara kuu za majimbo matano ya Wilaya ya Magharibi B, Jeshi la Polisi limechukua jukumu lake la kulinda usalama ndani ya vituo vya uandikishaji. Hakuna misafara ya Polisi barabarani wala mitaani na hakujaripotiwa matumizi ya nguvu popote.

About The Author

error: Content is protected !!